loader
Picha

Majibu ya maswali muhimu Mfungo wa Ramadhani

HIKI ni kipindi cha mfungo mtukufu wa Ramadhani ambapo waumini wa Kiislamu wanatimiza moja ya nguzo tano za dini yao. Katika Makala haya tunawaletea maswali na majibu muhimu yanayoelezea masuala mbalimbali kuhusu mfungo wa Ramadhani.

Swali: Nia ya kufunga inapatikanaje?

Jibu: Kila sifa njema ni milki ya Mwenyezi Mungu. Wanazuoni mahiri katika sheria na kanuni za dini (fuqahaa) wanakubaliana kwamba, kujichunga na vitu vinavyoharibu swaumu (pia hutamkwa saumu) kuanzia alfajiri inapoingia hadi Magharibi.

Nia ni nguzo kuu ya funga na asiyeweka nia wanazuoni wanakubaliana kwamba hana funga. Nia ni ya moyoni mwa mtu na si kutamkishwa na mtu mwingine kama wengi wanavyodhani au kama inavyofanyika katika baadhi ya misikiti wakati wa swala ya Isha.

Wanazuoni wengi wanasema nia ya kufanga ipatikane kila siku kabla ya kuingia alfajiri na kwamba, hata kujiandaa kwa ajili ya daku kwa lengo la kufunga kesho yake ni nia tosha. Hata hivyo, wapo pia wanazuoni wanaoamini kwamba ukichukulia Ramadhani nzima kama ibada moja, basi ukinuia kufunga mwezi mzima tayari ni nia inayotosha pia.

Wanazuoni pia wanasema kufunga si kujizuia kwa kula na kunywa pekee, bali pia kujizuia na machafu kama vile kusengenya, kusema uongo, kutazama maovu na hata kuyaendea.

Swali: Dua ipi sahihi wakati wa kufuturu?

Jibu: Baadhi ya wafungaji wengi wakati wa kufuturu huleta dua ya “Allaahumma laka swumtu wa ‘ala rizqika aftartu” (Ewe Mwenyezi Mungu Mlezi, kwa ajili yako nimefunga na kwa riziki ulionipa ninafungua swaumu ya leo).” Kufuturu kwa kuanza na dua hiyo kunatokana na hadithi dhaifu iliyoelezewa na Abu Dawood (2358) kutoka kwa Mu’aadh ibn Zuhrah, ambaye anasema alimsikia Mtume Muhammad (SAW) akisema dua hiyo wakati wa kufuturu.

Hakuna haja ya kutumia dua hii dhaifu kwa sababu kuna ripoti sahihi kutoka kwa Abu Dawood huyo huyo (2357) kutokana na hadith ya Ibn ‘Umar (Mwenyezi Mungu awe na radhi naye) ambaye anasema: Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akianza kufuturu alikuwa akisema: “Dhahaba al-dhamau’, wa abtallat al-‘uruuq wa thabata al-ajr insha Allah (Kiu imeondoka, mishipa ya damu imejaa, na malipo yatapatikana, kama Mwenyezi Mungu Mlezi atataka).” (al-Albaani katika Saheeh Abi Dawood).

Pili, ni muhimu kwa mtu aliyefunga kuomba dua wakati wote ikiwa ni pamoja na wakati wa kufuturu. Hii ni kutokana na mapokezi ya Ahmad (8030) kutokana na hadithi ya Abu Hurayrah (Mwenyezi Mungu Mlezi awe radhi naye) ambayo ina meneno mengi, lakini inaisha kwa kumkariri Mtume wa Allaah akisema: “Kuna watu watatu ambao dua zao hazirejeshwi (bila kupokelewa na Mwenyezi Mungu Mlezi): kiongozi mwadilifu, mtu aliyefunga swaumu hadi anapofuturu, na maombi ya mtu aliyepotezwa...”

Hadithi imepewa daraja la usahihi na Shu’ayb al-Arna’uut katika kitabu cha Tahqiiq al- Musnad. Hadithi hii pia imepokelewa na al-Tirmidhi (2525) kwa lafdhi tofauti ikiisha kwa kusema: “… na mtu aliyefunga wakati wa kufuturu…” nayo imepwa daraja la usahihi na al-Albaani katika Saheeh al-Tirmidhi.

Kwa mantiki hiyo, mfungaji anatakiwa kumuomba Mwenyezi Mungu amfanye kuwa mtu wa peponi na amuepushe na moto. Anaweza kumuomba Mungu amsamehe makosa yake pamoja kuomba dua kadhaa zinazokubalika kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislamu.

Swali: Ni vitu gani vinavyotengua swaumu?

Jibu: Mwenyezi Mungu ametupa ibada ya kufunga katika misingi ya busara ya hali ya juu. Anamtaka mja wake afunge, lakini katika mazingara ambayo hayatakuwa sababu ya yeye kudhurika lakini mfungaji hatakiwi kufanya kile ambacho kitaharibu funga yake.

Kwa msingi huo, vitu vinavyoharibu/kubatilisha swaumu vinaweza kugawanyika katika makundi mawili; mosi ni vinavyotoka mwilini kama vile kujitapisha kwa makusudi, kufanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani, kupata damu ya hedhi na kupiga chuku (tiba inayohusisha kutoa damu ama pia inajulikana kama kuumika au hijama -blood cupping). Vitu hivi vinapotoka ndani ya mwili huufanya kuwa dhaifu.

Kwa mantiki huyo, Mwenyezi Mungu Mlezi amevieleza kama vitu vinavyotengua swaumu (funga) na Mwenyezi Mungu Mlezi hataki mja wake ambaye funga imeshamfanya dhaifu halafu vitu hivi vinavyotoka mwili vizidi kumdhoofisha zaidi.

Aina ya pili ya vitu vinavyoharibu saumu ni vile vinavyoingia kwenye mwili wa binadamu kama vile kula na kunywa. Kama mtu atakula na kunywa hatofikia lengo la kufunga. Rejea Majmoo’ al- Fataawa, 25/248 Mwenyezi Mungu amezingumzia kwa kifupi vitu vinavyofungua saumu pale anaposema (tafsiri yetu):

“Hivyo mnaweza kujamiiana nao katika kutafuta kile ambacho Mwenyezi Mungu Mlezi atawajaalia (watoto), pamoja na kunywa hadi uzi mweupe (mwanga wa alfajiri) utakapojitokeza na giza la usiku kutoweka, hapo kamilisheni funga yenu (saumu) hadi giza litakapoingia.” [al-Baqarah 2:187] Katika aya hii Mwenyezi Mungu Mlezi ametaja vitu vitatu vinavyotengua saumu; kula, kunywa na kufanya tendo la ndoa.

Vitu vingine vinavyotengua swaumu vimetajwa na Mtume (SAW) kupitia hadithi zake (matamshi, matendo ama yale yaliyofanywa mbele yake akayaridhia ama kuyakataza). Kwa ushahidi wa Qur’an na Hadith za Mtume, baadhi ya wanazuoni wametaja mambo saba yanayotengua saumu ambayo ni: kufanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani, kujichua hadi kutoa manii, kupatwa hedhi (kwa akina mama) au damu ya uzazi (nifaas), kula na kunywa, chochote kinachoweza kuchukuliwa kama “kula na kunywa”, kutoa damu kwa njia ya hijama ama yanayofanana na hayo na kutapika kwa makusudi.

Kufanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani ni kosa kubwa kwa mfungaji. Ufafanuzi wa hili ni mpaka tupu mbili zinapokutana na hata kama mshindo haukutokea, watu hao wanakuwa wametengua funga yao. Licha ya kwamba hawatotakiwa kula isipokuwa kumalizia siku, wanakabiliwa na kufanya kafara kubwa.

Wakati anayefungua kwa sababu sita zilizobaki analipa siku alizokosa peke yake, mwenye kufanya tendo la ndoa na mkewe anatakiwa kulipa kwa kufunga siku 60 au kulisha maskini 60 ama kumwachia mtumwa huru kama anaye.

Ushahidi wa hili unatokana na Hadithi ya Abu Hurayrah (Mwenyezi Mungu Mlezi awe na radhi naye) ambaye alisema: Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (swallallahu alaihi wasallam) huku akitweta na kusema, “Nimeangamia, nimeangamia miye, Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mlezi!” Akamuuliza, “Kwanini umeangamia?” Akasema, “Nimefanya tendo la ndoa na mke wangu mchana wa Ramadhani.” Mtume (SAW) akamuliza: “Unaweza kucha huru mtumwa?” Akasema: “Hapana.” Akamuuliza:

“Unaweza kufunga kwa miezi miwili inayofuatana?” Akajibu: “Hapana.” Akamuuliza: “Unaweza kulisha maskini sitini?” Akasema: “Hapana.” Unaweza kuiona hadithi hii katika al-Bukhaari, 1936 na Muslim, 1111. Ufafanuzi kuhusu kujichua kwa kutumia mkono hadi kufikia mshindo (masturbation) kunaelezwa kuwa, mbali ya kuwa kitendo hicho ni haramu kwa Muislamu, pia kinatengua saumu ya mfungaji.

Ushahidi wa mtu kufungua kwa kufanya kitendo hicho haramu ni kutokana na maeneno ya Mwenyezi Mungu Mlezi katika Hadithi Qudsi anapomzungumzia mfungaji kwa kusema: “Anaacha chakula chake, kinywaji na matamanio kwa ajili yangu...” (al-Bukhaari Hadithi Namba 1894 na Muslim, 1151). Kitendo cha mtu kufikia mshindo (kutoa manii kwa kujichua) kinaingia kwenye eneo la ‘matamanio’ ambayo mwenye kufunga anatakiwa kujizuia nayo.

Kwa hiyo anayejichua, tena katika Mwezi wa Ramadhani, anapaswa kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu Mlezi na kuacha kula na kunywa, lakini siku hiyo anatakiwa kuilipa. Wanazuoni wanakubaliana kwamba kama ataanza kujichua kisha akaacha bila kufikia mshindo, anapaswa kuleta toba kwa kosa hilo, lakini funga yake itakuwa haijatenguka.

Mtu aliyefunga anapaswa kujiweka mbali na mambo yanayotamanisha kama vile kutoangalia watu waliovaa nusu uchi, picha za utupu na asikaribishe mawazo yanayoweza kumfanya atamani kufanya tendo la ndoa ama kujichua. Kuhusu mtu kutokwa na madhii (majimaji ambayo si manii), wanazuoni walio wengi wanakubaliana kwamba hayatengui saumu ya mtu.

Kuhusu kifunguzi cha tatu, kula na kunywa, wanazuoni wanafafanua kwamba chochote kitakachofika tumboni kupitia mdomoni kitakuwa kimetengua saumu ya mtu. Hata Mtume (swallallahu alaihi wasallam) anasema: “Ingiza maji zaidi ndani ya pua (wakati unashika wudhu), isipokuwa unapokuwa umefunga.” Imesimuliwa na al-Tirmidhi, 788.

Kama maji yanayofika tumboni kupitia pua yangekuwa hayatengui swaumu, Mtume (Amani na rehema za Mwenyezi Mungu Mlezi ziwe juu yake) asingewaambia waliofunga wasizidishe maji ndani ya pua. Kuhusu yale yanayoingia pia kwenye kichwa cha habari ‘kula na kunywa’ yanahusisha mambo yafuatayo: Mosi, ni kuongezewa damu kwa mtu ambaye anafunga kama ametokwa na damu kwa wingi kiasi cha kutakiwa kuongezwa damu.

Hili linabatilishwa swaumu kwani damu inatokana na chakula na vinywaji. Pili, ni kulishwa chakula ama kitu mbadala wa chakula kwa njia ya mpira ama dripu. (Fatwa ya Shekhe Ibn Uthaymeen katika Majaalis Shahr Ramadhaan uk 70). Itaendelea Ijumaa Chanzo cha makala haya ni Mtandao wa Islam-questions and answers. Majibu ya maswali muhimu Mfungo wa Ramadhani

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi