loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Hivi ndivyo tunavyohudumia shehena za nafaka bandarini’

BANDARI ya Dar es Salaam na nyingine zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), zimekuwa zikipitisha shehena za aina mbalimbali kutoka nje au kusafi risha kwenda nje.

Kutegemea aina ya shehena na namna ya kuzishughulikia, shehena hizo zimewekwa katika makundi tofauti. Zipo shehena zilizo katika makasha, shehena mchanganyiko (ambazo haziko katika makasha zinazojulikana pia kama shehena kichele), shehena ya mafuta pamoja na magari.

Nafaka ni moja ya shehena kichele inayopita bandarini na katika makala haya, Kaimu Meneja Idara ya Nafaka, Tatu Moyo, anatoa maelezo namna wanavyohudumia shehena hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndiyo kubwa kuliko zote nchini.

Moyo anasema kwa kawaida idara yake ina kazi mbili kubwa; kuhudumia mzigo wa kichele kwa kuupitisha au kuuhifadhi pamoja na kuushona katika mifuko kutegemea matakwa ya mteja.

“Mzigo tunaoshona unakuwa umekuja kama kichele, lakini baadaye tunaushona kwenye viroba kwa sababu tunavyo vifaa kwa ajili hiyo,” anasema. Anasema katika mwaka huu wa fedha wa 2018/19, Bandari ya Dar es Salaam ilijiwekea malengo ya kupokea tani 2,042,900 za nafaka, lakini hadi kufikia Aprili mwaka huu tani 1,489,863 zilikuwa zimepokelewa.

Anasema katika mwaka wa fedha 2017/18 bandari ilijiwekea malengo ya kuhudumia tani 2,292,500 za nafaka lakini tani zilizohudumiwa zilikuwa 1,825,860. Katika kipindi hicho anasema, hali ya uchumi wa dunia haukuwa mzuri huku baadhi ya nchi jirani zinazopitishia mzigo wao katika Bandari ya Dar es Salaam zikikumbwa na machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kuhusu shehena inayopokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam, Moyo anasema kwa kiasi kikubwa ni ngano, mbolea na mahindi. Anasema: “Hii ngano huja kwa ajili ya matumizi ya nchi yetu pamoja na nchi za Rwanda na Burundi. Pia, tunapokea sana mbolea kwa ajili yetu Tanzania, Rwanda na Zambia.” Kuhusu taratibu za mtu kuagiza shehena ya nafaka nje, au kuisafirisha kwenda nje ya nchi, Moyo anasema mteja anaweza kuanza kwa kuziona mamlaka husika ikiwemo bandari wakamsaidia mahala pa kuanzia.

Kwa kifupi anasema, ni pamoja na mteja kuwa na vibali ya kusafirisha shehena au kutoa nje shehena na kisha kuwasiliana na mawakala wa meli. Akielezea hatua kwa hatua shughuli ya kuhudumia mzigo kichele inavyofanyika bandarini, Kaimu Meneja Idara ya Nafaka anasema kwanza, wanapata taarifa ya ujio wa meli yenye mzigo kupitia kwenye vikao vyao vya mipango ambavyo hufanyika kila siku.

Anasema baada ya hapo, wanaandaa kikao baina ya wakala wa meli anayemwakilisha mwenye meli na mteja ili kuratibu shughuli za kuhudumia meli husika. “Hapa huwa tumeshajua mzigo uko kiasi gani na hivyo kuandaa vifaa.

Meli ikishafunga gati baada ya kupata nafasi tunapeleka vifaa vinavyohusika ambavyo ni vya kuzoa nafaka kwenye meli (grabs) na vifaa vinavyowezesha kuimwaga nafaka hiyo kwenye magari (hoppers),” anasema.

Anasema magari yanapoingia bandarini tayari kupakia nafaka, kwanza hupimwa yakiwa matupu kabla ya kupakia mzigo ili kujua uzito wake na kisha yakishapakia mzigo yanapimwa tena kwenye mzani na hivyo kujulikana gari limepakia tani ngapi. Hatua hii anasema ndiyo inayowezesha tozo mbalimbali kufanyika ikiwemo kodi ya serikali.

Anasema taratibu zote zinazohusisha wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA) na tasisi zinazoangalia ubora wa vyakula zikikamilika, mzigo huruhusiwa kutoka nje ya bandari.

“Wakati mwingine, mteja anaomba mzigo wake kushonwa na hapo tunamshonea palepale kwenye gati kwa kutumia mashine zetu za kisasa. Kama mteja atataka vifurushi vya kilo tano tano, kilo kumi au zaidi tunamshonea.” “Wakati mwingine mteja anaomba mzigo wake utunzwe kwenye maghala yetu kwa kuwa hawezi kuutoa wote moja kwa moja na hivyo tunautunza kwenye maghala yetu (silos) hadi atakapokuwa tayari kuuchukua,” anasema.

Anasema mteja anatozwa gharama kidogo za kuweka mzigo kwenye silos na anapotaka kushonewa mzigo wake, hutozwa pia gharama kidogo hutegemea ukubwa wa mzigo anaotaka. Kuhusu mtu anayesafirisha nafaka nje, Moyo anasema kimsingi taratibu ni zilezile kama za kuingiza kama vile kupata vibali vya kusafirisha, kuwaona mawakala wa meli, kufuata taratibu za bandari, kupimwa kwa mzigo na kisha kumiminwa kwenye meli.

Akifafanua kuhusu ukaguaji wa mzigo, Moyo anasema, meli inapoingia bandarini na kufunga, kunakuwa na wakaguzi wa kuangalia usalama wa chakula kutoka taasisi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na nyinginezo na kwamba, taasisi hizo zikisharuhusu ndipo mzigo unapokuwa tayari kushushwa. Meneja huyo anawahakikishia wateja kwamba, kupitishia mzigo katika Bandari ya Dar es Salaam ni uamuzi sahihi kwa sababu licha ya tozo za bandari kuwa rafiki kulinganisha na bandari za nchi nyingine, mzigo unabaki salama kwa asilimia 100.

“Bandari ina ulinzi wa uhakika, kuna walinzi binadamu, mbwa na kamera za ulinzi (CCTV),” anasema. “Kwa vile tunahudumia pia majirani zetu wa Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na Kongo (DRC) ninawaomba waendelee kutumia Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ni salama kama lilivyo jina lake na tunafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, saa 24, siku saba kwa wiki. Hapa mzigo haujawahi kupotelea hapa,” anasema.

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) juzi ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi