loader
Picha

Watanzania mil 18 waajiriwa viwanda vidogo

IMEELEZWA na Wizara ya Viwanda na Biashara kwamba sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo, imetoa ajira kwa zaidi ya Watanzania milioni 18 hadi sasa.

Aidha, viwanda 32 kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, vimepewa notisi za kuwasilisha mipango ya kuviendeleza ifikapo Mei 31, mwaka huu au la, vitarejeshwa serikalini.

Kauli hizo zimo katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara, iliyowasilishwa bungeni na Waziri mwenye dhamana, Joseph Kakunda.

Katika wasilisho hilo, Waziri Kakunda ameomba Bunge kuidhinisha makadirio ya wizara yake ya kukusanya mapato ya jumla ya Sh milioni 14.3 na matumizi ya Sh 100,384,738,648. Mwaka uliopita wizara hiyo iliidhinishiwa matumizi ya Sh 143,334,153,648.

Akifafanua mafanikio katika sekta ya viwanda, Kakunda alisema kwamba jumla ya miradi mipya 304 imesajiliwa na kati ya hiyo, miradi 107 ilisajiliwa chini ya Kituo cha Uwekezaji (TIC), miradi 194 ilisajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na miradi mitatu ilisajiliwa na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (EPZA).

Alisema miradi hiyo inatarajiwa kuongeza jumla ya ajira 11,793.

Aidha alisema Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) limeratibu na kuhudumia viwanda vidogo vipya 1,400 vilivyotoa ajira 4,200.

Hata hivyo, alisema katika mwaka wa fedha 2018/2019 uhamasishaji wa Sido, uliwezesha uanzishwaji wa viwanda 607 ambavyo kati ya hivyo, viwanda 151 vimeanzishwa kupitia Mikakati ya Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP); viwanda 28 kupitia kupitia kongano; viwanda 20 kupitia kiatamizi na viwanda 408 kupitia huduma nyingine.

Alisema kwamba wizara ina mpango wa kuimarisha zaidi Sido ili iweze kuongeza zaidi maeneo ya kufanyia kazi wajasiriamali nchini na pia kuimarisha teknolojia 40 zilizowezesha kuanzishwa kwa viwanda kwenye ubanguaji korosho, usindikaji wa mihogo na teknolojia ya usindikaji vyakula.

Kakunda alisema kwamba tathmini ya uwekezaji kwa viwanda chini ya Mamlaka ya EPZ na SEZ tangu mamlaka ya EPZ kuanzishwa, imeonesha mafanikio makubwa na kwamba hadi Septemba 2018, EPZA imetoa leseni za kuanzisha viwanda kwa kampuni 169 zilizowekeza mitaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.219 na kuajiri wafanyakazi 56,312.

Alisema EPZ yenyewe ilisajili kampuni tatu za uwekezaji, ambazo ziliingiza mitaji ya moja kwa moja dola za Marekani milioni 45.7 na kutoa ajira 815.

Alisema pamoja na changamoto mbalimbali hasa za miundombinu wezeshi katika maeneo ya EPZ na SEZ, ujenzi wa viwanda 10 unaendelea akitoa mfano wa Kiwanda cha African Dragon Enterprises Limited kikianza uzalishaji, na kuchangia mapato ya zaidi ya Sh bilioni 7.96 kati ya Desemba 2018 na Februari 2019. Kiwanda hicho kipo Bagamoyo.

Viwanda vilivyobinafsishwa Kakunda alisema kwamba kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, 88 vinafanya kazi na 68 havifanyi kazi. Pia alisema kwamba kati ya vinavyofanya kazi, 42 vinafanya kazi vizuri sana, 46 wastani na 20 vimefutwa.

Pia viwanda vingine 48 wamiliki wake wameshindwa kuviendesha kwa mujibu wa mikataba ya mauziano na hivyo 16 kurejeshwa serikalini na 32 kupewa notisi ya kupeleka mipango ya kuviendeleza.

Hata hivyo, Kakunda alisema kwamba katika baadhi ya viwanda vilivyorejeshwa, vimebainika kuwa nyaraka zake zimetumika kukopa mikopo mikubwa, ukilinganisha na thamani yake wakati wakubinafsisha na wengine hawajalipa mikopo hiyo.

Pia wapo ambao wameshindwa kukabidhi nyaraka za viwanda.

Alitahadharisha kwamba wanaohusika na matendo hayo, wanakabiliwa na kosa la kuhujumu uchumi wa nchi na kuwataka wamalizane na mabenki kwa kulipa mikopo yao yote ifikapo Mei 31, mwaka huu.

Alisema kinyume na hapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na serikali haitaongeza muda wa utekelezaji wa agizo hilo.

Akizungumzia Kiwanda cha Matairi Arusha, Kakunda alisema kwamba tayari hati ya Makubaliano ya Awali (MOU) kati ya NDC na SAYINVEST Overseas (T) Limited imetiwa saini Januari 5, mwaka huu na kwamba kiwango cha mtaji kilichoelezwa na kampuni hiyo kinakubalika.

Aidha, alisema kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya bidhaa za chuma kwa asilimia 303.54 kutoka tani 226,000 hadi kufikia tani 912,000 kwa mwaka. Tanzania ina viwanda 25 vya vyuma vinavyoajiri wafanyakazi 23,150.

Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji bei ya bidhaa mbalimbali zimepanda, ikiwamo nondo ya milimita 16 kutoka wastani wa Sh 32,500 kwa mwaka 2917/2018 na kufikia wastani wa Sh 37,579 kwa mwaka 2018/2019.

Vile vile, bei ya bati geji 32 madukani imepanda kutoka Sh 13,456 mwaka 2017/2018 na kufikia Sh 14,520 mwaka 2019, huku geji 30 imepanda kutoka Sh 17,632 hadi kufikia Sh 18,385 Aidha, bei ya saruji ya mfuko wa kilo 50 ilipanda na kufikia Sh 15,895 ikilinganishwa na Sh 14,759 ya mwaka 2017/2018, sawa na ongezeko la asilimia nane.

Kwa mujibu wa kamati ya kudumu ya viwanda, biashara na mazingira, upatikanaji wa fedha kutoka hazina umekuwa hauridhishi kwa ajili ya wizara hiyo.

Akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Masoud Ali Khamis alisema ni vyema serikali ikapeleka fedha zinazokadiriwa na Bunge kwa wizara hiyo kwani katika kipindi cha miaka mitatu fedha zimekuwa zikiendelea kupungua.

Alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017 zilizotoka zilikuwa asilimia 42.37 mwaka 2017/2018 zilitoka asilimia 30.64 na mwaka 2918/2019 zimetoka asilimia 24.28.

Kamati hiyo imeishauri serikali kuwa makini wakati wa kupanga viwango vya kodi kwa kulinganisha na viwango vya kodi duniani, hususani ndani ya jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama.

ILI kukabiliana na ugonjwa wa Covid- 19 unaosababishwa na virusi ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi