loader
Picha

Wataturu wanavyoamini mkojo wa ng’ombe kukinga maradhi

WATATURU ni moja ya makabila wilayani Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga. Baadhi ya watu katika kabila hili, wanaaminika kutumia mkojo wa ng’ombe kama kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kwa watoto wadogo.

Watu wa kabila (siyo wote), wanaamini mkojo wa ng’ombe ni kinga kwa kuwa mnyama huyo anakula aina nyingi za majani. Hata hivyo wanakiri kuwa, hawana uhakika wa kitabibu kama kweli ni kinga ingawa wanadai wanaamini umekuwa ukiwasaidia.

Mkazi wa kijiji cha Magalata, kitongoji cha Mabambasi, Seda Magena, anakiri wamekuwa wakiwapa watoto mkojo wa ng’ombe kama chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali, ikiwamo malaria.

Anasema wakitaka kuwapa watoto mkojo huo, humvizia ng’ombe akikojoa na kuukinga kwa bakuli au kikombe na ukiwa wa moto moto humpa mtoto. Magena anasema mtoto akishakunywa baadaye atatapika na kuharisha.

Dalili hizo ndizo zinazowapa imani kuwa mkojo huo wa ng’ombe umefanya kazi mwilini mwa mtoto. “Mkojo wa ng’ombe unaondoa minyoo kwa watoto, kuumwa tumbo na magonjwa mengine ambayo yanawanyemelea watoto mara kwa mara na tumekuwa tukifanya hivyo kwa watoto wetu wote hakuna madhara wanayopata ya kuugua mara kwa mara,” anasema Magena.

“Watoto huwa pia tunawapaka mwilini mafuta ya ng’ombe (samli) kukinga ngozi yao na baada ya miezi miwili tunawaanzishia chakula kama vile uji mwepesi uliowekewa maziwa hatujawahi kuhudhuria hospitali hata siku moja iwe kliniki kupima uzito au kupata chanjo zinazotolewa na serikali chanjo yetu ni mkojo wa ng’ombe,” anasema Magena ambaye ni mkunga wa jadi.

Utamaduni huo wa kunywa mkojo wa ng’ombe unaungwa mkono na mkazi mwingine wa kijiji hicho, Bulalu Ndashi. Anasema wamekuwa wakipewa mkojo huo tangu wakiwa wadogo ili wasipate maradhi mbalimbali ndio maana wameendelea kuwapa watoto wao mpaka leo.

Salome Sizya, mkazi wa kijiji hicho lakini si Mtaturu, anasema ameishi na watu wa kabila hilo kwa muda mrefu na ni kweli baadhi yao huwapa watoto mkojo wa ng’ombe lakini baadhi walioelimika huwapeleka watoto hospitali kwa chanjo na tiba wanapoumwa.

“Ipo kazi ya kufanya kutoa elimu kwa watu wa kabila hili maana wachache ndio wameelimika wanakwenda hospitali na wanajichanganya na jamii nyingine, lakini wengine wamekuwa wakijitenga hawana muda wa kusikiliza jamii nyingine inafanya nini ndio maana wanaendeleza zaidi dawa za kimila,” anasema Sizya.

Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Alphonce Bagambyaka, anasema kuwa ng’ombe hutoa uchafu mwilini kama viumbe hai vingine, hivyo kama wanawapa watoto mkojo wa ng’ombe, wanawapa uchafu na wanapaswa kuacha.

“Kitaalamu ng’ombe ana ammonia nyingi kuliko binadamu sababu hali vyakula vyenye wanga, sifahamu kama mkojo wa ng’ombe kwa binadamu una madhara gani au hauna mpaka watafiti wabaini,” Bagambyaka.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Suzan Monanka, anasema kuwa jamii ya kabila la Wataturu ni wachache wanaohudhuria hospitali na ikitokea ameletwa hospitalini, huwa katika hali mbaya na wengi hufariki.

Mratibu wa Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Suzan Kulindwa, anasema kuwa wakazi wengi wa kata ya Magalata, ni Wataturu na elimu imeanza kuleta mabadiliko hasa kutokana na kuwa na zahanati. Anasema mwaka 2017 wajawazito waliohudhuria kliniki ni 285 na mwaka jana (2018) walihudhuria 293 ikiwa ni ongezeko la wajawazito wanane.

Kulindwa anasema mwaka 2017 waliojifungulia katika zahanati ni 200 na mwaka 2018 walikuwa 186. Anasema wajawazito wawili waliripotiwa kujifungulia nyumbani mwaka 2017 na hakukuwa na taarifa ya aliyejifungulia nyumbani mwaka jana (2018).

Kwa mujibu wa Kulindwa, watoto waliopata chanjo ya vitamin A kwa watoto wenye umri wa miezi sita mwaka 2017 ni 129 na mwaka 2018 ni 80. Kwa watoto wa mwaka mmoja kwa 2017 ni 161 na mwaka 2018 ni watoto 160. Anaeleza kuwa kwa upande wa matone ya vitamini A kwa watoto wanaoanzia miezi 12 hadi miaka mitano kwa mwaka 2017 walipewa watoto 442 na mwaka 2018 walipewa 2051 na wote hupatiwa vidonge vya kukinga minyoo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Marwa Ngutunyi, anasema kuwa makuzi ya mtoto yanahitaji afya iliyo bora isiyo na maradhi. Anasema mtoto asipopatiwa kinga ugonjwa huwa sugu zaidi na kuhatarisha maisha ya mtoto. Akizungumzia afya ya mtoto hasa utamaduni wa Wataturu wa kuwapa watoto mkojo wa ng’ombe, Dk Ngutunyi anasema mtoto anapoharisha kwa muda mrefu ni hatari sana kwa afya.

Anasema ipo haja kwa jamii hiyo kubadilika na kuacha kuwapatia watoto vitu vichafu au ambavyo havijaandaliwa kwa usafi au kuthibitishwa na mamlaka husika za afya. Anasema mtoto asipopata chanjo na matibabu yanayofaa na kwa wakati, tatizo alilonalo linakimbilia kwenye uti wa mgongo au damu. Dk Ngutunyi anasema chanjo ya rota imeweza kusaidia kupunguza magonjwa ya kuhara kwa watoto ingawa bado wanakuja baadhi ya watoto wakiwa kwenye hali ya ugonjwa wa kuharisha na nimonia au homa ya matumbo.

Wataalamu kutoka taasisi ya Children in Crossfire, Davis Gisuka, Msanifu wa Malezi na Makuzi ya Watoto na Frank Samson, Mratibu wa Programu ya Makuzi na Malezi ya Maendeleo ya Watoto (ECD), kwa nyakati tofauti wanasema kuwa mtoto anatakiwa kuwa na afya njema aweze kukua vizuri. Samson anasema kitaalamu ubongo kwa mtoto huanza kujijenga kupata akili ya ufahamu kuanzia siku 0 hadi 1000 yaani mimba hadi miaka miwili ubongo wa mtoto unaweza kufanya kazi kwa asilimia 92 kama akiwa hana maradhi yanayomsumbua.

Mratibu wa shughuli za lishe mkoani Shinyanga, Denis Madeleka, anasema matone ya vitamini A kwa watoto yanasaidia kupunguza udumavu na kuwa na uwezo mkubwa wa kuona Aidha anasema dawa za minyoo wanakazopewa huenda kuua aina mbalimbali za minyoo na kumwezesha mtoto kukua vizuri akiwa na afya njema na kuujenga mwili wake vizuri na ni lazima mtoto azipate.

Madeleka anasema chanjo hutolewa mara mbili kwa mwaka kwa watoto wa miezi sita hadi miezi 59. Anasema faida mojawapo ya vitamin A ni kukinga mwili dhidi ya maradhi na kumfanya mtoto akue vizuri.

Anasema, hupunguza hatari ya mtoto kupata surua kwa asilimia 33. Aidha Madeleka anasema upataji wa chanjo hizo unapunguza mfumo wa hewa unaosababisha mtoto kupata nimonia na kuhara. Mratibu wa chanjo Mkoa wa Shinyanga, Timothy Sosoma, anasema hawajawahi kusikia kuwa Wataturu wanawapa watoto mkojo wa ng’ombe kama chanjo na kuahidi kulifuatilia suala hilo na kulifanyia kazi.

Anasema wamewahi kupeleka elimu ya chanjo katika kijiji hicho na ilipokewa vizuri ingawa baadhi ya watu walijificha na hawakuwa tayari kupokea wala kwenda hospitali na kueleza kuwa inawezekana ndio hao wanaoendeleza utamaduni huo mbaya wa kuwanywesha watoto mkojo wa ng’ombe.

Sosoma anasema kinachotakiwa zaidi kwa baadhi ya Wataturu wenye tabia hiyo ni elimu zaidi kuhusu umuhimu wa kupata chanjo zilizothibitishwa kitaalamu kwani mkojo wa ng’ombe haufai kwa kuwa haujathibitishwa na ni hatari.

Anasema chanjo ya rota inayomkinga mtoto kwa magonjwa ya kuharisha hupunguza magonjwa kwa asilimia 60. Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 inaeleza wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba watoto wanapelekwa kwenye chanjo, wanapatiwa huduma za afya na kupewa miongozo na matunzo.

Sheria hiyo pia inasema jamii inapaswa kuwa bega kwa bega kufanikisha wajibu huu kwa kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kuchukua hatua pale ambapo watoto wanaonekana kunyimwa haki zao ikiwa ni pamoja na kupewa tiba zisizothibitishwa kitaalamu kuhusu ubora na usalama wake.

Afrika ni bara lililobarikiwa kuwa na maliasili nyingi, ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi