loader
Picha

Muundo mikataba ya gesi wapitiwa upya

SERIKALI kwa sasa iko katika hatua ya kuchambua na kupitia upya muundo wa kifedha na kiuchumi, utakaotumika kwenye mikataba ya uchimbaji na utafutaji wa gesi ili kuweza kuinufaisha nchi.

Aidha, serikali imebainisha kuwa imejiandaa na haina wasiwasi kwenye malipo ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rufiji.

Akijibu hoja wakati wa kuhitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Aderaldus Kilangi alisema hatua hiyo imetokana na kubaini upungufu uliokuwepo ndani ya mikataba hiyo baada ya serikali kupitia upya.

“Hatua ya kuchambua muundo ni katika kutekeleza mapendekezo ya kamati iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuchunguza namna taifa inavyoweza kunufaika kwenye sekta ndogo ya gesi na uvuvi,” alisema.

Dk Kilangi alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), kuhusu sababu ya serikali kutotoa leseni mpya za uchimbaji na utafutaji gesi.

“Moja ya mapendekezo ya kamati uliyoiunda (Spika Ndugai) kuchunguza sekta ndogo ya gesi na uvuvi, ni kurejea mikataba ya utafutaji na uchimbaji na kazi hiyo ikapewa ofisi ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali). Tulianza kazi kuipitia mikataba yote, tukaunda timu kutoka wizara na sekta mbalimbali za serikali,” alisema.

Dk Kilangi alisema kuwa ofisi yake ililazimu kuijengea uwezo timu hiyo baada ya kupitia mikataba yote 11 ya utafiti na uchimbaji gesi.

“Tuligundua kuna kitu muhimu kukiangalia ambacho ni “Economic and Financially Modeling (muundo wa kiuchumi na kifedha). Siri nzima ipo hapo kama tunapata au kupoteza, hivyo tukaja na awamu nyingine ili ifanye kazi kwa mwezi mmoja.

“Tulichokifanya ilikuwa kuangalia muundo gani wa kifedha na kiuchumi uliotumika ikagundulika lazima kama nchi kuangalia inapendekeza mfumo upi ambapo kazi hiyo itafanyika kuanzia Juni 6 hadi 25 mwaka huu,” alisema. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema serikali imejiandaa na haina wasiwasi kwenye malipo ya mradi wa kuzalisha umeme wa mradi wa Rufiji.

“Tumeshalipa Sh bilioni 723. Si kama tumefanya makosa hapana. Serikali ilikuwa inafahamu kuwa bajeti iliyopitishwa ni Sh bilioni 700 kamili. Tumefanya hivyo kwa sababu ya umuhimu wa mradi huu.

“Kuhusu na hizo Sh bilioni 28 zinazodaiwa kutolewa bila ridhaa ya bunge, mamlaka ya kufanya uamuzi wa kuhamisha mafungu ni ya Waziri wa Fedha na Mipango. Unapokuwa na jukumu la msingi ambalo halipaswi kusubiri yapo mamlaka kwa waziri ambaye alihamisha fedha kutoka fungu 21 hazina kwenda fungu 58,” alisema.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mussa Sima alisema Mradi wa Kuzalisha Umeme kwenye Mto Rufiji, una umuhimu mkubwa kwenye uchumi wa nchi.

Alisema madai kuwa utekelezaji mradi huo, utavunja mkataba wa mbuga ya Selous kuwa urithi wa dunia si kweli, bali mkataba ulikuwa tayari.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kimesema, mkoa wa Pwani una ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi