loader
Picha

Miradi ya kimkakati yaongeza mapato

SERIKALI imesema yapo manufaa ya muda mfupi yatokanayo na ujenzi wa miradi ya kimkakati na kutoa mfano wa ujenzi wa SGR kwamba unaingiza Sh bilioni 5.2 kwa mwezi kama malipo hapa nchini.

Aidha imesema kwamba zaidi ya wakandarasi 500 wa hapa nchini wanafanya shughuli mbalimbali katika mradi huo wa kimkakati.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ameyasema hayo wakati anajibu hoja za wabunge hasa manufaa ya muda mfupi ya miradi ya kimkakati.

Serikali katika miradi yake mikuu ya kimkakati inajenga reli ya SGR, inakarabati reli ya kati (meter gauge), inaimarisha kampuni ya ndege na pia kupanua uwezo wa bandari.

Alisema reli hiyo itakapomalizika ambayo inatarajia kusafirisha mizigo tani za metriki milioni 17 kutoka nchi za Congo DRC, Uganda, Burundi na Rwanda na kuingizia taifa pato kubwa zaidi.

Alisema kwamba fedha hizo zinalipwa hapa nchini kwa ajili ya shughuli mbalimbali pamoja na malipo ya wafanyakazi na huduma nyingine.

Aidha alisema kwamba Kampuni ya ATCL itaendelea kutanua mbawa zake kufikia maeneo mengi zaidi huku viwanja vyua ndege vikiendelea kuboreshwa na kuwekewa taa.

Alikanusha madai kwamba fungu 62 kuhusu ununuzi wa ndege na uendeshaji wake umehamia Ikulu na kusema kwamba fungu hilo litabaki kuhudumia ndege hizo ndio maana limeombewa fedha za ununuzi wa ndege na maandalizi ya awali.

Aidha akizungumzia mradi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo ilitokea vuta nikuvute baada ya Mbunge wa Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa (CCM) kuondoa shilingi na kuomba Bunge lijadili, hatima ya mradi huo, Waziri Kamwelwe alisema kwamba mazungumzo yanaendelea na kwamba anatarajia yatakuwa na mwisho mzuri.

Alisema barua waliyoandikiwa China Merchants imechukua muda mrefu kujibiwa lakini kwa sasa wamejibu na kwamba wapo tayari kwa mazungumzo hasa vifungu viwili ambavyo vinaonekana kuondoa maslahi na mamlaka ya nchi.

Bunge jana pia lilipata ufafanuzi mbalimbali kuhusu miradi ya ujenzi wa Reli ya Kusini (Mtwara hadi Mbambabay- Mchuchuma) na Kaskazini (Tanga hadi Musoma) ambapo Waziri wa Fedha, Philip Mpango alisema kwamba wanataka kuitekeleza miradi hiyo katika mpango wa kushirikisha sekta binafsi maarufu kama PPP.

Pia serikali imesema inapokea ushauri wa matumizi ya ununuzi wa hisa na uwekaji rehani (bond) ili kupata fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya kimkakati. Bunge lilipitisha bajeti ya wizara hiyo jana na leo Wizara ya Viwanda na Biashara itawasilisha bajeti yake.

ILI kukabiliana na ugonjwa wa Covid- 19 unaosababishwa na virusi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi