loader
Picha

‘Mwenge haumuonei mtumishi wa umma’

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkorea amesema Mwenge wa Uhuru unaokimbizwa hapa nchini kwa ajili ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, haupo kwa ajili ya kumuonea mtu yeyote ama mtumishi wa umma. Mkorea aliyasema hayo jana katika kijiji cha Mwawile wilayani Misungwi wakati hafla ya makabidhiano ya mwenge huo kutoka kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwenda kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza.

Alisema mwenge upo kwa ajili ya kukagua na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa mapana ya nchi na wananchi wake. “Sisi kama viongozi wa Mwenge wa uhuru, tutafanya kazi kwa bidii na juhudi kubwa bila ya kumuonea mtu yeyote,” alisema na kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa mapokezi mazuri kwa kipindi chote ambacho wamekimbiza mwenge huo mkoani humo.

Akitoa salaamu za mkoa kwa kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kitaifa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio alisema jumla ya miradi 63 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 15.9 inatarajiwa kuzinduliwa na mbio za mwenge wa uhuru mkoani Mwanza. Alisema kati ya miradi hiyo itakayozinduliwa na mwenge huo wa uhuru unaotarajiwa kukimbizwa jumla ya kilomita 855.11 kwa nchi kavu na umbali wa majini maili 72, miradi 13 yenye thamani ya Sh bilioni 4.82 itawekewa mawe ya msingi.

Miradi 16 ya Sh bilioni 4.5 itazinduliwa, miradi 18 ya Sh bilioni 3.34 itafunguliwa na miradi 16 iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 na 2018 yenye thamani ya Sh bilioni 3.24 itafunguliwa. Mwenge wa uhuru ukiwa mkoani Mwanza kwa mwaka jana, ulitembelea miradi 56 yenye thamani ya Sh bilioni 13.68 ambapo katika miradi hiyo, miradi 17 iliwekewa mawe ya msingi, 17 ilizinduliwa, 12 ilifunguliwa na miradi 10 ilikaguliwa.

Alisema miradi hiyo yote imegharimikiwa na fedha kutoka Serikali Kuu Sh bilioni 9.4, michango ya halmashauri Sh bilioni 1.9, nguvu za wananchi Sh bilioni 3.40 na michango ya wahisani Sh bilioni 1.12. Alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19, makundi ya vijana 179 na watu wenye ulemavu 30 walipatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 479.3 na kuwanufaisha wanachama 1,883.

Kabla ya kukabidhi mwenge huo kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela alisema ukiwa mkoani Shinyanga mwenge huo umezindua, kuweka mawe ya msingi zaidi ya miradi 53 yenye thamani ya bilioni 47.5.

Alisema kati ya fedha hizo zilizotumika, nguvu za wananchi ni Sh milioni 447, mchango wa halmashauri Sh bilioni 4.4, Serikali kuu Sh bilioni 31.3, wahisani Sh bilioni 5.5 na sekta binafsi Sh bilioni 5.92.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Na Nashon Kennedy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi