loader
Picha

Changamoto za tafsiri na namna ya kuzikabili

Tafsiri ni zoezi la uhamishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja (chanzi) kwenda lugha nyingine (lengwa). Dhamana ya tafsiri ni kuleta ulinganifu wa mawazo, ujumbe au taarifa kati ya matini chanzi na matini lengwa.

Kwa maneno mengine, ni kitendo cha kubadilisha kile kilichoelezwa katika lugha moja kwenda katika lugha nyingine kwa kutumia maneno na istlahi zinazofanana au zinakaribia kufanana na kile kinachomaanishwa katika lugha chanzi. Kwa msingi huo, unapotafsiri unapaswa kutafuta maneno katika lugha lengwa yanayofanana na yale ya lugha chanzi.

Lakini mara nyingi hakuna ulinganifu wa neno kwa neno kati ya lugha mbili. Hapo ndipo mfasiri anapokumbana na changamoto mbalimbali katika kazi hii. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na tofauti za kiutamaduni, kimuundo, kisarufi, kimsamiati, kisayansi na pia uzingatiaji wa hadhira. Kama tunavyojua, lugha ni sehemu ya utamaduni na inaeleza utamaduni wa jamii inayohusika.

Kwa mfano, maana za methali, nahau na misemo, inatofautiana katika tamaduni mbalimbali. Sifa moja muhimu ya miundo kama hiyo, ni maana ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na maana za maneno yaliyotumika kuiunda.

Kwa mfano msemo wa Kiingereza: “A storm in a tea cup”. Msemo huu hauna maana ya moja kwa moja na maneno yanayouunda. Na unapojaribu kutafsiri neno kwa neno kamwe hutapata maana iliyokusudiwa. Mfano, kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili kuwa ni “Dhoruba ndani ya kikombe cha chai” haileti maana iliyokusudiwa. Maana halisi ya msemo huo ni “Kuwa na wasiwasi mkubwa kwa jambo dogo”.

Tuangalie mifano michache ya methali na misemo;

Mfano: Methali na nahau: After a storm comes calm – Baada ya dhiki faraja – na sio baada ya dhoruba unakuja utulivu. Penny wise pound foolish – mwangalifu wa mambo madogo na kutojali makubwa – na wala sio busara wa sarafu mjinga wa pauni. Rule with rod iron – Kutawala kwa mabavu na sio Kutawala wa kiboko cha chuma. Katika suala hilohilo la utamaduni, mfasiri anapata changamoto nyingine linapokuja suala la kutafsiri matini zenye mambo ya kiutamaduni.

Kwa mfano katika Kiswahili, kuna majina ya undugu kama vile baba mdogo au baba mkubwa au mjomba, ambao wote hao katika Kiingereza ni “uncle”/. Vivyo hivyo, shangazi/mama mdogo au mama mkubwa katika Kiingereza ni ‘aunt’, mpwa katika Kiswahili linatumika kwa mwanamke na mwanamume, lakini sivyo hivyo katika Kiingereza ambapo maneno yanayotumika ni ‘niece’ kwa mpwa wa kike na ‘nephew’ kwa mpwa wa kiume.

Pia, tafsiri inaweza kuathiriwa na uzingatiaji wa hadhira, yaani, wasikilizaji na wasomaji ni akina nani kwa kuzingatia elimu yao, umri, makundi ya kijamii, itikadi n.k. Je, wameelimika au hawana elimu? Uzingativu huo unaweza kumpa changamoto mfasiri katika uchaguzi wake wa msamiati na muundo. Katika suala la sarufi, ukiangalia namna sarufi inavyohusika, hakuna lugha mbili zinazoeleza vipengele vyote vya maana katika namna inayofanana, kwa mfano muda, namba, jinsi n.k.

Mfano: The student is very tall. She is in form four. Mwanafunzi ni mraefu sana. Yuko kidato cha nne.

Sentensi ya Kiingereza inaonesha kwamba mwanafunzi ni msichana; lakini ya Kiswahili haionyeshi hivyo, kwa sababu lugha haina kielelezo cha jinsi. Katika Kiingereza kibainishi “the” kinatumika wakati katika Kiswahili hakuna kibainishi.

Katika mazingira kama haya suluhisho ni kutoa maelezo ili kutaja ni mwanafunzi yupi anayezungumziwa. Kutokana na changamoto zote zilizotajwa hapo awali, wataalamu wameeleza mbinu mbalimbali zinazoweza kumsaidia mfasiri kukabiliana nazo ili kupata tafsiri nzuri isiyopotosha maana iliyomo katika lugha chanzi.

Swali la kujiuliza ni kwamba, ni jinsi gani mfasiri anatatua matatizo ambayo yameibuka wakati wa mchakato wa kutafsiri? Yaani, ni mbinu gani amezichagua? Ili kufanya hivyo tunahitaji mbinu za tafsiri. Mbinu ni matokeo ya uchaguzi unaofanywa na mfasiri, uhalali wake utategemea maswali mbalimbali yanayohusiana na muktadha, madhumuni ya tafsiri, matarajio ya hadhira n.k.

MBINU ZA TAFSIRI

Mbinu za tafsiri kwa kawaida hutumika pale yanapotokea matatizo ya kutopata maneno yenye ulinganifu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa. Matatizo yanaweza kugawanywa katika maeneo kadhaa.

Eneo la kwanza ni kwamba, mara nyingi kunakuwa hakuna ulinganifu wa maneno katika lugha lengwa yatakayotumika katika lugha chanzi. Wakati mwingine, kunaweza kuwa na maneno au maelezo yenye muundo sawa katika lugha chanzi na lugha lengwa, lakini yakawa na maana tofauti katika kila lugha na hasa katika misemo, nahau, methali n.k.

Zipo mbinu mbalimbali zinazotumika katika kukabiliana na matatizo ya kutafsiri dhana ngumu katika lugha chanzi na hasa dhana za kiutamaduni zinazotofautiana kutoka lugha moja hadi nyingine. Baadhi ya mbinu hizo ni:- Ubadilishaji au uhamishaji Mbinu hii ni ya uhamishaji wa neno kutoka lugha chanzi kwenda katika matini ya lugha lengwa kama sehemu ya tafsiri. Katika mbinu hii, mfasiri anachukua maelezo au neno la kutoka katika lugha ya asili (lugha chanzi) kama lilivyo bila ya kulitafsiri.

Kwa mfano, baadhi ya majina ya nchi isipokuwa kama yana tafsiri inayotambulika, majina ya mitaa, magazeti n.k. Kwa mfano, Zambia, Zimbabwe, Tanzania n.k Kutohoa Hii ni mbinu ya kubadilisha matamshi au tahajia ya neno katika lugha chanzi ili yalingane na matamshi au tahajia ya lugha lengwa, au kulipa neno muundo wa kifonetiki wa lugha lengwa.

Mfano:

Kiingereza Kiswahili

eucaliptus - mkaratusi

jacaranda - mjakaranda

Kangaroo - Kangaruu

Internet - Intaneti

Kuazima neno Kuazima ni kuchukua neno moja kwa moja kama lilivyo kutoka katika lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila ya kulitafsiri. Mbinu hii hutumika pale ambapo hakuna kabisa neno lenye ulinganifu au dhana yake katika lugha lengwa. Mbinu hii siyo nzuri sana kwani itawanyima wasomaji wa lugha lengwa kufahamu maana ya neno lililotumika bila ya kutafsiriwa.

Kutoa maelezo ya neno Mbinu hii inatumika pale ambapo mfasiri anakutana na neno ambalo halina ulinganifu katika lugha lengwa, hivyo analazimika kutoa maelezo ya neno hilo ili lieleweke katika lugha lengwa. Mfano: Pediatrician – daktari bingwa wa magonjwa ya watoto. Gynecologist – daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama. Surgeon– Daktari bingwa wa upasuaji.

Tafsiri ya kutumia kifungu cha maneno Katika mbinu hii inatolewa tafsiri kwa kuzingatia shughuli inayofanyika. Mara nyingi mbinu hii inatumika wakati hakuna neno linalolingana kati ya lugha chanzi na lugha lengwa. Baadhi ya wataalamu wanasema mbinu hii ni mbinu sahihi zaidi ya kutafsiri yaani, kulifanya neno kuwa la kiutamaduni

Mfano:

Carpenter – fundi seremala

Plumber – fundi bomba.

Artisan – Fundi mchundo Kurekebisha / ulinganifu

Urekebishaji unatokea wakati kitu maalumu katika utamaduni wa lugha moja kinaelezwa katika namna tofauti kabisa inayojulikana au inayofaa katika utamaduni wa lugha nyingine. Mbinu hii inatumika zaidi katika methali, misemo n.k. Htumika pia kwa mazingira yanayofanana kwa kutumia msemo/fungu la maneno lililo tofauti kabisa; mfano tafsiri ya methali, misemo au nahau.

Mfano:

(i) After a storm comes calm – Baada ya dhiki faraja.

(ii) A storm in a tea cup – Wasiwasi mkubwa kwa jambo dogo.

(iii) Make hay while the sun shines – Samaki mkunje angali mbichi.

(iv) No need to cry over split milk – Maji yakimwagika hayazoleki.

Kuliondoa neno Hii ni mbinu ambayo maneno yasiyotafsirika au yasiyo na ulinganifu katika lugha lengwa yanaachwa, na yale yenye ulinganifu tu ndiyo yanayotafsiriwa. Mbinu hii siyo nzuri kwa sababu kuacha neno kunaweza kusababisha upotoshaji wa maana, isipokuwa kama neno lililoachwa siyo muhimu kwa kuzingatia ujumbe unaotolewa.

Katika mbinu hii, mfasiri anapaswa kuwa makini kwa sababu kuliondoa neno kunawanyima wasomaji haki ya kupata ujumbe kamili kutoka katika lugha chanzi.

HITIMISHO

Uchaguzi wa mbinu unapaswa kufanywa kwa uangalifu ili kuendana na malengo ya kutafsiri matini maalumu. Katika kutafsiri mfasiri anaweza kutumia mbinu zaidi ya moja. Kama mtu anataka kuwa mwaminifu kwa wasomaji wa lugha chanzi na lugha lengwa, uchaguzi mzuri utakuwa ni ule unaohakikisha kwamba mbinu zinazotumika zitawezesha mawasiliano na kutoa picha halisi ya kile kilichoelezwa katika lugha chanzi.

Mwandishi wa Makala hii anatoka Idara ya Tafsiri na Ukalimani - Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).

Afrika ni bara lililobarikiwa kuwa na maliasili nyingi, ...

foto
Mwandishi: Vidah Mutasa

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi