loader
Picha

Wabunge wataka sheria ya hakimiliki ibadilishwe

WABUNGE wamechachamaa bungeni wakiomba sheria ya hakimiliki na hakishiriki ya 1999 ibadilishwe ili kuwasaidia wasanii kulinda kazi na haki zao kwani hadi sasa wanapata kipato duni kisicholingana na ubora wa kazi zao.

Wabunge hao, Maulid Mtulia wa Kinondoni (CCM) na Joseph Mbilinyi wa Mikumi (Chadema), wamelalamika kitendo cha wasanii kuendelea kudhulumiwa kazi zao na wakaomba serikali ilete muswada wa mabadiliko ya sheria bungeni ili ipewe meno kulinda kazi zao. Mtulia alihoji serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wasanii ili kupata stahiki zao na akahoji sera na sheria zinasaidiaje wasanii hao kumiliki na kunufaika na kazi zao za sanaa.

Mbunge wa Mikumi, Mbilinyi akiuliza swali la nyongeza bungeni, alihoji lini sheria namba 7 ya mwaka 1999 itapelekwa bungeni ili kubadilishwa ipewe meno ya kuwasaidia wasanii kupata stahili za kazi zao. Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza (pichani) alisema katika hatua ya kwanza mkakati uliopo ni kuhakikisha Chama cha Hakishiriki Tanzania (COSOTA) kinakuwa chini ya wizara ya habari kutoka wizara ya viwanda ili kazi na haki za wasanii zidhibitiwe vizuri.

Shonza alisema ni kweli sheria hiyo ina upungufu lakini kabla ya kufanyiwa marekebisho, inatakiwa kuhakikisha Cosota inarudishwa ili kuwa taasisi chini ya wizara ya habari kwani sasa ipo wizara ya viwanda na biashara. Alisema ni kweli wasanii wanasajili kazi za Cosota ambayo ipo chini ya wizara ya viwanda na biashara hata kama wizara ya habari ndiyo yenye dhamana ya kusimamia wasanii nchini.

Shonza alisema wizara inatambua changamoto zinazowakumba wanasanii nchini, lakini akawaomba watengeneze kazi zenye ubora na ubunifu wa hali ya juu ili kushindana kwenye soko. Alisema ili kunusuru kazi zao zisiibiwe wanaweza kuachana na mtindo wa kutengeneza kazi katika CD, wakasonga mbele kisayansi na kiteknolojia kwa kutengeneza kazi zao kwa njia ya mtandao kama alivyofanya msanii Wema Sepetu ambaye amepata faida kubwa.

Shonza aliwaonya wasanii kuepuka kuingia mikataba mibovu na wasambazaji wa kazi zao, badala ya kuuza kazi tu wanauza hata kazi-mama ambayo inawafanya waendelee kuumia wakati wote. Shonza alisema Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ilielekeza kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia hakimiliki ambayo ni sehemu muhimu ya dhana pana ya milikibunifu.

Hivyo mwaka 1999 ikatungwa sheria ya hakimiliki na hakishiriki ambayo chini yake maslahi ya watunzi wa kazi za sanaa, wafasiri, watayarishaji wa vihifadhia sauti, wachapishaji yanalindwa kicheria na chombo cha kusimamia haki hizo Cosota kilianzishwa.

Hivyo sera na sheria vipo kulinda maslahi ya wasanii, lakini tatizo ni uelewa mdogo wa wasanii wenyewe kuhusu haki zao na ulinzi wake kisheria. Ili kukabiliana na tatizo la wasanii hilo, Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania na Baraza la Sanaa la Taifa, imetoa elimu kwa wadau 5,200 kuhusu masuala ya hakimiliki, hakishiriki, mikataba na makubaliano kupitia mafunzo ya kuwajengea uwezo ili wawe walinzi wa kazi nahaki zaokwa kuingia mikataba yenye maslahi.

MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Simba, raia wa Burundi, Meddie Kagere ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi