loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wapigakura huchagua mtu au chama?

NIMEPATA kuuliza swali hilo mtandaoni na likaamsha mjadala mkubwa.

Kwenye mjadala huu niliangalia matokeo ya uchaguzi wa Afrika Kusini mwaka huu na kulinganisha na uchaguzi wetu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 2015.

Nionavyo, kwa kuangalia vyama vya CCM na ANC tunawaona wagombea wawili; John Magufuli na Cyril Ramaphosa walioingia madarakani kwenye mazingira yanayofanana. CCM na ANC vyote ni vyama tawala vikongwe.

Kwa historia vimekuwa kimbilio la wanyonge. Kwa CCM ilifika wakati baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho walianza kutenda kinyume na mahubiri yao.

Hawakuishi tena kama walivyohubiri. Wakaitumia siasa kufanya biashara na kujinufaisha binafsi. Jambo baya zaidi, CCM kama chama kikagubikwa na kashfa nyingi za ufisadi uliofanywa na watendaji waliotokana na chama.

Kero namba moja ya wapigakura ikawa rushwa na ufisadi. Wapigakura wa CCM wakaanza kuonesha wazi kukichoka chama chao hicho.

Wakamtaka mtu atakayesimama upande wao, na kwa utendaji wake wana imani angepambana na rushwa na ufisadi na kuwaletea maendeleo.

Karata ilimwangukia Rais John Magufuli. CCM iliyokuwa kwenye hatari ya mgombea wake kupata chini ya asilimia 50 na wabunge wake wengi kuangukia pua na hata kukosa majority bungeni, mgombea wake urais, John Magufuli akapata asilimia 58 na wabunge wakawa wengi kutengeneza majority (wingi).

Miaka mitatu ya Magufuli imepita bila wapigakura wa Watanzania kusikia habari za kashfa kubwa za rushwa na ufisadi kwenye nchi.

ANC kwa upande wake kuelekea uchaguzi wa mwaka huu ilikumbwa na hali kama ya CCM.

ANC ilianza kuchokwa na wapigakura wake walioanza kuegemea zaidi kwa EFF ya Julius Malema yenye mrengo wa kushoto wa itikadi kali na hata wapigakura wa ANC wa tabaka la kati walianza kufikiri kuwapigia Democratic Allianze (DA) wenye mrengo wa kihafidhina.

Mwandishi na mchambuzi William Gumede kabla ya uchaguzi wa Afrika Kusini alitamka kuwa ANC kabla ya ujio wa Rais Ramaphosa walikuwa kwenye hatari ya kupata asilimia 40 au chini ya hapo.

Wangekosa wingi bungeni. Wapigakura wa ANC walirudisha imani yao kwa ANC kupitia rekodi ya kiutendaji ya mgombea wao, Rais Ramaphosa ambaye amegombea akiwa na ajenda mbili kubwa: Mosi, kurekebisha hali ya uchumi na pia kupambana na rushwa na ufisadi hata ndani ya chama chake.

Katika uchaguzi, ANC ikapata asilimia 57. Cyril Ramaphosa akawa ameiokoa ANC kutoka kwenye hatari ya kuanguka. Swali linalobaki ni kwa namna gani marais Ramaphosa na Magufuli watatumia umaarufu wao binafsi kuviimarisha vyama vyao? Na ni kwa namna gani wataweka misingi ya uwepo wa vyama vya siasa vilivyojikita kiitikadi?

Na mara nyingi hatujiulizi swali hili; siasa ni nini? Kwenye kitabu chake cha mwaka 1962; ’ TUJISAHIHISHE’, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere anaandika;

”Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia umoja (chama) wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, nk, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi.”

”Swali ambalo twalisikia mara kwa mara; ” Hali yetu ya baadaye itakuwaje?

Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye (mwananchi) jambo fulani kama tuzo! Anasahau kabisa kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla.

Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya Jumuiya, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi.

Kama wanachama wa TANU, hasa viongozi, hawatakihukumu chama chetu kwa mahitaji ya jumii yao, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, hakitadumu.

Wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama.” Mwl. Nyerere anaendelea; ” Dalili nyingine ya ubinafsi, na ambayo ni ugonjwa mbaya sana, ni fitina.

Kanuni moja ya TANU inasema; ”Nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko.” Lakini bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua.” (J.K Nyerere Tujisahihishe 1962). Nini adili ya maneno ya Mwalimu? Misingi ya kisiasa hujengwa na itikadi.

Vyama vyetu siku hizi haviongozwi na itikadi bali matashi ya mtu mmoja mmoja, vinaongozwa kama taasisi binafsi. Itikadi ni kama zimekufa. Tunasahau, kuwa lililo kubwa kabisa kuzidi yote ni Dola- State.

Ni nchi tuliyozaliwa na tunayopaswa kuwa tayari kuipigania, wakati wowote. Inashangaza sana siku hizi, baadhi ya wenye kuitwa viongozi wanakuwa mbele kuiponda nchi, kuidhalilisha dola.

Ni kana kwamba wana nchi nyingine za kukimbilia ya kwetu ikiangamia. Hii ni nchi kubwa kuliko hao wenye kututoa kwenye reli ya kufikiri kama taifa moja. Tukiwaendekeza tutaifikisha nchi yetu kusiko kwema.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi