loader
Picha

Serikali yakabidhiwa Terminal III

JENGO la tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) limekabidhiwa rasmi kwa serikali tayari kwa matumizi baada ya ujenzi wake kukamilika.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Julius Ndyamukama amesema jana mkandarasi alikabidhi kwa Wakala wa Barabara (Tanroads) na kisha kwa TAA.

“Leo (jana) mkandarasi anatakiwa amalize akabidhi kwa Tanroads ambaye ndiye mwajiri wake. Tanroads watatukabidhi leo saa 8,” alisema Ndyamukama na kuongeza kuwa hatua hiyo imekamilika siku mbili kabla ya tarehe ya mwisho iliyopangwa ambayo ni Mei 31.

Kampuni ya Kimataifa ya BAM kutoka Uholanzi, ndiyo iliyojenga jengo hilo, ambalo limekamilika ndani ya wakati na kukidhi matakwa ya mkataba. Msimamizi wa ujenzi huo ulioanza mwaka 2013, ilikuwa Kampuni ya Arab Consulting Engineers ya Misri. Mkandarasi (BAM) alitakiwa kukabidhi jengo kwa serikali Mei 31.

Alipotembelea kiwanja hicho hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema jengo hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka, litakabidhiwa Mei 29; hatua ambayo imetekelezwa.

Katika ziara hiyo, waziri alisema baada ya Mei 29 (leo), TAA wataanza kufanya majaribio ya matumizi mbalimbali katika jengo hilo.

Aidha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea uwanja huo Machi mwaka huu, alitaka TAA kukamilisha taratibu za kuanza kutumika kwa jengo hilo akisisitiza kwamba mkandarasi akishakabidhi kwa serikali, lianze kutumika mara moja.

Jengo la tatu la abiria na eneo jipya la kutua, kushushia abiria na kuegesha ndege la JNIA, limewekewa huduma na mifumo ya kisasa, ikiwamo ya kiusalama na kufanya kiwanja kuwa cha aina yake katika Afrika Mashariki.

Kitahudumia abiria milioni sita kwa mwaka huku yakiwapo maegesho ya magari 2,075 kwa wakati mmoja. Miongoni mwa huduma zilizowekwa ni mifumo ya mawasiliano ya kisasa huku kukiwa na mifumo ya ukaguzi inayowezesha kuhudumia abiria 2,800 kwa saa.

Zipo mashine zinazowezesha wenye pasipoti za kielektroniki kujihudumia haraka bila kusubiri kukaguliwa na watumishi wa uhamiaji.

Aidha eneo la uchukuaji mizigo lina mikanda minne yenye urefu wa meta 80 inayowezesha watu wengi kuchukua mizigo kwa wakati mmoja.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kimesema, mkoa wa Pwani una ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi