loader
Picha

Shahidi- Nilimuona Mbowe akihamasisha maandamano

SHAHIDI wa pili katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Shaban Abdallah (19), ameeleza kuwa alimuona Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akiwahamasisha wafuasi wake kuandamana kuwasogelea askari licha ya tangazo la kuwataka kutawanyika.

Shahidi huyo ambaye ni mchomelea vyuma anayeishi Kinondoni Moscow, Dar es Salaam amedai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Abdallah alidai, Februari 16, mwaka jana alikwenda asubuhi kwenye eneo lake la kazi eneo la Kinondoni Moscow ambapo huwa anafanya kazi ya kutengeneza vitanda na vyuma.

Alidai kuwa, siku hiyo majira ya saa 11 jioni alipewa fedha na mwajiri wake kwa ajili ya kwenda eneo la Mkwajuni kununua vifaa vya kazi ambapo alifika dukani kwa mtu aliyemtaja kwa jina la Baba John na kufanikiwa kununua vitu hivyo.

Alidai wakati wakifanya hesabu kabla ya kuchukua mzigo, kwa mbali walisikia zogo, lakini hawakuzifuatilia sana.

Alidai zogo lile lilizidi kusogea, ndipo waliamua kutoka dukani na kwenda nje kuangalia ambapo wakaona watu wengi katikati ya barabara wakitokea eneo la Morocco wakielekea eneo la Magomeni huku wakiwa wameshika mawe na marungu.

Aliendelea kudai, waandamanaji hao walionekana kuwa katika hali ya shari na walikuwa wakiimba ‘Hatupoi mpaka mmoja afe watatuua’ kwa kuwaangalia yeye na Baba John walijua kuwa ni watu wa Chadema kwa kuwa walikuwa wamevaa sare, skafu na bendera za Chadema huku viongozi wao wakiwa mbele.

Alidai aliweza kuwatambua Mbowe, Halima Mdee, John Mnyika na Ester Matiko ambao walikuwa wakiongoza wafuasi hao.

Alidai wakati wakiendelea kuwaangalia waandamanaji hao waliona gari la askari likija nyuma yao huku likiwatangazia watawawanyike lakini waliendelea kuandamana.

“Waandamanaji waliweza kulisogelea gari la askari na kuanza kuwarushia chupa za maji, mawe na marungu. Nilimuona Mbowe akiwahamasisha wananchi kuendelea kuandamana kuwasogelea askari huku wakiwa na viongozi wengine,” alidai Abdallah.

Shahidi huyo alidai kuwa, baada ya hapo, askari walipiga mabomu ya mochozi ambapo kila mtu alikimbilia njia yake.

Mbali ya Mbowe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Taifa, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa, Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Vicent Mashinji, Mbunge wa Kawe, Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi