loader
Picha

Bodaboda wamulikwe kwa jicho la ziada

TAARIFA ya kwamba idadi ya vifo vya waendeshaji bodaboda kwa robo ya mwaka huu, kati ya Januari na Machi imepungua ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka jana inatoa matumaini kwa uhai wa Watanzania.

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Usalama Barabarani, Deus Sokoni idadi ya waendeshaji bodaboda waliopoteza maisha katika kipindi hicho ni 73 na majeruhi wakiwa 121.

Amesema katika kipindi kama hicho mwaka jana bodaboda waliokufa walikuwa 108 na waliojeruhiwa walikuwa 214. Bila shaka kupungua kwa idadi ya vifo na majeruhi haikutokea tu bali kulikuwa na juhudi za ziada kukabiliana na udhibiti wa ajali.

Licha ya ukweli kwamba idadi ya vifo na majeruhi pia imepungua katika kipindi hicho kwa madereva wa magari, waendeshaji baiskeli na watembea kwa miguu, sisi tunapenda kuzungumzia zaidi madereva wa bodaboda kwa sababu katika uhalisia ndiyo wanaoongoza katika uvunjaji wa sheria za usalama barabarani tena kwa makusudi.

Sote ni mashahidi kuona madereva wa bodaboda wakibeba abiria bila kuvaa kofia ngumu kwao na abiria wao, wakipakia abiria zaidi ya wawili au mishikaki huku wakivuka bila aibu maeneo ya makutano ya barabara nyenye taa hata kama zinaonesha alama nyekundu ya hatari inayowataka wasimame.

Hapa tunapenda kutoa mwito maalumu kwa askari wetu wa usalama barabarani kwamba hali ya vifo vya bodaboda na majeruhi inaweza kupungua zaidi iwapo makosa hayo ya wazi yanayoshuhudiwa na raia wa kawaida bila taaluma ya kipolisi, yanapaswa kushughulikiwa ipasavyo.

Ni wazi kwamba vitendo vya kuvuka makutano ya barabara yenye taa zinazoonesha rangi nyekundu ni kama vile haiwahusu waendeshaji bodaboda.

Wakati mwingine wanapita huku polisi wa usalama barabarani wakiwashuhudia wakijua vilivyo kwamba kama ni gari ikifanya hivyo, hukamatwa mara moja na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Sisi tunajiuliza kinachoshindikana kufanya hivyo kwa bodaboda ni nini hasa? Kwa nini tunaona kama vile wao wana sheria tofauti na madereva wengine wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu?

Sisi tunaamini kwamba iwapo hatua za makusudi na za kisheria za usalama wa barabarani zikichukuliwa kwa vitendo kuwapatia wanachostahili bodaboda wanaovunja sheria hizo kwa makusudi, idadi ya vifo na majeruhi itapungua zaidi.

Pamoja na changamoto za mapungufu hayo, tunapenda kukipongeza Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kwa kazi hiyo nzuri ya kupunguza ajali hizo.

Hakuna ubishi kwamba watazichukua changamoto tulizozieleza kwa hatua chanya ili kuongeza nguvu na mafanikio makubwa zaidi katika udhibiti wa vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani. Hili linawezekana. Tufanye kwa umakini unaostahiki kunusuru maisha ya raia wetu.

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi