loader
Picha

Ufungaji ‘simulator’ utakavyoboresha umahiri katika Chuo cha Bandari

CHUO cha Bandari cha Dar es Salaam kinajiandaa kufunga kifaa cha kufundishia kwa vitendo (simulator) chenye thamani ya Sh bilioni 1.6 katika juhudi zake za kuboresha umahiri wa wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo.

Mkuu wa chuo hicho, Dk Joseph Kakeneno, anasema kifaa hicho kinachotazamiwa kufungwa mwezi ujao, kimenunuliwa nchini India na kwamba kitakifanya chuo hicho kutoa wanafunzi bora zaidi katika kukidhi mahitaji ya sasa ya ajira. Anasema uwekaji wa simulator hiyo ni sehemu ya mpango mkakati walio nao wa muda mrefu wa kujenga kituo cha kisasa cha mafunzo ya umahiri wa kibandari nchini.

“Ni kituo ambacho kitakuwa na mkusanyiko wa vifaa mbalimbali vya kufundishia kwa maana ya simulator mbalimbali, vifaa halisi vya kufanyia mazoezi na vifaa vya kutegeneza kitu kinachofanana kabisa na bandari,” anasema. Simulator ni nini? Hiki ni chombo au kifaa kinachofanya kazi mithili ya kifaa halisi na katika mazingira halisi.

Dk Kakeneno anafafanua akisema kuwa, simulator inayofungwa chuoni hapo imeundwa kutegemea mahitaji yao na hivyo itatumika kufundishia mambo mbalimbali yanayohusu huduma za kibandari kwa mpigo. “Kwa hiyo, mwanafunzi akija akikaa pale anafanya mafunzo kivitendo mithili ya anavyokuwa kwenye kifaa halisi,” anasema. Dk Kakeneno, anasema Chuo cha Bandari hakifanyi kazi ya kufundisha pekee,bali pia kuwapima na kuwapa leseni za kufanya kazi bandarini.

Anasema mtambo huo pia utasaidia kumpima mtu uwezo wake kabla ya kwenda kutumia vifaa halisi vya kibandari. “Kutokana na uwezo huo mtambo utatoa majibu kwamba mhusika sasa ana uwezo huo wa kufanya shughuli za kibandari, au la,” anasema. Anasema tayari kuna vyuo kadhaa nchini vyenye stimulator, lakini hii inayoletwa ndiyo itakuwa ya kwanza kwa vyuo vya Afrika Mashariki kumudu kufundisha mambo mengi yahusuyo masuala ya kibandari kwa mpigo kutokana na ukubwa wake.

Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri), Olivary John, anasema kifaa hicho kitaondoa changamoto wanayoipata wanafunzi wanapokwenda kuanza kazi baada ya kuhitimu mafunzo yao na kupata vyeti na leseni zinazotolewa na chuo hicho kwani wakiwa hawana uzoefu halisi wa kazi wanazokwenda kufanya katika baadhi ya maeneo.

“Kwa mfano, kunapokuwa na jua kali, mwanafunzi anashindwa kuendesha vile vyombo na hivyo kijana anashindwa kuendana na kile chombo ili ufanisi uendelee kuwa wa juu na hivyo matokeo yake ni ufanisi unashuka.’’

Anasema chombo hicho kitaondoa pia changamoto ambayo wanafunzi wao huipata wakati wanapoanza kazi katika vyombo vinavyotumika katika utendaji wa kila siku kulazimika kusimama kwanza ili kutoa mafunzo kwao. “Lakini sasa kupitia kifaa hicho, mwanafunzi ataingia kazini akiwa na umahiri wa moja kwa moja wa kutumia vifaa kwa sababu simulator ina uwezo wa kufanya kama kifaa halisi,” anasema.

Akizungumzia kuhusu utalaamu wa kukituimia kifaa hicho, John anasema katika mkataba wa manunuzi ya chuombo hicho, anayekuja kufunga mtambo anawajibika kutoa mafunzo kwa kipindi cha mwezi mzima kwa timu ya wataalamu wa chuo kwa maana na waalimu watakaoutumia kufundishia. Anasema kuna wakufunzi sita, waendesha mtambo (operators) sita na mafundi wa mtambo wawili watakaopata mafunzo mahususi ya kuangalia mtambo huo.

“Kwa hiyo utaona kutakapokuwa na mushekeli, hakutakuwa na haja ya kuwaita wafungaji wa mtambo, bali matatizo yatarekebishwa na mafundi wetu,” anasema. Aina tatu za kozi Kuhusu kozi mbalimbali zinaotolewa na chuo hicho, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo huyo anasema, kimsingi wanatenga kozi katika mafungu matatu, kozi za muda mrefu, kozi za muda mfupi na kozi kwa ajili ya mahitaji maalumu ya mteja (tailor made courses).

“Tulishawahi kupata wateja wa kozi kwa ajili ya mahitaji yao kutoka Rwanda, tulishawahi kupata kutoka kampuni ya Acacia, kutoka Serengeti Breweries na kadhalika. Hawa wate wanakuja na mahitaji maalumu,” anasema.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Bandari Dar es Salaam, Robert Jonathan anasema kadri siku zinavyosonga mbele, chuo kinazidi kutoa mafunzo bora na kwa umahiri zaidi.

Mwanafunzi huyo anayesoma kozi ya kuhudumia mizigo (Shipping and Port Management) katika chuo hicho anafafanua mabadiliko makubwa yaliopo katika chuo hicho hasa kwa upande wa mafunzo kwa vitendo. “Chuo hiki ndicho pekee katika eneo hili la Afrika Mashariki kinachotoa mafunzo kuhusu uhudumiaji mizigo. Ni chuo kizuri kilicho katika mazingira mazuri ya kujifunzia pia,” anasema.

Mkufunzi wa Uhandisi na Usimamizi wa Shughuli za Matengenezo, Mhandisi Wilfred Mathew, anahimiza wanafunzi wengi kupenda masomo ya sayansi na wakipata nafasi kujiunga na chui hicho.

Anaamini kwamba, kutokana na vijana wengi kukimbia sayansi ndiyo maana madarasa ya masuala ya uhandisi chuoni hapo yana wanafunzi wachache. Huku akiamini kwamba, masomo ya sayansi hayana ugumu sana kama wanafunzi wengi wanavyoambizana, ana matumaini ya wanafunzi zaidi kusoma sayansi kipindi hiki nchi inavyojielekeza katika uchumi wa viwanda. Mhadhiri huyo ambaye amekuwa chuoni hapo kwa muda wa miaka 25 anajivunia wanafunzi wake kwamba wamekuwa wakifanya vizuri kila wanakokwenda kufanya kazi.

Anasema wapo ambao wamejiendeleza hadi kufikia ngazi ya shahada ya uzamili. Mwanafunzi wa Mwaka wa Pili katika chuoni hicho, Mariam Hamisi anapongeza ufundishaji kwa vitendo chuoni hapo unaowafanya wawe na umahiri mkubwa kiutendaji. Mariamu anasema masomo ya sayansi siyo magumu kama atayapenda na kujituma. Msichana huyo mwenye ndoto za kuwa mhandisi ‘mkubwa’ nchini, anatoa mwito hasa kwa wasichana wenzake kuchangamkia masomo ya sayansi kwani ‘yanalipa’.

Ufungaji ‘simulator’ utakavyoboresha umahiri Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo cha Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko (wa pili kulia) akisalimiana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe katika mahafari ya chuo hicho mwanzoni mwa mwaka huu jijini Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo cha Bandari, Dk Joseph Kakeneno.

WAKAZI 1,639 wa vijiji vya Matongo na Nyabichune katika eneo ...

foto
Mwandishi: Na Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi