loader
Picha

Madereva wa mabasi kutogoma leo

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafi ri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imesema hakuna mgomo wa madereva wa mabasi yaendayo mikoani leo kama taarifa zilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumapili iliyopita.

Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Lameck Kamando kwenye mkutano wake na vyombo vya habari.

Ujumbe huo ambao ulielezwa kusambazwa na Umoja wa Madereva uliwataka madereva wote wa mabasi kugoma kuanzia leo kwa nia ya kupinga adhabu za faini kubwa zinazotolewa na Sumatra kutokana na madereva hao kukiuka Mfumo wa Kudhibiti Mwenendo wa Mabasi (VTS) kwa kwenda mwendokasi wa zaidi ya kilometa 80 kwa saa.

Kutokana na kusambaa kwa taarifa za mgomo huo ambao umeleta taharuki kwa wasafiri, Kamando alisema Sumatra ilikutana na wadau likiwemo Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) na Chama cha Madereva Tanzania (UWAMATA) ambao kwa pamoja walisema taarifa hizo siyo za kweli, hivyo hakuna mgomo wowote.

“Mgomo haupo kwa sababu ni batili na haukufuata kanuni na taratibu, kama kuna mtu anasisitiza upo basi ajitokeze na aeleze sababu za msingi za kuitisha mgomo huo, Sumatra tunawakumbusha wamiliki wa mabasi wafuate masharti ya leseni zao,” alisema Kamando.

Kamando alisema kero za madereva hao wamezipokea na watazifanyia kazi. Mwanasheria Mkuu wa UWAMATA, Frank Sanga alisema licha ya mgomo huo kutokuwepo, lakini madereva wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu na Sumatra kutokana na faini wanazotozwa kwa kutofuata kanuni za mamlaka hiyo badala ya Sheria ya Usalama Barabarani.

Alisema hali hiyo imekuwa ikijitokeza zaidi mikoani hususani mkoani Morogoro ambako madereva hutozwa kati ya Sh milioni 1 hadi Sh milioni 28 na wakati mwingine hulazimishwa kulipa sehemu ya faini hizo hapohapo hali inayowafanya madereva kuyatelekeza magari na kukimbia.

“Tumeshafungua kesi mbili Mahakama Kuu dhidi ya Sumatra, kesi namba 257/2019 na kesi namba 87/2019 ili mahakama itoe ufafanuzi kwamba madereva wanapaswa kuadhibiwa kwa sheria ya usalama barabarani au kwa kanuni ya Sumatra, kwa hiyo nawaomba madereva wasigome mpaka hapo mahakama itakapotoa maamuzi, kugoma wakati jambo liko mahakamani siyo sahihi, ni kuinyima haki mahakama kuamua kuhusu kile ambacho tumekipeleka mahakamani,” alisema Sanga.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Musilimu, alisema baada ya kufuatilia ujumbe unaosisitiza kuwepo kwa mgomo huo, walibaini kuwa ulisambazwa na Umoja wa Madereva Tanzania lakini pasipo kuandikwa jina au cheo cha mhusika. Katika hali hiyo, alisema mgomo huo unakosa uhalali na ni kosa la jinai.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi