loader
Picha

Serikali yatenga bilioni 88/- kulipa wakandarasi nchini

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imetenga Sh bilioni 88 kulipa wakandarasi mbalimbali nchini wanaotekeleza miradi ya maji.

Aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rita Kabati (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani kuhakikisha inawalipa wakandarasi wanaoidai ambao wengi wao hawajalipwa madai yao.

Aweso alisema serikali imetenga fedha hizo kwa lengo la kulipa makandarasi wote nchini akiwemo mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji katika mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo ambaye tayari amelipwa zaidi ya Sh bilioni moja.

Akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF) aliyetaka kujua serikali imefanya tathmini ili kujua ni asilimia ngapi ya miradi 10 ya visima 10 katika kila wilaya iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) imefanikiwa au haijafanikiwa.

Naibu waziri huyo alisema katika mwaka 2016, wizara iyo ilifanya tathmini ya kina nchi nzima ili kujua idadi ya visima vyote vilivyochimbwa kwa awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika halmashauri zote Tanzania Bara. “Idadi ya visima vilivyochimbwa vilikuwa 1,485 kati ya hivyo, visima 990 sawa na asilimia 67 vilipata maji na visima 494 sasa na asilimia 33 vilikosa maji,” alisema.

Alisema maeneo ambayo visima vyake vilikosa maji, serikali ilitumia vyanzo vingine mbadala kama vile chemchemi, mito, maziwa au kujenga mabwawa ili kuhakikisha maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango wa vijiji 10 yanapata huduma bora ya majisafi na salama.

Alisema kwa sasa serikali imeanzisha Mfuko wa Maji wa Taifa ambao unalipa miradi yote iliyochelewa kukamilika na miradi mipya inayoendelea kujengwa katika halmashauri zetu, lengo ikiwa ni kumpatia huduma bora ya maji kwa kila mwananchi.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi