loader
Picha

Kwa kasi hii, Tanzania itawika kimichezo Afrika, duniani

SEKTA ya sanaa na burudani imekuwa kinara katika uchangiaji wa mapato nchini, imeelezwa hivi karibuni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anasema Dodoma katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo alibainisha kuwa sekta hiyo imekuwa kinara baada ya kukua kwa asilimia 13.7.

Hali hiyo ni tofauti kabisa na ilivyozoeleka kwenye taarifa za ukuaji uchumi, kwani sekta zilizokuwa zikiongoza huku nyuma ni ujenzi, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo na habari na mawasiliano, wakati sanaa na burudani zikiwa chini.

Akiwasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya wizara yake, Dk Mpango anasema kuwa sekta ya sanaa na burudani zimeongoza kwa ukuaji zaidi ya sekta zingine, ambazo ni ujenzi (asilimia 12.9), uchukuzi na uhifadhi wa mizigo (asilimia 11.8), huku habari na mawasiliano ikikua kwa asilimia 9.1.

RIPOTI YA WATAALAMU Mwaka jana, ripoti ya wataalamu iliyotolewa na Kampuni ya PriceWaterHouseCoopers, ilionesha kuwa sekta ya sanaa na burudani, imeanza kuchangia mapato makubwa kwenye uchumi wa nchi.

Ilieleza kuwa sekta hiyo ilianza kuchangia karibu dola za Marekani milioni 496 (sawa na sh trilioni 1.1) kwa mwaka 2017, ambazo sawa na ongezeko la asilimia 28.2 ya kiasi ambacho kilipatikana kutokana na shughuli za habari na burudani mwaka 2016.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kiasi cha mapato yaliyotajwa kuchangia kutokana na shughuli za habari na burudani ni matumizi ya intaneti, televisheni, sinema, michezo ya video, uchapishaji wa magazeti na majarida, uchapishaji wa vitabu, muziki na radio.

Ripoti hiyo inakadiria kuwa sekta hizo mbili zitakuwa na wastani wa asilimia 18.3 kwa mwaka na mapato kufikia dola za Marekani bilioni 1.2 ifikapo mwaka 2022, kiasi ambacho ni mara 2.3 zaidi ya kile kilichopatikana mwaka 2017.

NA MICHEZO NAYO Sanaa na Burudani haikuwa pekee yake katika wizara hiyo ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hivyo michezo nayo inatarajia kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na shughuli mbalimbali.

Baadhi ya shughuli za michezo, ambazo nazo zinatarajia kuingiza kiasi kikubwa cha fedha ni pamoja na mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo ya soka ya kitaifa pamoja na kimataifa yatakayofanyika kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini.

Pia usajili wa wachezaji katika kipindi hiki, ambapo wachezaji wanaotoka nje fedha zao za usajili pamoja na mishahara yao ya ile ya wachezaji wazawa, itakatwa kodi na kuliingizia taifa fedha nyingi.

Kwa miaka takribani 40 hivi sawa na miongoni minne, Sekta ya Michezo nchini japo imekuwa chanzo cha ajira, lakini haijatoa mchango mkubwa katika pato la taifa, na hiyo ni kutokana na timu za taifa na klabu kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa.

Mwaka huu, ni mwaka wa michezo na hasa soka nchini. Michezo nchini imekuwa kama nyota inayowaka, kwani nchi imepata mafanikio makubwa kutokana na nchi kupata bahati kushiriki katika mashindano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2019, nchini Misri na Tanzania kuandaa mashindano ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17, U-17.

Hivyo, kutokana na nyota hiyo kuwaka, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, chini ya Waziri Dk Harrison Mwakyembe, Naibu wake, Juliana Shonza na wakurugenzi wa sekta mbalimbali katika wizara hasa sekta ya michezo wameweka mkakati kuhakikisha taifa linapata pato zaidi kupitia michezo.

Mkakati wa wizara, unaanzia katika bajeti ya wizara ya mwaka 2019/20, ambapo imeweka mkakati kuhakikisha Tanzania inang’ara, inapaa na inasonga mbele kimichezo Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa ujumla.

BAJETI YA MWAKA HUU Katika bajeti ya mwaka huu, ambapo Bunge limepitisha Sh 30,879,483,000 kwa ajili ya shughuli na maendeleo ya wizara, kiasi kingine kitatumika katika kuinua michezo ili Tanzania iwe kinara kama ilivyo katika uchumi ambao unakua kwa asilimia saba.

Waziri Dk Mwakyembe wakati anasoma bajeti anasema wizara hiyo imejipanga kimkakati kuhakikisha michezo inaleta pato kubwa la taifa kwa kuhusisha kwanza, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995.

Sera hiyo haiendani na kasi ya ulimwengu wa michezo na soka wa sasa. Anasema mkakati mwingine umelenga kuweka mkazo katika vyama vya Michezo na Mashirikisho yote nchini ambayo ni wadau wa michezo na hasa soka nchini, kuhakikisha yanasimamia wana michezo na kutoa elimu ya kinga na afya ili kulinda afya zao.

Upande wa pili, Mwakyembe amebaini kwamba Kamati za Michezo za Mikoa na Wilaya haziendani na kasi ya wizara, hivyo ameagiza Kamati za Michezo za Mikoa na Wilaya kuongeza kasi katika kukuza na kuendeleza michezo nchini.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) halijafanya vya kutosha kuhusu kutafuta mawakala wa wachezaji, Mwakyembe anaona ili kufikia mafanikio katika sekta ya michezo, BMT lazima itengeneze kanuni za namna ya kufanya uwakala kwa wachezaji wa Tanzania.

“Nawaagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutengeneza Kanuni zitakazosaidia uendeshaji wa Uwakala wa Wanamichezo hapa nchini ili kusaidia wanamichezo kuendeleza vipaji vyao na kujitangaza kimataifa,” anasema Mwakyembe.

Sekta ya michezo kupitia taasisi zake, inatakiwa kuona fahari na kujipanga kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri hasa baada ya Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Barani Afrika nchini Misri, Juni, 2019 baada ya kushindwa kufuzu kwa miaka 39.

Waziri Mwakyembe alikuwa bega kwa bega pia na Katibu Mkuu Susan Mlawi kufanya maandalizi pamoja na kukagua viwanja vya Gymkhana, JMK Park, Azam Complex, Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru kujiridhisha na hatua za ukarabati zilizofikiwa kabla ya Afcom ya U-17 iliyofanyika nchini mwaka huu.

Mkakati huo wa Afcon 2019 ulisimamiwa kwa karibu na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya fainali hizo Leodegar Tenga, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kufanya maandalizi kabla ya mashindano hayo kufanyika Aprili 14 – 28, 2019 ambapo timu ya Serengeti Boys haikufanya vizuri.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao anasema hata fursa ya ujio wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), Gianni Infantino kuja nchini, kumechangia kuitangaza nchi na michezo kwa ujumla wake.

Si soka la wanaume tu linaloipaisha Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kukutana na Waziri wa Habari, Dk Mwakyembe na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia kupata taarifa ya maendeleo ya timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kunaleta hamasa katika wizara kujipanga katika kukuza michezo nchini.

FURSA NYINGINE Waziri Mwakyembe anaona fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu Afrika Mashariki (Cecaaf) na Mashindano hayo yatahusisha nchi tano wanachama, ni fursa adhimu kwa Tanzania.

Lakini pia kuwa mwenyeji wa mashindano ya Mpira wa Miguu wa Walemavu ni fursa nyingine na kutangaza vivutio vya nchi kimataifa.

Katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kung’ara Bunge wameunda Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa wenye Ulemavu.

Wabunge hao ni William Ngelleja, Venance Mwamoto, Margret Sitta, Riziki Lulinda na Amina Mollel.

Wizara ya Maliasili na Utalii inaona kwamba ujio wa timu ya Sevilla FC kutoka Hispinia na kucheza na timu ya Simba, umechangia kutangaza utalii wa nchi yetu kupitia michezo na hasa mchezo wa soka.

Mbuge wa Chemba, Juma Nkamia anaomba serikali kuhakikisha fedha zinazoombwa kwa ajili ya wizara hiyo kuinua michezo nchini ipewe kwani bila kufanya hivyo ndoto za kuendelea kuinua sekta hiyo itakuwa haifikiwi kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita.

Dk Mwakyembe anawahakikishia wabunge na wananchi kwa ujumla kwa kusema wizara yake itaendelea kuinua michezo nchini kupitia sekta michezo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara na inatumia vizuri fursa ya kushiriki katika michezo ya kimataifa.

Afrika ni bara lililobarikiwa kuwa na maliasili nyingi, ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi