loader
Picha

Simba yasaka pointi za ubingwa

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC, leo watakuwa katika Uwanja wa Uhuru kumenyana na Ndanda FC, mchezo ambao kama watashinda watazidi kujitengenezea nafasi nzuri ya kuutetea ubingwa wao kwani watabakiza pointi moja kuutwaa.

Ili Simba ijihakikishie ubingwa inatakiwa kufikisha pointi 89 ambazo hata ikifungwa mechi zilizosalia bado itakuwa bingwa kutokana na hazina kubwa ya mabao iliyojiwekeza.

Yanga inao uwezo wa kufikisha idadi hiyo ya pointi ikishinda mechi zake zote lakini lazima iwe na idadi kubwa ya mabao kuizidi Simba, jambo ambalo ni gumu.

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 85 ilizozikusanya katika michezo yake 34 ilizocheza ikifuatiwa na Yanga iliyo nafasi ya pili na pointi zake 83 ikiwazidi Simba michezo miwili.

Ligi Kuu Tanzania inayoshirikisha timu 20 inaitaka kila timu kucheza mechi 38 ili kukamilisha msimu hivyo kama Simba watapata pointi nne katika mechi ya leo na inayofuata itakuwa mabingwa hata kabla haijamaliza mechi zake.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kumaliza dakika 90 kwa suluhu.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema anajua mashabiki wa timu hiyo wanachokihitaji ambacho si kingine bali ni ushindi, atahakikisha wanafanya hivyo licha ya ratiba kuwabana kwa kuwalazimu kucheza mechi nyingi ndani ya kipindi kifupi.

“Tunajua tuna muda mfupi ambao unatubana hata kufanya maandalizi ya nguvu, lakini kwa kuwa tunajua umuhimu wa mechi zetu zilizopo mbele yetu inatulazimu kupambana kivyovyote na kupata ushindi,” alisema Aussems.

foto
Mwandishi: Mohammed Mdose

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi