loader
Picha

Bandari Bagamoyo moto bungeni

WABUNGE wameonesha kukerwa na kutokamilika kwa mazungumzo na kampuni ya China inayotaka kuwekeza bandari ya Bagamoyo kwa takribani miaka saba sasa.

Aidha wamesema mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa miaka saba sasa huku nchi nyingine zikikamilisha miradi kama hiyo katika muda mfupi ni dalili kwamba kundi linalofanya mazungumzo limeshindwa kutekeleza wajibu wake na kuiweka nchi katika safari nzuri ya kiuchumi.

Pia wamesema kitendo cha kushindwa kukamilisha mazungumzo hayo kwa sababu zilizoelezwa kwamba ni kwa manufaa ya taifa hazina mashiko.

Wakichangia katika hoja ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyotolewa bungeni Alhamisi iliyopita wabunge waliitaka serikali kukamilisha mazungumzo hayo kwa manufaa ya taifa.

Wakati wa uwasilishaji wa hoja ilielezwa kuwa mradi huo umesimama kwa kuwa masharti yaliyowekwa katika kufikia mkataba ikiwamo kuachiwa jukumu la tozo katika bandari na pia suala la uanzishwaji wa viwanda katika eneo la Bagamoyo na Tanga kuachiwa kampuni hiyo.

Pamoja na kuitaka serikali kujieleza, baadhi ya wabunge wamesema kwamba Bunge liunde kamati ya kuishauri serikali na pia kuwa na nafasi kujadili uamuzi wa serikali inapoachana na miradi mikubwa ya kimkakati baada ya kutumbukiza fedha za umma hapo.

Wakiungwa mkono na Spika Job Ndugai ambaye alizungumza kwa dakika moja akichangia hoja za wabunge wengine umuhimu wa mradi huo; yeye alibaki akishangaa kilichotokea mpaka serikali ikauacha.

Wabunge walisema kwamba bandari ya Dar es Salaam kwa sasa pamoja na upanuzi wote, imefikia mwisho na haiwezi tena kubeba meli mpya za kizazi cha nne na kuendelea.

Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) alisema inafaa Bunge na wananchi kuihoji serikali pindi inapoacha miradi mikubwa yenye tija kwa taifa kama mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

“Kwanini kama nchi tunaacha mradi kama huu...” alisema Ally na kuongeza mradi wa bandari haikuwa ujenzi wa bandari pekee, bali kutengeneza ukanda maalumu wa uchumi wa Bagamoyo ambao ungeleta ajira na kuifanya Dar es Salaam ipumue.

Amesema kwa mujibu wa mradi huo mji wa Bagamoyo ungelikuwa wa kisasa zaidi na kutoa nafasi ya ukuaji wa nchi.

Alisema bandari hiyo ambayo ingelikuwa kubwa katika Afrika na ya pili kufuatia bandari ya Rotterdam, Uholanzi ingeneemesha uchumi wa nchi kutokana na idadi za meli zilizokuwa zikitakiwa kutia nanga.

Alisema wananchi wangefaidika kwa kuuza bidhaa mbalimbali ikiwamo matunda, maji na bidhaa nyingine zinazohitajika katika meli. Alisema haoni sababu ya kucheleweshwa kwa mradi huo wakati umepangwa kutekelezwa na nchi mbili rafiki za Oman na China.

Spika Ndugai yeye akihoji kuna nini bandari ya Bagamoyo alisema kwa jinsi walivyopewa maelezo nchini China wakati wa moja ya ziara huko, mradi huo ni mkubwa mno na haiwezekani kuuachia hivi hivi tu.

Alisema walipofanya ziara Shenzen, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki aliwafikisha Makao Makuu ya kampuni hiyo inayomilikiwa na serikali ya China Merchant na kupata maelezo.

Alisema katika maelezo hayo waliambiwa kuna haja ya kuharakisha mazungumzo kwa kuwa wakuu wa Bodi wenye moyo wa dhati na Tanzania walikuwa wanakaribia kustaafu.

“Sijui kuna nini... ukisikiliza presentation (maelezo) utaunga mkono,” alisema Spika Ndugai, akisisitiza kuwa haelewi nini kimekwamisha mradi huo muhimu ambao ungeitumbukizia nchi dola za Marekani bilioni 10.

Aidha katika ziara hiyo ya mwaka juzi, Spika Ndugai alisema Wachina hao walisema kwamba wanashangaa kwa taifa kama Tanzania kuanza kujenga reli badala ya bandari kwani bandari ingelikuwa ya kwanza ili kupokea mizigo ya reli.

Wabunge wengi waliochangia walisema kwamba ujenzi wa bandari hiyo na mji wake wa kiviwanda ungesaidia kurejesha kwa haraka gharama za ujenzi wa reli ya kisasa. Vile vile wajenzi hao walikuwa wanajenga reli ya kisasa kuanzia Bagamoyo na kuiunganisha na reli ya Tazara.

Mbunge wa Bagamoyo, Dk Shukuru Kawambwa (CCM) alisema mradi huo mkubwa wa kielelezi ambao ulihusisha ujenzi wa bandari, viwanda na kuwa eneo maalumu la kiuwekezaji likiwa na viwanda vikubwa 190 baada ya mazungumzo na kutia saini hati mbalimbali kushindwa kujengwa ni hasara kwa taifa.

Alisema wakati Tanzania inaendelea kuzungumza katika kipindi hicho hicho cha kuanzia mwaka 2012 kampuni hiyo imejenga bandari za kisasa katika nchi za Djibouti, Togo, Nigeria na Sri Lanka.

Alisema wananchi wa Bagamoyo walitoa sehemu kubwa ya ardhi wakitambua umuhimu wake, lakini ukiangalia ukubwa wa mradi na athari zake chanya katika uchumi wa nchi, serikali inawajibika kueleza kumetokea nini.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alitaka kujua sababu za kusimamisha mradi huo ambao ungeliingiza nchini dola za Marekani bilioni 10 na kuiweka Tanzania katika ushindani.

Mbunge wa Buchosa, Charles Tizeba (CCM) alisema wakati SGR ikimalizika watanzania watakuwa kituko kwa kuwa kutakuwa hakuna bandari ya kuhudumia mizigo inayoletwa na reli hiyo na kuitaka serikali kuendelea na mradi wa bandari ya Bagamoyo.

Alisema Bagamoyo ilikuwa ni jibu ya ubora wa wa reli inayojengwa ambayo inatarajiwa kuhudumia ndani na nchi za jirani.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Magereli (Chadema) alisema kwamba tatizo linalokumba Tanzania liko katika sera na mipango na kusema taifa lazima liwe na uangalifu katika kupanga na kutekeleza maamuzi yake.

Alisema kuna orodha ndefu ya mambo ambayo yanaanzishwa na kutumia fedha za walipa kodi halafu hayamalizwi na kuhoji kutotekelezwa kwa mradi wa bandari ya Bagamoyo kwa sababu za masharti yaliyotolewa na mwekezaji pamoja na hatua kubwa iliyokwishafikiwa na matumizi ya fedha za walipa kodi katika hatua hizo.

Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM) alisema kama taifa lazima liwe na fikra mpya za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kukubali kuingia katika mikataba huku vihatarishi vyake vikijulikana, kwa kuzingatia maslahi mapana na thamani ya mradi wenyewe kwa umma.

Alitaka timu ya mazungumzo kukwamua mazungumzo hayo na kuhakikisha kwamba nchi inasonga mbele.

Wabunge wengine walioongelea bandari ya Bagamoyo ni Mbunge wa wa Rufiji Mohamed Mchengelwa (CCM) ambaye alisema ni aibu kwa wanasheria kukaa miaka saba kujadili mradi muhimu kama huo wakati nchi nyingine zinatekeleza miradi yao.

Mwingine ni Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), Mbunge wa Hanang Mary Nagu (CCM) ambaye alihusika kutia saini mradi wenyewe na mbunge wa Singida Magharibi, Elibarick Kingu (CCM) ambaye alisema kwamba wakati wa miaka 2008 na 2012 wakati wa utiaji saini naye alikuwa katika kitengo cha ushauri. Hata hivyo Waziri Kamwelwe alisema kwamba mazungumzo yanaendelea na kwamba anatarajia yatakuwa na mwisho mzuri.

ILI kukabiliana na ugonjwa wa Covid- 19 unaosababishwa na virusi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi