loader
Picha

Mechi chungu, tamu Simba, Yanga

WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara inakaribia mwishoni wababe na vigogo wa muda mrefu Simba, Yanga ndio wanaokimbizana katika uongozi. Kila mmoja alikuwa na malengo Simba inataka kutetea taji na Yanga inataka kuchukua baada ya kulikosa msimu uliopita.

Lakini baadhi ya changamoto zilizojitokeza kupitia harakati zao za mapambano ya kutafuta pointi tatu kwa kila mechi, hazikuwa rahisi na wala sio rahisi mpaka sasa. Zipo mechi kadhaa walizopoteza ambazo walizipa matumaini kama wangeshinda wangekuwa sehemu fulani lakini walijikuta wakipata matokeo tofauti na matarajio yaliyowaumiza mashabiki wao.

SIMBA Vs KAGERA

Hamna kitu kinaumiza kama kupoteza mechi mbili kwa mtu mmoja ndani ya msimu mmoja. Mechi hii ni wazi kuwa iliwaumiza Simba kupita kiasi kwasababu walikuwa na matarajio ya kutaka kuvunja mwiko na kulipiza kisasi. Simba waliweka historia nzuri msimu huu ya kutopoteza mchezo wowote kwenye uwanja wa nyumbani lakini bado Kagera ndio waliovuruga mipango baada ya kufunga 1-0 ikiwa ni siku chache walitoka kuwafunga wekundu hao Kaitaba mabao 2-1.

Unaweza kusema Kagera ni timu pekee iliyoweka historia ya kuifunga Simba michezo miwili. Kagera sio mara ya kwanza kutibua shangwe za wanamsimbazi msimu wa 2016/2017 mechi ya mzunguko wa pili Simba ilihitaji ushindi ambao ungempa nafasi ya kuwa bingwa lakini matokeo yake walijikuta wakila kichapo cha mabao 2-1.

Kipigo hicho kiliwaumiza Simba kiasi kwamba walikata rufaa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka pointi tatu wapewe wao, wakidai mchezaji Mohamed Faki alichezeshwa akiwa na kadi tatu za njano. Lakini hawakufanikiwa baada ya kesi yao kutupiliwa mbali huku pia, wakisema wangekata rufaa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kitendo ambacho kiliishia hewani. Pia, msimu uliopita wakati wanakabidhiwa Kombe lao la ligi mbele ya mgeni rasmi Rais John Magufuli wakala tena kichapo cha bao 1-0.

Kiliwaumiza kupita kiasi kwasababu walitaka kumfurahisha Rais kwa kupata matokeo mazuri yenye shangwe za ubingwa.

SIMBA Vs AZAM FC

Wekundu hao waliamini wanaweza kupata pointi tatu mbele ya Azam baada ya mzunguko wa kwanza kuwafunga mabao 3-1. Lakini matokeo yaliishia sare ya 0-0. Hayakuwapendeza kwasababu miongoni mwa mechi tano walizotangaza kushinda na hizo zimo. Hata hivyo, bado Simba ina nafasi ya kutangaza ubingwa mapema katika mechi tatu zijazo kama itafanikiwa kushinda zote.

MBAO Vs SIMBA

Simba ilikuwa haijawahi kufungwa na Mbao zaidi ya ushindi na sare lakini msimu huu ikiwa imetoka kusajili majembe makali ilijikuta inaambulia kichapo cha bao 1-0 kwenye uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.

Ni mchezo ambao uliwaumiza mashabiki wa wekundu hao kwani ndio kwanza ulikuwa mwanzo wa ligi na huo ulikuwa ni mchezo wa nne tangu kuanza kwa msimu na wa kwanza kupoteza. Mashabiki wa kanda ya ziwa hakika walitamani kuona timu yao inapata ushindi kutokana na ubora wa kikosi hicho ulioanza nao. Lakini mpira ndivyo ulivyokuwa na matokeo hayo.

MECHI YA KIHISTORIA

Pamoja na uchungu wa mechi hizo za juu lakini Simba imeweka historia kwa mechi ya Coastal katika mchezo wake wa hivi karibuni uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru. Bila shaka wekundu hao walitoka wakiwa na furaha baada ya kushinda mabao 8-1 huku washambuliaji wawili Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wakiweka historia ya kupiga ‘hat trick’ katika mechi moja.

Hii ni mechi haitosahaulika na mpaka sasa Coastal Union ndio timu pekee iliyofungwa mabao mengi msimu huu. CHUNGU ZA YANGA, SIMBA Yanga baada ya mzunguko wa kwanza kutoka suluhu dhidi ya Simba, mzunguko wa pili wakala kichapo cha bao 1-0.

Ni kichapo kilichowaumiza mashabiki wa timu hiyo kwasababu walitoka kuonyesha Simba kuwa licha ya kuwa wanapesa hawana lolote mbele ya timu isiyokuwa na pesa. Walitaka kuonyesha kuwa wao sio dhaifu wanaweza kupambana na kikosi cha bilioni kama ilivyokuwa inasemwa kwa matani yao. Lakini mwisho wa siku Simba iliibuka mbabe.

STAND Vs YANGA

Yanga iliumizwa na matokeo ya bao 1-0 iliyofungwa na Stand United kwani yalivuruga mipango yao kwasababu walitaka kuendeleza ubora wao ili kusimama pazuri. Sio mara ya kwanza kufungwa kwenye uwanja wa CCM, Kambarage Shinyanga kwani msimu wa 2015/2016 waliwahi kufungwa tena bao 1-0. MTIBWA Vs YANGA Hii mechi ilichezwa kwenye uwanja wa Jamhuri na Yanga kufungwa bao 1-0.

Ni miongoni mwa michezo iliyotibua mipango yao katika harakati za kuwania taji kwasababu walihitaji ushindi kuwahakikishia nafasi ya kupigania taji. Kitendo cha kupoteza japo walikuwa wanajitia moyo lakini mipango yao ilianza kuvurugika.

LIPULI Vs YANGA

Kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Lipuli kwenye uwanja wa Samora, mkoani Iringa kiliwaumiza mno mashabiki wa Yanga na mpango wao katika vita ya kuwania taji la ubingwa ikaanza kutoweka. Walijiona sasa harakati zao za kuwania taji zinaweza kuwa ngumu hasa ikizingatiwa kwamba watani zao walikuwa na viporo vingi hivyo, walianza kukata tamaa kwa kuona kuwa huenda wasiwe tena na nafasi ya ubingwa.

Ni wazi kama wangeshinda pengine ingefufua matumaini japo kidogo lakini mwenendo huo uliwavuruga. Mbaya zaidi Lipuli ikaja tena ikawachapa mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho kipigo kilichofanya kutolewa kabisa kwenye mashindano hayo. Hawataisahau Lipuli namna ilivyopoteza mipango yao lakini ndivyo mpira ulivyo kuna wakati una matokeo ya kufurahisha na muda mwingine matokeo ya kikatili.

BIASHARA Vs YANGA

Hata walipokuja kupoteza mchezo huu kwa bao 1-0 hivi karibuni ni kama tayari hawakuwa tena na matumaini. Matumaini yao yameibuka upya baada ya Simba kupoteza mchezo dhidi ya Kagera na kupata sare 0-0 dhidi ya Azam FC lakini kuna kazi kubwa.

Mechi tamu kwa Yanga ni dhidi ya Mbao. Ilikuwa ni furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kufanikiwa kuvunjwa mwiko msimu huu na kuwafunga Mbao mabao 2-1 kwenye uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza. Bado ligi haijaisha huenda kuna mechi nyingine zikaongezeka za vilio kwa timu zote mbili. Kuelekea mwishoni mwa msimu mambo huwa ni magumu mno.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi