loader
Picha

Serikali yaridhia mikataba yenye maslahi kifedha

OFISI ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imesema serikali imeridhia mikataba ya kimataifa mingi inayosimamia mazingira yenye fursa ya kupata fedha kwa ajili ya kupambana na changamoto mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Hivyo, imeitaka Bodi ya Mpito ya kusimamia Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji Kaboni (NCMC), kuzichangamkia fursa hizo kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kituo kwa faida ya taifa.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Malongo alisema hayo juzi mjini Morogoro katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bodi ya Mpito ya kusimamia Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji Kaboni, yaani hewa ukaa (NCMC).

Alisema kituo hicho kina umuhimu kwa taifa na serikali itahakikisha inaweka mikakati madhubuti ya kukiendeleza ili kiweze kuleta matunda mazuri kwa kizazi cha sasa na kijacho na taifa kwa ujumla.

Kituo hicho cha kisasa kimejengwa kwa ufadhili wa serikali ya Norway katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA), ambacho kitainufaisha Tanzania kutokana na biashara ya hewa ukaa na kilifunguliwa Mei 19, mwaka 2016 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba.

Hivyo, Malongo aliitaka bodi hiyo yenye wataalamu mbalimbali kutoka Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais kutumia utaalamu wao kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha baada ya kukamilika ufadhili wa Serikali ya Norway.

Pia aliitaka bodi hiyo kupendekeza serikalini kuhusu namna na mfumo wa wa uendeshaji na usimamizi kwa vile kituo hicho hakioneshi kinawajibika na mamlaka zipi, lengo ni kukiwezesha kiwe endelevu kwa manufaa ya taifa.

“Ni muhimu kwa serikali kukiendeleza kituo hiki baada ya ufadhili wa Serikali ya Norway kumalizika, fursa zipo nyingi kwani tayari serikali imeridhia mikataba ya kimataifa mingi hasa ya mazingira ambazo kuna fursa ya kupata fedha kwa ajili ya kupambana na changamoto mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi ,” alisisitiza.

Naye, Mratibu wa kituo hicho, Profesa Eliakim Zahabu alisema mwaka 2008 Serikali ya Tanzania na Serikali ya Norway zilitiliana saini makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa kutokana na ukataji miti ovyo na uharibifu wa Misitu (MKUHUMI).

Profesa Zahabu alisema makubaliano hayo yalilenga kuijengea Tanzania uwezo kwa ajili ya kutekeleza Mkuhumi yaliyokuwa ni ya miaka mitano (2008-2013) na kipindi cha majaribio ambayo Norway iliahidi kutoa hadi jumla ya dola za Marekani milioni 100.

Mratibu wa kituo hicho alisema wazo la kuanzisha kituo cha NCMC lilijitokeza wakati wa utayarishaji wa Mpango wa Taifa wa Mkuhumi mwaka 2009, miaka mitatu baadaye mwaka 2012 makubaliano ya kuanzisha na kukilea kituo hicho yalisainiwa kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na SUA, ambapo mradi huo ulianza Januari, mwaka 2016.

Hata hivyo, alisema kazi kubwa ya kituo hicho ni kuratibu upimaji , uwasilishwaji na uhakiki wa takwimu za kaboni kwa niaba ya serikali na ili kutimiza jukumu hilo na mengine ni pamoja na kutoa huduma ya kitaalamu kwenye upimaji, uwasilishaji na uhakiki wa takwimu za kaboni nchini.

Kwa upande wao, Makamu Mkuu wa chuo kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda pamoja na Mwenyekiti wa bodi hiyo ya mpito, Paul Sangawe kwa nyakati tofauti walisema kuwa ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi bado ni muhimu kwa taifa hivyo wadau na wafadhili wanahitajika kuunga mkono jambo hilo.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi