loader
Picha

'Askofu’ kuzikwa Jumatatu Mbuguni

MAZIKO ya aliyekuwa mmiliki wa timu ya Pallson ya Mbuguni wilayani Arumeru mkoani Arusha, Thomas Mollel maarufu Askofu yanatarajiwa kufanyika Jumatatu, nyumbani kwake Mbuguni.

`Askofu’ ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya tanzanite na mmiliki wa migodi hiyo iliyoko wilayani Simanjiro mkoani Manyara, alifariki juzi mkoani Dodoma baada ya kuanguka ghafla bafuni saa 4 usiku sehemu alikofikia. Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya ya kichama ya Meru, Shabani Mdoe alisema kuwa kwa sasa chama kinaangalia namna ya kusafirisha mwili huo kwa njia ya ndege hadi katika Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA).

Mdoe alisema ratiba ya ndege inaonesha kuwa mwili utawasili Arusha Jumapili Mei 26. Alisema kwa sasa wanakaa na familia kuangalia kama watakubaliana na ratiba hiyo na kama itashindikana, basi kuna uwezekano wa kusafirisha mwili kwa njia ya barabara ili mwili uweze kuja mapema Arusha kuwahi maziko siku ya Jumatatu kama ilivyopangwa.

Katibu alisema Askofu ambaye aliwahi kuwa diwani na kabla ya mahuti kumkuta alikuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Meru alikwenda Dodoma na wafuasi wengine kumsindikiza Mbunge mteule Dk John Pallangyo aliyepita bila kupingwa kwenda kuapishwa bungeni.

Alisema `Askofu’ mbali ya kuwa mwanasiasa ni mpenzi mkubwa wa soka na alianzisha timu ya Pallson iliyotamba hadi Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini sasa timu hiyo haiko tena katika ulimwengu wa soka.

Naye Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Zakharia Mjema alisema chama kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha `Askofu’ kwani alikuwa mdau mkubwa wa soka mkoani Arusha na msaada mkubwa kwa chama cha soka. Alisema kuwa mmiliki huyo wa Pallson atakumbukwa kwa mambo mengi katika tasnia ya soka mkoani Arusha na nchi kwa ujumla kuwataka wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi siku ya mazishi ya mpenzi huyo wa soka Arusha ikiwa ni njia ya kumuenzi.

Naye mchezaji wa zamani wa Pallson, Fidelis Nzowa maarufu kwa jina la Chief amepokea taarifa ya kifo cha `Askofu’ kwa masikitiko, kwani alikuwa sio mmiliki tu wa timu bali alikuwa mzazi kwa wachezaji wote waliowahi kuichezea timu hiyo. Naye Denis Shemtoe timu Meneja wa zamani wa timu ya AFC ya Jijini Arusha alisema anamfahamu vizuri Askofu na kamwe pengo lake halitazibika katika soka la Mkoa wa Arusha.

TIMU ya taifa ya Tanzania kwa wachezaji wenye umri wa ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi