loader
Picha

Marufuku mifuko ya plastiki vita ya kiuchumi

SERIKALI imesema uamuzi wa kupiga marufuku uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki ni vita vya kiuchumi, kwa kuwa jambo hilo limekuwa likipingwa tangu mwaka 2003.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayehusika na Muungano na Mazingira, January Makamba kwenye kikao na wahariri wa vyombo vya habari.

Makamba amesema operesheni hiyo, inagusa maslahi ya kiuchumi ya baadhi ya watu wakiwemo wazalishaji na wauzaji wakubwa, ambao hawako tayari kuona mifuko hiyo inapigwa marufuku hapa nchini.

Waziri huyo alisema biashara ya mifuko ya plastiki ni moja kati ya biashara kubwa zilizokuwa zikifanyika kimagendo kwa muda mrefu kutokana na kuwepo kwa viwanda bubu vingi ambavyo vilikuwa havilipi kodi.

Alisema katika uchunguzi wao walibaini kuwepo kwa viwanda bubu zaidi ya 100, ambavyo vingi viko kwenye majumba ya watu.

Alisema kiwanda kidogo tu kinaweza kuzalisha maelfu ya tani ndani ya saa moja.

“Jambo hili ni gumu kwa sababu tulijaribu kuiondoa mifuko hii tangu mwaka 2003, lakini tukashindwa kwa sababu hii ni moja ya biashara kubwa iliyokuwa ikifanyika kwa njia za magendo. Tunawaomba wananchi watuunge mkono na watoe taaarifa kama watabaini kuna mtu anazalisha mifuko hii au ameihifadhi,” alieleza Makamba.

Makamba alisema serikali imepata taarifa kwamba kuna watu wamejipanga kufanya kampeni ya kupinga operesheni hiyo kuanzia Juni mosi, kwa kuwa wana maslahi na biashara hiyo.

Alisema wamejipanga kukabiliana na jambo hilo, kwa kuwa kinachofanyika ni operesheni ya kitaifa kwa maslahi ya taifa zima.

Alisema jambo hilo linawapa wasiwasi baadhi ya watu, kwa kuwa litawalazimu kubadilika kitabia kutokana na mifuko hiyo kuwa sehemu ya maisha yao kwa muda mrefu na imewaathiri kitabia, kama ilivyokuwa kwa watumiaji wa madawa ya kulevya.

Alisema kwa kuwa watu walizoea kwenda sokoni, madukani au magengeni mikono mitupu, wakijua watapata mifuko ya kubebea bidhaa zao huko huko, hivyo kuondolewa kwake itawalazimu watu kubadilika kitabia na kuanza kutumia mifuko mbadala.

Kwa kuwa lengo la serikali lilikuwa kuiteketeza mifuko hiyo baada ya kukusanywa kutoka kwa wauzaji na wananchi, Makamba alisema jambo hilo halitafanyika, kwa kuwa kuna kampuni tatu zimejitokeza zitakazotumia mifuko hiyo kuzalisha mabomba ya maji na madawati.

Alilitaja moja ya kampuni hizo kuwa ni Kampuni ya Falcon iliyopo jijini Mwanza na kuwataka watu wenye shehena kubwa ya mifuko hiyo, kuipeleka kwenye kampuni hizo.

Alisema katika kipindi cha kuanzia Juni mosi hadi Julai mosi, mkazo mkubwa utakuwa kwenye kuiondoa mifuko hiyo na baada ya operesheni hiyo kukamilika, itafuata kazi ya kuondoa taka za mifuko ya plastiki zilizotupwa maeneo mbalimbali kama vile kwenye mitaro na mito.

Kwa upande wake, Mtekelezaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Dk Madoshi Makene, alisema wamiliki na wauzaji wakubwa wa mifuko ya plastiki, walishapewa taarifa na walijaza fomu maalumu kuhusu katazo hilo, hivyo atakayekiuka jambo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.

Dk Makene alisema mifuko ya plastiki, ina madhara makubwa, kwa kuwa ikipigwa na jua au ikiwekwa kwenye jokofu au kutumika kuwashia moto inatoa mionzi mingi ya hatari.

Alisema mionzi hiyo inaathiri kiafya kwa binadamu, ikiwemo kupata saratani na kuharibu nguvu za uzazi kwa wanaume na wanawake kwa kuwa inatengenezwa kutokana na mabaki ya mafuta ya petroli.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kimesema, mkoa wa Pwani una ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi