loader
Picha

Yanga yafikiria ubingwa

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema nafasi ya kutwaa ubingwa kwa timu hiyo anaona bado iko wazi kwa kuwa kwenye soka lolote linawezekana.

Aidha, kocha huyo amesema kama figisu za kuihujumu timu hiyo zitakoma na waamuzi kutenda haki, chochote kinaweza kutokea na kwamba mpira una matokeo ya ajabu hata michezo waliyosaliwa nayo wapinzani wao Simba ambao wanaopewa nafasi kubwa kutwaa ubingwa, wanaweza kupoteza na kuwapa wao nafasi ya kutwaa taji hilo.

Zahera alitoa kauli hiyo baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam katika mwendelezo wa ligi hiyo na kuifanya timu hiyo kupanda kileleni kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya bingwa mtetezi, Simba.

Matokeo hayo yaliifanya Yanga kufikisha pointi 83 baada ya kucheza michezo 36 wakisaliwa na mechi mbili mkononi zitakazoamua hatma yao ya kutwaa ubingwa, huku wakimuombea mabaya Simba mwenye michezo mitano apoteze ili atwae taji hilo.

“ Kwenye mchezo wa leo (juzi) ulikuwa mgumu kwetu kwa sababu wachezaji walikuwa hawana ari ya kucheza kutokana na kuchoka baada ya kusafiri umbali mrefu bila kupata nafasi ya kupumzika kutoka mkoani Mara, nashukuru tumepata ushindi ambao unatufanya kuwa kileleni,” alisema Zahera.

Zahera aliwapongeza wachezaji wake licha ya kucheza chini ya kiwango, lakini walipambana bila kuchoka kwa dakika zote na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu, ambazo walikuwa wanazisaka kwa udi na uvumba.

Kwa upande wa kocha wa Ruvu Shooting, Mzanzibari Abdulmutik Haji aliwapongeza Yanga kwa kupata ushindi huo, huku akieleza sababu za kufungwa ni kwa wachezaji wake kushindwa kufuata maelekezo aliyowapa.

SERIKALI baada ya kufanya kikao na wadau wa michezo imesema ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi