loader
Picha

Yanga yarejea nafasi yake

YANGA jana ilirejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting. Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, timu zote zilishambuliana kwa zamu lakini ni Yanga iliyoipenya ngome ya ulinzi ya Shooting zaidi.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 83 kileleni mwa msimamo ikiwa na tofauti ya pointi moja na mabingwa watetezi Simba, wanaotarajiwa kucheza kesho dhidi ya Mtibwa Sugar. Bao la Yanga liliwekwa kimyani na Pappy Tshishimbi katika dakika ya 16 akiunganisha pasi ya Deus Kaseke na kuujaza mpira wavuni. Bao hilo lilizidi kunogesha mechi baada ya pande zote mbili kushambuliana kwa zamu.

Yanga walikosa mabao kadhaa ya wazi ambapo katika dakika ya 30, Heritier Makambo na Raphael Daudi walikosa mabao baada ya mipira yao kugonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuokolewa na mabeki wa Shooting. Makambo alipata nafasi nyingine katika dakika ya 59 ambapo akiwa peke yake na kipa akapiga shuti hafifu lililoshindwa kufika golini.

Shooting ilibadilika kipindi cha pili na kutawala lakini umakini mdogo wa washambuliaji wake uliwanyima mabao. Timu hiyo nusura iandike bao dakika ya 87 baada ya mchezaji wake Fully Zully shuti lake kudakwa na kipa Clous Kindoki wa Yanga.

Ruvu Shooting imebaki nafasi ya 14 ikiwa na pointi 42. Kwenye uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mwadui ililazimishwa sare ya mabao 3-3 na Mbao. Matokeo hayo yanaifanya Mbao kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo ikiwa na pointi 44 na Mwadui ni ya 19 ikiwa na pointi 38.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi