loader
Picha

Umuhimu wa uchumi wa viwanda Tanzania

JAPOKUWA ajenda ya kuanzisha viwanda imekuwepo tangu tulipopata uhuru, ajenda hiyo imepata umaarufu mkubwa na kupewa kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Wanazuoni wengi wanataja ujenzi wa viwanda kama suala lisilokwepeka na kwamba ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi, kuleta maendeleo endelevu na kuondoa umaskini. Historia inaonesha kwamba, nchi nyingi zilifanikiwa kuvunja mzunguko wa utegemezi na kujijengea uwezo wa kutetea maslahi yao kwa kuanzisha viwanda.

Ndiyo maana, Dira ya Tanzania ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inalenga kufanya uchumi wa Tanzania kufikia kiwango cha kati (kipato cha Dola za Marekani 3,000 (takribani Sh milioni 6 kwa kila mtu kwa mwaka) kwa kuanzisha viwanda.

Duniani kote, tafsiri pana ya viwanda inajumuisha: uchimbaji wa madini na mawe; utengenezaji wa bidhaa na huduma; uzalishaji na usambazaji wa umeme, gesi, mvuke na hewa baridi; usambazaji wa maji, usimamizi wa maji taka, taka nyingine na shughuli za kurekebisha/kuzuia uharibifu wa mazingira; na ujenzi.

Hivyo, ujenzi wa uchumi wa viwanda ni kufanya mageuzi ya kimfumo, kijamii na kiuchumi yanayotawaliwa na teknolojia na kuongeza uzalishaji yanayofanya viwanda kuchangia katika ukuaji wa uchumi zaidi ya sekta ya kilimo.

Manufaa ya viwanda kwa Watanzania Japokuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya uanzishwaji wa viwanda na maendeleo ya watu na kuondoa umaskini; uanzishwaji wa viwanda ukiratibiwa vizuri una manufaa mengi yakiwamo kutengeneza ajira kwa wananchi kwani viwanda vinapoanzishwa na kupanuka, vinakuwa na uwezo wa kuajiri watu wengi.

Mengine ni kustawi kwa shughuli za kiuchumi kama ongezeko la uzalishaji wa malighafi, usafirishaji wa bidhaa, huduma, na biashara mbalimbali zinazoongeza ajira. Hata hivyo, mchango wa viwanda katika ajira utategemea: kama viwanda hivyo vinatumia teknolojia ya mikono zaidi au mitambo kama vinaajiri watu wenye elimu ya juu au ya kawaida.

Lakini pia kama sehemu kubwa ya malighafi zinazotumika zinatoka ndani au nje ya nchi na kama viwanda vipo vijijini au mijini. Manufaa mengine ni kupanua soko la bidhaa za kilimo: Hii inatokea kwa wafanyakazi wa viwandani kutumia bidhaa za kilimo na uzalishaji viwandani kutokana na mazao ya kilimo kama malighafi na hivyo, kuimarisha na kutoa uhakika wa soko la bidhaa zinazotokana na kilimo hali inayohamasisha uzalishaji zaidi.

Ni kwa njia hiyo viwanda vinakuwa kichocheo cha mageuzi ya kimfumo ya kijamii na kiuchumi katika sekta ya kilimo. Kuwapo kwa viwanda vingi nchini, kunaongeza uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi na unapanua wigo wa upatikanaji wa bidhaa na huduma hali inayoruhusu uchaguzi katika kukidhi mahitaji. Aidha, huwezesha kuokoa fedha za kigeni zilizopo.

Mfano, tukizalisha sukari ya kutosha, hatutahitaji kutumia pesa za kigeni tulizo nazo kuagiza sukari kutoka nje ya nchi, badala yake tutatumia pesa hizo kuagiza bidhaa ambazo hatuna uwezo wa kuzizalisha nchini. Hali kadhalika, kwa kuzalisha vyetu wenyewe vinatufanya tujitegemee. Kufanikiwa kwa mpango huu kunategemea upatikanaji wa bidhaa na huduma hizo, ubora wake, bei na kama Watanzania wanapenda vya kwao au vya nje.

Aidha, ziada ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini zinaweza kuuzwa nje ya nchi ili kutupatia fedha za kigeni. Kwa nchi nyingi za Kiafrika, mauzo ya bidhaa nje yamechochea ukuaji wa uchumi. Pesa za kigeni zinazopatikana zinasaidia kununua mahitaji ya muhimu kama petroli, teknolojia, na dawa za wanyama na binadamu ambazo hatuwezi kuzalisha nchini.

Utalii ni moja ya huduma ya umuhimu tunazozalisha na kupata pesa za kigeni. Kuanzishwa na kupanuka kwa viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi, kunaiongezea serikali mapato, hivyo kuwahudumia wananchi hasa masikini kwa kuwapatia huduma muhimu kama elimu bure, maji, matibabu, umeme, barabara na nyumba. Kufanikiwa kwa mpango huu kunategemea utashi na uwezo wa wawekezaji kulipa kodi na serikali kukusanya kodi na kuzitumia kwa manufaa ya wananchi. Maadui wakubwa wa eneo hili ni rushwa na ufisadi.

Kwa bahati nzuri, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, inapambana na maadui hao kwa vitendo. Imebainika kuwa, uwepo wa viwanda nchini husaidia ukuaji wa teknolojia ya kisasa ambayo ni hitaji muhimu kwa nchi. Wawekezaji huja na teknolojia ambayo wazawa hujifunza na kuitumia katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, hivyo kuongeza tija.

Uwekezaji kutoka nje hupunguza mahitaji ya mtaji, ambayo mara nyingi unakuwa hautoshi. Mwisho, uwepo wa viwanda vingi na imara nchini, huongeza mapato kutokana na mwingiliano wa shughuli mbalimbali za kiuchumi. Viwanda vina mchango mkubwa kuchochea mwingiliano wenye tija wa sekta mbalimbali hivyo, kuongeza kipato cha sekta zote.

Viwanda vinapoanzishwa na kupanuka, vinahitaji malighafi zaidi. Ili kutimiza azma hiyo, wakulima watazalisha malighafi zaidi na hivyo kujipatia pesa zaidi. Lakini ili wakulima wazalishe zaidi wanahitaji, dawa, mbolea, mbegu bora, na zana za kilimo zinazozalishwa viwandani. Uzalishaji viwandani unapoongezeka, wafanyakazi hupata mapato makubwa na mahitaji yao ya bidhaa na huduma yataongezeka.

Wazalishaji wa bidhaa na huduma nao wataongeza uzalishaji na hivyo kipato chao kitaongezeka. Vivyo hivyo, kwa watoa huduma za usafiri, benki, bima, afya na elimu. Mwingiliano au ushirikiano huo, unanufaisha sekta hizo na uchumi kwa jumla. Hata hivyo manufaa hayo yatapatikana tu iwapo viwanda vinatumia malighafi na huduma kutoka ndani na Watanzania wanapenda kutumia kilicho chao.

Hivyo, ili kukuza uchumi, kupata maendeleo endelevu na kuondoa umasikini; ujenzi wa uchumi wa viwanda hauepukiki nchini. Watanzania waunge mkono ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza katika viwanda na kulipa kodi. Watanzania pia wapende kununua kinachozalishwa Tanzania wakizingatia kuwa katika hili wanajenga ubora unaostahiki katika uchumi endelevu. Profesa Kitojo Wetengere ni Mchumi. Aliwahi kufanya kazi katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa (Centre for Foreign Relations). Kwa sasa ni Mshauri Binafsi wa masuala ya uchumi.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu ...

foto
Mwandishi: Prof. Kitojo Wetengere

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi