loader
Picha

Nishati mbadala inavyoendeleza utalii Pori la Akiba Selous

TAKRIBANI kilomita 30 kutoka Wilaya ya Liwale, kuna Pori la Akiba la Selous lenye upepo mwanana unaochangamsha matawi ya miti yanayoungana na ndege kutoa sauti ya kuvutia.

Utajiri wa mbuga hii kubwa barani Afrika, ndio chanzo cha mapato ya kigeni kwani wawindaji kutoka sehemu mbalimbali duniani huomba vibali kwa ajili ya uwindaji wa kitalii. Hata hivyo, uendelevu wa mapato kutoka Selous unategemea zaidi ushiriki wa jamii iliyozunguka maeneo hayo pamoja na teknolojia ya nishati salama ili kulifanya eneo hilo kuendelea kuwa asili.

Hii inamaanisha hasa utunzaji mazingira. Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Wanyamapori imeandaa “Mwongozo wa kutenga na kuendesha Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori nchini Tanzania.” Mwongozo huu ndio uliotoa mwanya kwa vijiji vinane vinavyozunguka Pori la Akiba la Selous katika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi kuungana na kutengeneza Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Maendeleo Endelevu ya Mangingo.

Kupitia mpango shirikishi wa uhifadhi, vijiji vya Ndapata, Mlembwe, Mpigamiti, Barikiwa, Chimbuko, Kimambi, Ilambo na Mimwi katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi vimeweza kuanzisha jumuiya inayotambulika kisheria ambayo inamiliki na kuendesha vitalu vitano katika pori hilo.

Ndani ya eneo la wanyama wakali, kuna jengo lililojengwa kitamaduni na kuna huduma zinazohitaji umeme ikiwemo vinywaji baridi, maji ya moto na hata majiko. Japokuwa hakuna nyaya za umeme zilizopita katikati ya pori hilo, lakini mhifadhi ambaye pia ni mwakilishi wa Jumuiya ya Mangingo, Mapambano Ngayunga anasema eneo hilo ndipo wawindaji wanapopumzika.

Juu ya paa la kibanda hicho kinachotumiwa na wawindaji kupumzika na kupata viburudisho, kuna miundombinu ya umeme utokanao na mionzi ya jua (sola). Kibanda cha pili kina paneli (moduli) zilizowekwa sawa kuwezesha ukusanyaji wa mionzi hiyo na kuibadili kuwa katika hali ya umeme ili kuendeshea miradi unayohusiana na uhifadhi na uwindaji.

Ngayunga anapoulizwa juu ya sababu za kuamua kutumia umeme huo wa sola hususani katika eneo hilo badala ya umeme wa kutoka gridi ya taifa, hasa ikizingatiwa kuwa Liwale imeunganishwa na gridi hiyo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) anasema: “Tunataka sekta ya utalii iwe endelevu.”

Anasema uamuzi wa kutumia umeme huo katika miradi ya Mangingo ambayo ni uhifadhi na uwindaji endelevu umelenga kuvifanya vitalu walivyokabidhiwa vya Hokororo, Nachingo, Kimila, Naimba na Namawe kutopoteza uhalisia wake ikiwa na kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu. “Tukiweka nguzo za umeme wa kawaida hapa, ina maana tutakata miti kwa wingi tutachimba ardhi ili kupata mashimo ya kusimika nguzo.

Yote hiyo ni kuharibu uhalisia wa hifadhi na kuhatarisha makazi ya wanyama,” anasema mhifadhi huyo wa Jumuiya ya Mangingo. Anaeleza kuwa, uhifadhi umekuwa na changamoto hasa katika kipindi hiki ambapo watu wanatafuta maeneo ya kilimo huku mabadiliko yakiwa yanaathiri sekta ya utalii. Hii ndiyo maana jumuiya hiyo, kwa mujibu wa Ngayunga, imejikita katika teknolojia itakayosaidia sekta sekta ya utalii kuwa endelevu.

Matumizi ya umeme wa sola katika Pori la Akiba Selous Watalii wa uwindaji wanahitaji kupumzika baada ya kusaka wanyama mbugani kwa mujibu wa vibali vyao. Ngayunga anasema ili kukidhi mahitaji ya wateja katika vitalu vyao likiwemo suala la kupata vinywaji, malazi na mahitaji mengine ya kibinadamu, chanzo cha nishati inayotumika katika eneo hilo ni jua.

“Tunatumia umeme wa jua kwa ajili ya kuchemsha maji ya kuogea, majokofu kuhifadhia vinywaji na bidhaa nyingine ambazo zinaharibika haraka,” anasema mhifadhi huyo. Kutokana na ufanisi wa katika teknolojia hiyo ya umeme jua, Jumuiya ya Mangingo imefanikiwa kuvutia watalii katika vitalu ilivyokabidhiwa. Kwa mujibu wa Ngayunga, hadi kufikia Julai, mwaka jana, jumuiya hiyo ilikuwa imepata kupata Sh milioni 20.

“Fedha hizo tulizigawanya kwa kila kijiji ambacho ni mwanachama wa jumuiya na zimetumika katika ujenzi wa vyoo vya shule na huduma za maji,” anasema mwakilishi wa jumuiya hiyo ya Mangingo. Kaimu Meneja wa Pori la Akiba la Selous Kanda ya Kusini Mashariki (Liwale), Adam Mboto, anasema kupitia sera ya uwajibikaji katika jamii, waliamua kuwashirikisha wanavijiji kupitia jumuiya zao ili kusaidia uhifadhi huku vijiji navyo vikinufaika kupitia programu hiyo kama ilivyo Mangingo kwa sasa.

Matumizi ya umeme wa sola yameonekana kuwa njia mbadala katika utalii endelevu huku ripoti ya ‘Hali ya Upatikanaji wa Nishati Tanzania Bara ya Mwaka 2016,” iliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kushirikiana na Rea ikionesha kuwa, nishati itokanayo na jua ni chanzo cha pili kinachotegemewa mkoani Lindi kuzalisha mwanga baada ya taa za kuchaji.

Ripoti hiyo ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati Tanzania Bara ambayo ilichapishwa mwaka 2017 inaonesha kuwa, asilimia 14.8 ya kaya zilizopo katika Mkoa wa Lindi inategemea nishati ya jua kama chanzo cha kuwapatia mwanga. Ripoti hii inaonesha hivyo huku Sensa na Makazi ya mwaka 2012 ikionesha kuwa Lindi ina watu 864,652.

Utafiti uliofanywa na Arif Karabuğa Kupla wa Chuo Kikuu cha Süleyman Demirel nchini Uturuki na wenzake wanne uliojikita kwenye masuala ya utalii na nishati unaeleza: “Nishati mbadala ni sahihi kwa sababu haichafui mazingira wakati wa uzalishaji wake na unapunguza gharama.”

Utafiti huo uliochapishwa 2015 kwenye jarida la Sayansi, European Scientific Journal, na kupewa kichwa cha habari: “Nishati Jadidifu Suluhisho la Utalii,” umeeleza kuwa nishati mbadala kama umeme jua, joto ardhi, upepo na nyinginezo zinaweza kutumika hotelini na kuokoa gharama nyingi huku ikisaidia uhifadhi wa mazingira. Maendeleo Endelevu (SDG) Na. 7 Kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), kutoka mwaka 2000 hadi 2016, uwiano wa idadi ya watu walioweza kutumia nishati uliongezeka kutoka asilimia 78 hadi asilimia 87.

Idadi ya watu ambao hawawezi kupata huduma hiyo ilishuka hadi chini ya bilioni 1. Pamoja na maendeleo hayo katika sekta ya nishati, takwimu za mwaka 2016 za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonesha watu bilioni 3, sawa ma asilimia 41 ya idadi yote ya watu duniani, bado wanatumia nishati zisizo salama kwa ajili ya kupikia. SDG 7 inahusisha suala la nishati na maendeleo ya kiuchumi.

“Ongezeko la matumizi ya nishati ya mafuta pasipo hatua madhubuti za kukabiliana na ongezeko la gesi chafu lina madhara na mabadiliko ya tabianchi. Lindi na matumizi ya umeme wa sola Pamoja na Mpango wa Serikali kusambaza umeme kupitia Rea kwa kasi mkoani Lindi, bado nishati itokanayo na jua inaonekana kuwa ndiyo rahisi zaidi hasa kwa matumizi ya umma.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, barabara za miji na mikoa zitafungwa taa zitumiazo nishati ya jua ili kuimarisha usalama wa mijini na kupendezesha mandhari. Zambi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Lindi, anasema kuwa kwa uzoefu, taa zitumiazo umeme wa sola zilizofungwa katika baadhi ya mitaa mjini Lindi, zimesababisha kuongezeka kwa usalama huku wafanyabiashara wakiwa huru kufanya kazi hadi usiku.

Afrika ni bara lililobarikiwa kuwa na maliasili nyingi, ...

foto
Mwandishi: Sauli Giliard

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi