loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Umuhimu wa kuchangia shule tulizosoma

KUNA msemo mmoja wa wahenga unaosema: “Elimu ni ufunguo wa maisha.” Mbali na kukumbuka msemo huu wa wahenga, pia nakumbuka Rais wa Kwanza Afrika Kusini ambaye pia ni miongoni mwa wanaharakati wa Afrika, Nelson Mandela aliwahi kusema: “Education is the most powerful weapon which you can use to change the world” akimaanisha kuwa, elimu ni silaha kali zaidi unayoweza kutumia kuubadili ulimwengu.

Katika makala haya, nitazungumzia elimu, nguvu ya elimu kwa maendeleo ya taifa na namna Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyompa kila raia haki ya kupata elimu. Ibara ya 11, Kifungu cha Pili ya katiba hii inampa kila raia haki ya kujielimisha. Katika Ibara ya 11 (2) Katiba inasema: “Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake.”

Hapa, kifungu hiki kinatoa haki ya kikatiba kwa raia kuweza kujipatia elimu katika fani anayoipenda ili kupanua upeo. Kimsingi, elimu ni moja katika nguzo kubwa kwa maendeleo ya taifa lolote.

Nchini Tanzania, elimu bure imeweza kusaidia watoto maskini kwenda shule kwa kuwa Rais John Magufuli tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, anatekeleza kwa vitendo sera ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi kidato cha nne.

Ninapoitazama nguvu ya elimu, na ninapotazama ugunduzi na maendeleo ya teknolojia yanayotokana na maendeleo ya elimu katika nchi zilizoendelea, naamini bado Tanzania na Afrika kwa jumla, tunaweza kupiga hatua kubwa kwa kuwekeza katika elimu ya watoto na vijana wetu hasa elimu kwa vitendo.

Kwa msingi huo, ninaona umuhimu wa mfumo wa elimu nchini kuzingatia vitendo tangu ngazi za chini na pia, wajengwe katika kukusanya uzoefu, kujifunza kwa muda mrefu na hatimaye, kuanza kulitumikia taifa mapema kwa ubora zaidi. Ndiyo maana ninaipongeza serikali chini ya Uongozi wa Rais John Magufuli kwa kutoa elimu bure, pia ninashauri kuhakikisha mfumo wa elimu tangu ngazi za chini, unajikita zaidi katika kujenga misingi imara zaidi ya utafiti, ubunifu na kufanya kwa vitendo.

Ili hilo lifanyike kwa manufaa, tuliosoma zamani katika nafasi mbalimbali tunaweza kuisaidia serikali kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchangia nguvu zetu na mali mbalimbali kama pesa, vifaa vya ujenzi na kufanya ukarabati unaowezekana ili nguvu zetu zinapoishia, serikali isaidie kukamilisha. Kufanya hivi kutaisaidia serikali kutatua kero ya uhaba wa madarasa, ubovu wa vyumba vya madarasa kama kuvuja kwa mabati na upungufu au dosari nyingine ukiwamo upungufu wa samani kama madawati.

Ni muhimu kuzingatia kuwa, mmoja kati ya wanafunzi walioguswa na kukarabati shule alizosoma awali zilizosababisha afike hapa alipo, anaweza kuacha alama ya fadhila kwa wanafunzi wenzake wanaohitaji msaada ili kuwaepushia adha mbalimbali ikiwamo ya kusoma huku wakinyeshewa mvua kutokana na mabati ya madarasa yao kuvuja. Hivi ndivyo, Dk Mosses Mwizarubi alivyoona umuhimu na kuamua kufanya kwa manufaa ya umma.

Mwizarubi ameamua kurudisha fadhila shuleni kwa kufanya ukarabati wa shule za msingi mbili alizosoma jijini Arusha ambazo ni Shule ya Msingi Sinoni na Shule ya Msingi Uhuru. Mwenyewe anasema, aliamua kukarabati shule hizo kwa kushirikiana na wadau wake wa karibu, baada ya kuomba na kupata kibali cha Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.

Katika ukarabati huo wakati wa likizo fupi ya mwezi Aprili mwaka huu, wamefanikiwa kubadilisha paa na sakafu katika madarasa matano katika Shule ya Msingi Sinoni, na kujenga mtaro wa kutoa maji ya mvua na kujaza vifusi katika maeneo yaliyokuwa yakituama maji na kusababisha kero vipindi vya mvua. Anasema katika Shule ya Msingi Uhuru, wanategemea kukamilisha awamu ya kwanza ya ukarabati wakati wa likizo ya mwezi Juni mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwizarubi ukarabati huu anaufanya kila akiwa likizo. Anasema amefanya hivyo kama sehemu ya kumshukuru Mungu kwa mema aliyoyapata katika nchi yake na kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha watu wake wanapata elimu bora na katika mazingira bora.

Anasema: “Mungu ametupa nchi nzuri na viongozi wazuri sana ambao wametumika kuilinda amani ya nchi na ustawi wa watu wake, hivyo hatuna budi kuyakumbuka haya na kumshukuru Mungu kwa kushiriki kuchangia kuboresha huduma hizi kadiri ya nafasi na uwezo wetu.”

Mwizarubi anasema Serikali imekuwa ikifanya mambo makubwa tangu iingie madarakani, ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji; ununuzi wa ndege na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege. Mengine ni ujenzi wa barabara za lami na madaraja katika maeneo mengi nchini, ujenzi wa hospitali za wilaya zisizopungua 67 na vituo vya afya zaidi ya 350, utoaji wa elimu bila malipo, miradi mikubwa ya maji na huduma nyingine za kijamii kote nchini.

“Miradi hii inagharimu mabilioni ya fedha, na mimi kama mtumishi wa umma najua namna serikali ilivyojifunga kibwebwe kuikomboa nchi yetu kiuchumi, hivyo ni muhimu kujitokeza kuiunga mkono kadiri inavyowezakana,” anasema. Anaongeza: “… Hatupaswi kuiachia serikali ifanye kila kitu maana mambo ni mengi na rasilimali hazitoshi kufanya mambo yote kwa mkupuo, hivyo lazima tuiunge mkono katika mambo kama haya.”

Anatoa rai kwa Watanzania wote kuipenda nchi yao, kukumbuka walikotoka, walipo na wanakokwenda kwa kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani ili izidi kuboresha na kuimarisha huduma zake kwa jamii. “Tuzingatie kuwa, kila mmoja akikumbuka shule alizosoma na kufanya kitu kidogo kwa nafasi yake, mabadiliko makubwa katika maeneo yetu yataonekana dhahiri,” anasema na kuongeza: “Maendeleo ya nchi yetu yataletwa na sisi wenyewe, hakuna anayetupenda zaidi ya sisi tunavyoweza kujipenda.”

Kuhusu thamani ya msaada wake katika shule hizo anasema: “Sipendi kusema gharama za ukarabati wa shule hizi, bali nimeamua kukarabati kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenzangu waweze kusoma kwa bidii na utulivu wenye tija.”

Walimu wa shule zilizofanyiwa ukarabati wanamshukuru Dk Mwizarubi na wadau wenzake kwa kazi kubwa ya kuboresha miundombinu hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa moyo zaidi, huku wakiamini kupata matokeo makubwa na chanya. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sinoni, Mary Shayo anasema kabla ya msaada huo wa ukarabati wanafunzi walikuwa wakipata tabu ya kunyeshewa mvua hasa wakati wa mvua hali wanayosema sasa wanaondokana nayo.”

Hata hivyo anawaomba wadau wengine kuzidi kujitokeza na kuungana na Dk Mwizarubi kuisaidia shule yake kwano pia inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma muhimu kwa wanafunzi kama vile upungufu wa madarasa pamoja na madawati.

“Nashukuru kwa msaada huu ambao Sasa unatusaidia walimu na wanafunzi kusoma na kufundisha vyema darasani,” anasema Mmwalimu Mkuu Mary. Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Zulina Rajabu anasema kutokana na ukarabati huo hususan uwekwaji wa paa, mahudhurio ya wanafunzi darasani yamekuwa makubwa kwani wana uhakika na usalama wao hata mvua ikinyesha.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, walimu wao wamekuwa wakikumbana na adha ya kunyeshewa hasa katika msimu wa mvua hivyo kuwekewa mapaa mapya kumeongeza ari ya kufundisha. Mwalimu mmoja anayekataa kutajwa jina anasema: “Mungu hatawaacha watu waliofanya kazi hii, maadam wamegusa maisha ya wanyonge, lazima watabarikiwa.”

Wanafunzi Lucas John wa Shule ya Msingi Uhuru na Mary Issack wa Shule ya Msingi Sinoni, wanasema wameboreshewa mazingira ya kusomea na kutiwa moyo kusoma kwa bidii. Wanasema kabla ya msaada huo walikuwa wanahudhuria kwa mashaka wakihofia usalama wao na adha mvua inaponyesha. Wanasema hii ilikuwa inatokana na mabati kuvuja, hivyo ukarabati huo umewarudishia matumaini ya usalama dhidi ya adha ya mvua.

“Tunamshukuru kaka yetu au tumwite baba yetu kwa ukarabati wa shule hizi maana tulikuwa na mahitaji na bado tuna changamoto nyingi basi sisi wanafunzi tuige mifano ya kurudisha fadhila kwa wale waliotusaidia kutuondoa katika ujinga hata walimu wetu pia ambao muda mwingi huwa nasi kuliko wazazi au walezi wetu majumbani,” anasema Mary.

Mwenyekiti wa Masuala ya Elimu katika Jiji la Arusha ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita anamshukuru Dk Mwizarubi kwa msaada huo wa ukarabati huku akitoa rai kwa watu wengine kusaidia jamii zinazowazunguka katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii. Na kimaendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqqaro anasisitiza watu mbalimbali kusaidia jamii zinazowazunguka hususan katika sala la elimu pamoja na lishe ili kuwezesha wanafunzi kusoma kwa bidii wakiwamo wanafunzi wanaomaliza masomo yao shule za msingi na sekondari.

Dk Mwizarubi alisoma Shule ya Msingi Sinoni mwaka 1992 hadi 1995 kisha kuhamia katika Shule ya Msingi Uhuru alikohitimu masomo elimu ya msingi mwaka 1998. Mwizarubi ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu katika masuala ya fedha.

foto
Mwandishi: Na Veronica Mheta

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi