loader
Picha

Tukatae mikataba yenye masharti

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hayuko tayari kusaini mikataba tata yenye masharti yanayohatarisha taasisi za ulinzi na usalama kama jeshi au migodi, kwani itaiweka nchini katika hatari.

Alisema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge wakati wakichangia Hotuba ya Bajeti ya wizara yake, wakilaumu kwa kutosaini haraka mikataba ya miradi mikubwa.

Waziri Mpango alisema kuna miradi mikubwa kama ya bandari ya Bagamoyo, kiwanja cha ndege Zanzibar, Nduli na upanuzi wa Mto Msimbazi inayohusisha serikali kukopeshwa na wahisani huku ikiwa na masharti yasiyo na tija.

Alisema, kwa kuchelea kuhukumiwa baadaye kwa kusaini mikataba inayohatarisha jeshi au migodi yetu kuwekwa rehani serikali ikishindwa kulipa madeni, hayuko tayari kusaini mikataba.

Tumeguswa na kauli ya Dk Mpango na hivyo kuungana naye kusimamia maslahi ya Taifa kwa kuhakikisha mikataba yote inayoingiwa na nchi inakuwa isiyohatarisha usalama wa Taifa letu.

Tunasema hayo tukirejea nia mbaya ya baadhi ya nchi wahisani kutaka kuziingiza nchi maskini katika matatizo makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa kuzipa misaada yenye masharti. Imekuwa vizuri Dk Mpango ameamua kusema wazi kuhusu masharti yasiyo na tija kwa Taifa letu hivyo kuonesha tusivyo tayari kutawaliwa.

Wahisani wanatakiwa kujua Tanzania ni Taifa huru ambalo halihitaji kupewa au kufundishwa cha kufanya au kutofanya pale linapoomba msaada nje kwa maendeleo ya watu wake.

Wakae wakijua kuwa uombaji wa misaada ya kifedha, teknolojia au ufundi nje unapaswa kuzingatia ushirikiano wa kimataifa na misingi ya diplomasia yenye kuzingatia heshima na utu.

Kama nchi, hatutakuwa tayari kulazimishwa kuingia mikataba yenye masharti yasiyoenda na utu wa watu wetu, tamaduni zetu au kuhatarisha uhuru wetu, uwezo wake wa kujiendesha n.k. Kutaka kulazimisha kwa njia yoyote serikali kuingia mikataba yenye masharti tata siyo tu kunatia shaka kuhusu malengo yaliyojificha ya wahisani wa aina hiyo bali ni kutumia misaada hiyo kama fimbo kurudisha ukoloni tulioukataa.

Ni kwa msingi huo, tunasema tunamuunga mkono Dk Mpango katika msimamo wake huo thabiti na kuomba wabunge, mawaziri, viongozi wote wa serikali na wananchi kuunga mkono.

Wamuunge mkono wakijua hatoi msimamo huo kwa maslahi yake binafsi bali ya Taifa letu lote.

Asiyetaka kumuunga mkono ahesabiwe msaliti. Hatupendi kuamini Tanzania tunayoijenga sasa chini ya Rais John Magufuli itaendelezwa na watu wanaosaliti Taifa lao bali wapenda nchi yao.

KITUO cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinajitahidi sana kuboresha shughuli za ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi