loader
Picha

Amani na utulivu wa mfungo uwe endelevu

WAUMINI wa dini ya Kiislamu Tanzania wameungana na waumini wenzao duniani kwa ujumla wake kuhitimisha kwa amani na utulivu mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitr.

Akizungumzia sikukuu hiyo muhimu aliposhiriki swala ya Iddi katika msikiti wa Anwar, Dar es Salaam na baadaye Baraza la Idd lililofanyika ukumbi wa Tanga Beach Resort Tanga jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwakumbusha waumini hao kuendeleza mema waliyofanya wakati wa mfungo na pia kuwakumbuka wenye shida, wakiwamo yatima na wajane.

Alisisitiza kwamba utulivu uliojitokeza katika Mwezi Mtukufu uwe uendelevu kwa kuwaweka pamoja na kuimarisha mshikamano na kuvumiliana katika jamii nzima ya Watanzania.

Tunapenda kuungana na Waziri Mkuu kukumbushana pia kwamba ni utamaduni wa Watanzania kuishi na kushirikiana katika shida na raha tangu uhuru bila kubaguana na kupambana kwa misingi ya tofauti za rangi, dini, ukabila na itikadi za kisiasa.

Utamaduni huu umeweka Watanzania katika mshikamano wa aina yake kiasi cha kuigwa na mataifa mengine.

Mahubiri yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa na viongozi wetu wa serikali, dini, jamii na siasa katika sherehe hizo za Idd, ziendelee kudumishwa kwa manufaa ya wananchi na jamii kwa ujumla na atakayejaribu kuleta mfarakano katika mshikamano na utamaduni huu mzuri kwa nchi yetu asipewe nafasi.

Tunaeleza hayo kutokana na ukweli kwamba nchi za wenzetu wengine zimo katika mivutano, mifarakano na hata vita kutokana na kuendekeza masuala ya kibaguzi yaliyotajwa hapo awali.

Katika hili, tunatoa mwito kwa Watanzania wote kuwa walinzi wa mambo yanayotuweka pamoja kwa kuwadhibiti wale wanaoota kutaka kututenga na mshikamano huu.

Umoja na mshikamano wetu ulituwezesha kuzisaidia pia nchi karibu zote za kusini mwa Afrika kukabiliana vilivyo na vita dhidi ya wakoloni hadi vilivyomalizika na kuziacha nchi hizo kuwa huru kutokana na ukoloni uliokuwa unawakabili.

Hakuna ubishi kwamba siri ya mafanikio hayo ni umoja na mshikamano wa bila kubaguana tulioujenga kwa vitendo na hivyo kutufanya tulazimike sasa kuwa walinzi kwa kumtaja yeyote anayelenga kutusambaratisha kwa misingi ya ubaguzi.

Ni vizuri kukumbuka methali ya wahenga wetu isemayo ‘Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’.

Tunapenda pia kuchukua fursa hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wakiwemo polisi kwa kusimamia matukio yote mawili ya mafungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sherehe za Idd kwa usalama unaostahiki, kiasi cha wananchi kwa kiwango kikubwa kusherehekea kwa amani na usalama.

KITUO cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinajitahidi sana kuboresha shughuli za ...

foto
Mwandishi: Tahariri,

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi