loader
Picha

Kiungo Mbeya City aziita Simba, Yanga

KIUNGO mshambuliaji wa Mbeya City Idd Selemani (pichani) amesema timu yoyote iwe Simba au Yanga ikimuhitaji ijitokeze kufanya naye mazungumzo. Mchezaji huyo mkataba wake unaelekea ukingoni mwishoni mwa msimu huu ambapo alisema hakuna timu yoyote aliyofanya nayo mazungumzo mpaka sasa.

Akizungumza juzi, Selemani alisema timu yoyote itakayomuona na kuvutiwa na kipaji chake basi hawana budi kujitokeza kumalizana. “Ni kweli mkataba wangu unaelekea mwishoni na sijafanya mazungumzo yoyote, natarajia timu yoyote wakiniona na kuvutiwa na kiwango changu waje tuyamalize,”alisema.

Mchezaji huyo aliifungia timu yake bao la 10 juzi katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya na kuwapa matumaini ya kuendelea kubaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

Selemani amekuwa mwiba hasa kwa timu ngumu na kuipatia timu yake matokeo. Aliwahi kuifunga Yanga mara mbili msimu uliopita walipotoka sare ya bao 1-1 na yeye ndiye aliyesawazisha. Msimu huu aliifungia timu yake bao la kufutia machozi Yanga ilipoibuka na ushindi wa 2-1.

Na pia aliifungia timu yake bao moja katika mchezo dhidi ya Simba, wekundu hao walipoibuka na ushindi wa mabao 2-1. Alisema atafurahi kuona Mbeya City haishuki daraja na watapambana katika mechi za mwisho kuiwezesha timu yake kusalia kwenye ligi angalau katika sita bora.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi