loader
Picha

Terminal 3 JNIA kukabidhiwa mapema

JENGO la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3, Dar es Salaam litakabidhiwa mapema tofauti na ilivyoelezwa awali.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema, jengo hilo, ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka, litakabidhiwa Mei 29, ikiwa ni siku moja kabla tarehe ya awali iliyoahidiwa na mkandarasi.

Awali, mkandarasi aliahidi kukabidhi jengo hilo, Mei 30 kwa wamiliki, ambao ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi na Rais John Magufuli baadaye mwaka huu.

Tayari ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia 99.5 na sasa vitu vikubwa vinavyofanyika ni kufunga vifaa mbalimbali, vikiwemo vile vya usalama, milango, viti na vile vya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Alisema kuwa tayari ujenzi umeshakamilika na watu wa TCRA, Shirika la Mawasiliano nchini (TTCL), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wengineo wanaweka mifumo yao ya huduma ili kukamilisha ujenzi huo.

“Mtendaji Mkuu kwa sasa anahangaika na watoa huduma na wanaotakiwa ni wale wenye uwezo mkubwa na ambao hawafanyi kazi kwa mazoea na ni bora wakapatikana vijana wa kitanzania wenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma katika jengo hilo bora kabisa na la kisasa,“ alisema Kamwelwe baada ya kukagua jengo hilo.

Alisema baada ya Mei 29, wataanza kufanya majaribio ya matumizi mbalimbali katika jengo hilo, ambalo halina tofauti kabisa na majengo ya viwanja vya Ulaya na nchi nyingine zilizoendelea.

Pia Kamwelwe alisema baada ya kukamilika kwa jengo la terminal 3, ujenzi utahamia katika terminal 2, ambalo lenyewe litatumika kwa ajili ya abiria wa hapa nchini ambao wanatoka na kuwasili kutoka mikoa mbalimbali.

Terminal 3 ina madaraja 12, ambayo yana uwezo wa kuegesha ndege kubwa za idadi hiyo kwa wakati mmoja pia kutakuwa na mageti 16 ya kuingilia na kutokea katika ndege. Alisema kuwa katika kudhihirisha kuwa ujenzi wa terminal 3 tayari umekamilika, wafanyakazi wamebaki 1,000 kutoka 2,900, ambao walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali za ujenzi.

Waziri alisema ameridhishwa kabisa na maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo na baada ya Mei 29, TAA itakuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali kwa ajili ya watoa huduma uwanjani hapo.

Waziri alipotembelea jengo hilo alishuhudia watu wa TCRA, Idara ya Uhamiaji na wengineo wakifunga vifaa vyao, tayari kutoa huduma wakati wowote kiwanja hicho kitapoanza kutumika. Juni Mosi wataanza kutoa huduma kwa majaribio uwanjani hapo, hasa kujaribu mifumo mbalimbali kabla ya kutoa taarifa kwa Rais Magufuli kuuzindua jengo hilo la tatu la abiria.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads), Crispin Akoo alisema kutokana na maendeleo mazuri ya ujenzi, mkandarasi anatarajia kukabidhi jengo mapema.

Kuhusu maandalizi ya uendeshaji Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Julius Ndyamukama alimweleza Waziri Kamwelwe kwamba majaribio na maandalizi ya uendeshaji yalianza tangu Machi, mwaka 2018 na yapo katika hatua za mwisho.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kimesema, mkoa wa Pwani una ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi