loader
Picha

Daktari abainisha dalili za saratani za jicho kwa mtoto

IMEELEZWA kuwa uwepo wa weupe kwenye mboni ya jicho la mtoto au kengeza ni moja ya dalili za saratani ya jicho hivyo, wazazi waonapo dalili hiyo wanapaswa kuwapeleka watoto wao hospitalini haraka.

Kati ya vizazi hai 16,000 hadi 18,000 duniani asilimia moja huwa na saratani hiyo ambayo huchangia asilimia tatu ya saratani za watoto duniani na kwa Afrika, huchangia asilimia 10 hadi 15 ya saratani za watoto hao. Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Anna Sanyiwa ikiwa ni Wiki ya Kuongeza Uelewa kuhusu Saratani ya Jicho (Retinoblastoma) iliyoratibiwa na Taasisi ya Rotary Oysterbay.

Dk Sanyiwa alisema kuwa asilimia 80 ya watoto wenye umri kati ya mwaka mwaka mmoja hadi mitano wanaougua saratani ya jicho nchini, hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kuchelewa kupata matibabu ya ugonjwa huo.

Alisema kuwa ugonjwa huo haujatambulika kwa wazazi wengi nchini na kwamba si jambo rahisi kwao kupokea matokeo ya saratani kama vile watoto kutolewa macho. Alisisitiza kuwa uwepo wa chama cha wazazi ambao watapeana moyo na kushauriana kuhusu kukabiliana na saratani ya jicho utawezesha hata wagonjwa wapya kuhimili tatizo hilo.

Alifafanua kuwa changamoto wanayokutana nayo ni wazazi kuwachelewesha watoto hao kwenda hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu hivyo hufika wakiwa wamechelewa na ugonjwa unakuwa umesambaa. Dk Sanyiwa alieleza baada ya jicho kuharibika, tiba inayofanyika ni kuondoa jicho hali ambayo ni ngumu kwa mzazi kuipokea hivyo wengine hutoroka kabisa na kurudi pindi jicho likiwa limeharibika zaidi.

Kwa upande wake, mzazi wa mtoto mwenye saratani ya jicho, Rehema Kitunda alisema kuwa ugonjwa huo hauna dalili za awali ambazo zinamfanya mzazi aweze kugundua na kumpeleka mtoto wake hospitali. Kitunda alisema kuwa aligundua mtoto wake ana ugonjwa huo akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi saba na baada ya mtoto kuanza kuishiwa damu mara kwa mara ndipo wakaamua kupimwa magonjwa yote.

Aliongeza kuwa ili kudhibiti ugonjwa huu, inapaswa kuwepo na chanjo katika vituo vya afya na hospitali kwa lengo la kuwa kinga watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali. Aliwaasa wazazi wanapoona tatizo lolote kwa mtoto kukimbilia hospitali na kwamba hawapaswi kudharau wala kuhusisha na imani za kishirikina badala yake wawaamini madaktari kwani hawawezi kuondoa macho ya watoto wao bila sababu.

Naye, Mwanachama wa Rotary, Abdallah Singano alisema tatizo la saratani ya singano limekuwa kubwa hivyo ni lazima jamii ielimishwe juu ya ugonjwa huo. Singano alisema tayari wametoa vifaa vya kuchunguza, kutibu saratani na kuangalia kama tatizo limeisha vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 170 kwa ajili ya hospitali za Muhimbili na Mloganzila. Alisema miongoni mwa vifaa vya kutibu ugonjwa huo ni vya kufanya upasuaji wa jicho bila kulitoa na kuondoa tatizo hilo.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Na Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi