loader
Picha

Zahera- Makambo aliomba nimsindikize

KOCHA Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema baada ya mshambuliaji wake Haritier Makambo kupata ofa katika klabu ya Horoya AC ya Guinea alimuomba amsindikize ili asitapeliwe.

Zahera aliyerejea jana alfajiri na mchezaji huyo wakitokea Guinea aliweka wazi kuwa hakwenda huko kwa mapenzi yake mwenyewe bali mchezaji ndiye aliyemuomba msaada.

“Makambo mwenyewe aliomba akaniambia Kocha nimepata ofa naomba unisindikize ukanisaidie nisije nikatapeliwa, nami nikaona kweli hawa vijana wadogo wanaweza kudanganyika,”amesema.

Akizungumzia kama tayari ameshasaini, alisema sio kweli kwani alikwenda kufanyiwa vipimo na mazungumzo hivyo wameleta taarifa kwenye uongozi kuamua kwasababu bado ni mchezaji wa Yanga mwenye mkataba.

Alisema kama Yanga wakiamua kumuuza basi fedha zitakazopatikana zitakuwa ni kwa ajili ya klabu na zitasaidia katika usajili mpya kwa kutafuta wachezaji wengine wenye uwezo huku akikanusha taarifa za kuwa mchezaji huyo alikuwa akicheza kwa mkopo akitokea Motema Pembe ya DR Congo kama zinavyozagaa mitandaoni.

Alitolea ufafanuzi kuwa ikiwa mchezaji analipwa kwa mfano Sh 100 na akapata kwingine wakatoa ofa kubwa zaidi sio mbaya kwa mchezaji kilichobaki ni maamuzi ya muhusika na viongozi kuamua kwani bado wanaweza kumbakisha wakikubaliana.

Hata hivyo, alikataa kutaja kiwango cha mauzo ya mchezaji huyo akisema litakuwa ni suala la uongozi wa Yanga kama litaafikiana na klabu husika na sio jukumu lake kusema.

Hivi karibuni kulikuwa na taarifa juu ya mchezaji huyo kuwa tayari amesaini mkataba wa miaka mitatu katika klabu hiyo baada ya kuonekana picha akiwa anasaini na amevaa jezi zao.

Tayari Mwenyekiti wa Yanga Mshindo Msolla aliweka wazi juzi kuwa hakuna maafikiano yoyote kwasababu alichokuwa anajua mchezaji alikwenda kufanyiwa vipimo vya afya hivyo hakukua na makubaliano yoyote mpaka mazungumzo ya pande mbili yatakapokamilika.

Alisema kuna ofa nyingine mezani na kwamba wataangalia dau litakalonona ndilo watakubaliana.

NBA iko kwenye mazungumzo ya kuanza tena msimu kwenye hoteli ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi