loader
Picha

Serikali ilivyorejesha hadhi ya vyuo vya ualimu nchini

Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Vyuo vya Ualimu nchini umerejesha hadhi na heshima kwa wanachuo na wakufunzi katika vyuo hivyo.

CASMIR NDAMBALILO wa Idara ya Habari, MAELEZO anaelezea jinsi mradi huo ulivyowajengea mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia wanachuo na wakufunzi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

CHUO cha Ualimu Mpuguso ni miongoni mwa vyuo vinne vinavyotekeleza awamu ya pili ya Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Vyuo vya Ualimu Nchini.

Vyuo vingine vinavyotekeleza mradi huo wenye thamani ya Sh 36,475,000,000 ni pamoja na Kitangali wilayani Newala, Ndala wilayani Nzega na Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga.

Awali, chuo hiki ambacho kipo katika kijiji cha Mpuguso, umbali wa kilometa 11 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe, kilikuwa kinatumia majengo ambayo yalijengwa mwaka 1926 kwa ajili ya kutoa elimu kwa watoto wa machifu.

Akielezea kuhusu ujenzi na ukarabati huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo unaotarajia kukamilika mwaka huu unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa za kupata nafasi ya kujiunga na mafunzo ya ualimu.

Waziri Mkuu anasema mradi huo utasaidia, sio tu kuongeza fursa za wanafunzi kusomea ualimu, bali pia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300.”

Mkuu wa chuo hicho, Doroth Mhaiki anaishukuru Serikali kuamaua kujenga na kukarabati miundombinu ya chuo hicho kilichogeuzwa rasmi na serikali kuwa chuo cha ualimu mwaka 1975 na kwamba ukarabati huo ulianza mwaka 2016.

Anafafanua kuwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya chuo hicho uligawanyika katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ya utekelezaji wake iligharimu jumla ya Sh 5,789,841,143 wakati sehemu ya pili iligharimu Sh 3,814,349,468.

Anasema sehemu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa mabweni mawili ya ghorofa moja yenye uwezo wa kubeba wanachuo 314 yaliyogharimu Sh 2,092,854,800, nyumba tatu za watumishi za ghorofa moja zenye uwezo wa kuishi familia nne kila moja kwa thamani ya Sh 1,611,264,900 Aidha anasema ujenzi huo umehusisha pia nyumba moja inayojitegemea yenye thamani ya Sh 6,059,700 na ukarabati wa nyumba nne kwa gharama ya Sh 169,974,008.

Aidha, Mhaiki anasema kuwa jumla ya Sh 388,006,054 na Sh 371,168,921 zimetumika kwa kazi za nje na dharura.

Mkuu huyo wa chuo anaendelea kufafanua kuwa awamu ya pili ya ujenzi na ukarabati wa chuo hicho ilihusisha ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa moja yenye madarasa manne kila moja kwa thamani ya Sh 2,092,854,800 na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanachuo 294 kwa wakati mmoja kwa thamani ya Sh 1,611,264,900.

Vilevile anasema ujenzi huo ulihusisha maktaba yenye thamani ya Sh 307,048,000 na maabara moja ya sayansi yenye vyumba viwili, kila chumba kikiwa na uwezo wa kubeba wanachuo 40 kwa thamani Sh 298,127,275.

Kingine kilichojengwa ni ukumbi wa mikutano wenye thamani ya Sh 232,716,667 wenye uwezo wa kubeba wanachuo 240, vyoo vya madarasa vilivyogharimu Sh 140,274,169, ukarabati wa jengo la bafu na choo cha wasichana kwa gharama ya Sh 55,729,300 na kazi za nje Sh 107,860,300.

Anasema kwamba mabweni pia yamewekewa vitanda vipya, makabati na viti. “Awali chumba kimoja walikuwa wakilala wanachuo 22 ambapo kwa sasa wanalala wanachuo wanne tu,” anasema.

Kutokana na hatua hiyo, mkuu huyo wa chuo anasema, chuo sasa kina hadhi inayokistahili tofauti na awali ambapo chuo hakukuwa na maabara, maktaba, ukumbi wa mikutano.

“Mradi umekuwa na tija kubwa kwa wanachuo na walimu pia kwa kuongeza morali ya kusoma na ufundishaji,” anasema mkuu huyo wa chuo na kuongeza kuwa serikali imeitikia kilio cha muda mrefu kuhusu ukarabati wa vyuo vya walimu nchini.

“Sina budi, kwa niaba ya uongozi wa chuo, kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli kwa kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni ya za uchaguzi 2015,” anasema Doroth Mhaiki.

WILAYA ya Tunduru iliyopo mkoani Ruvuma imebarikiwa kuwa na utajiri ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi