loader
Picha

Wanaowapa mimba wanafunzi waadhibiwe

KASI ya wanafunzi kupata ujauzito katika shule za sekondari na msingi mkoani Mwanza imezidi kuwa kubwa ambapo wanafunzi 412 wametajwa kupata mimba katika mwaka mmoja tu wa 2018.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akitoa taarifa ya hali ya taaluma mkoani humo kwenye mkutano wa wadau wa elimu Mwanza.

Tumeguswa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaopata ujauzito na tunaungana na uongozi wa elimu na serikali mkoani Mwanza kukemea.

Vitendo vya kuwapa ujauzito wanafunzi shuleni havipaswi kuvumiliwa hata kidogo ndio maana tunaiomba jamii kuungana na serikali kuvipiga vita ili wasichana waweze kusoma na kumaliza. Haiingii akilini katika mkoa mmoja tu ndani ya mwaka mmoja kuwe na matukio ya wasichana 412 waliopata ujauzito huku jamii ikiangalia tu.

Tunasema haiingii akilini kwa sababu chanzo cha mimba hizo kinajulikana, wanafunzi hao kufanya ngono na watu wazima.

Ni kutokana na hilo tunasema, wanaume hasa watu wazima wa mkoa wa Mwanza wanapaswa kuchukua hatua kukabili hali hii mbaya haraka.

Na hii isiishie kwa wanaume wa Mwanza tu, bali wa nchi nzima kwani tatizo la mimba si la mkoa huo tu bali liko mikoa mingine nchini.

Ndio maana tunasema, jamii nzima inapaswa kuchukua hatua kali kupambana na wanaume wote wakware wanaoharibu maisha ya mabinti.

Kwa kupata mimba, ndoto za wasichana walio shule kuendelea na masomo zinafifishwa au hata kufa kwa sababu wanakatizwa masomo.

Ni vyema kila mtu nchini kwa nafasi aliyonayo, wazazi, wanafunzi, walimu na walezi wengine wakiwemo viongozi wa elimu wakatafakari hili.

Idadi ya wanafunzi 412 kupata mimba ndani ya mwaka mmoja kwa mkoa mmoja tu ni kubwa mno na haipaswi kufumbiwa macho iendelee tu.

Ni matarajio yetu kuwa vyombo vya ulinzi na usalama na asasi za kiraia za masuala ya elimu na haki za watoto zitalifanyia kazi suala hili.

Zichukue hatua kwa watu wote waliohusika na kuwaharibia maisha mabinti hao iwe fundisho kwa wakware wengine wenye tamaa na mabinti.

Kuchukua hatua kali kwa wakware ndio njia pekee ya serikali kukomesha uhalifu huu wa kijinsi, unaoharibu mipango ya serikali kuandaa wasomi hasa wanawake kwa gharama kubwa.

KITUO cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinajitahidi sana kuboresha shughuli za ...

foto
Mwandishi: Tahariri,

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi