loader
Picha

Mtwara wamkera Jafo

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Mtwara kukaa chini na kutafakari namna wanavyosimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa vituo vya afya mkoani humo.

Alitoa agizo hilo mjini hapa jana baada ya kutembelea ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mtimbwilimbwi kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani hapa kwa lengo la kujionea namna ambavyo ujenzi huo unaendelea.

Alisema, miradi mingi ya afya inayotekelezwa mkoani humo haiendi vizuri ikilinganishwa na miradi inayotekelezwa katika mikoa mingine nchini.

“Tatizo ninaloliona hapa, ni usimamizi wa viongozi na hapa sijafika Masasi inawezekana tatizo likawa ni hili hili. Nimekwenda pale Nanguruwe hali ni mbaya zaidi, nilitarajia kwamba nikifika Mtwara majengo yote yawe yamekamilika, lakini kasi hairidhishi kabisa,” alisema.

Waziri Jafo pia alitembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayotarajiwa kujengwa eneo la Nanguruwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ambapo alikuta ujenzi wake haujaanza na kuagiza kuwa hadi kufikia Juni 10, mwaka huu, uwe umeshaanza.

Pia alitembelea ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mkunwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ambako tayari ujenzi wake umeshaanza kutekelezwa huku zaidi ya Sh milioni 200 zikiwa tayari zimeshatumika.

“Naagiza, hadi kufikia tarehe 30, mwezi huu, majengo yote yawe tayari yamekamilika na napenda niseme wazi kabisa kuwa Mtwara hamna rekodi nzuri katika utekelezaji wa miradi hii. Naagiza hadi tarehe 30, mwezi huu miradi hii iwe imekamilika.”

Kwa upande wake, mkazi wa Nanyamba, Abdurazaki Kasembe alisema kusuasua kwa Kituo cha Afya cha Nanyamba kunatokana na viongozi wa mkoa kuwa chanzo cha kukwamisha miradi hiyo kwani wamekuwa na mvutano wa wenyewe kwa wenyewe.

WANAWAKE wenye matatizo ya Fistula nchini wametakiwa kuacha kujifungia ndani ...

foto
Mwandishi: Sijawa Omary, Mtwara

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi