loader
Picha

Lukuvi atoa siku tisa walipe bil 200/-

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametoa siku tisa kwa mashirika, kampuni na taasisi 207 zinazodaiwa kodi ya ardhi jumla ya Sh bilioni 200, kuhakikisha zinalipa ndani ya muda huo.

Akizungumza na watendaji wa kampuni, taasisi na mashirika yanayodaiwa kodi hiyo katika mkutano uliofanyika jijini hapa, Lukuvi alisema wanatakiwa kulipa kodi hiyo hadi Juni 20, mwaka huu, baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa zikiwemo za kufuta miliki na kupelekwa mahakamani.

“Taasisi, kampuni na mashirika yatakayochelewa kulipa hadi tarehe hiyo, siku inayofuata ya Juni 21, mwaka huu, wizara yake kwa kutumia mabaraza ya ardhi itaanza kazi ya kuwahoji waliogoma au waliopuuza kulipa kodi hiyo na kuamua kuwachukulia hatua kwenda mahakamani,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alitoa orodha ya mashirika, kampuni na taasisi zinazoongoza kwa madeni ni TTCL inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni 40, Tanesco bilioni 25, Narco bilioni 23, NBC bilioni 17 na Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) bilioni 10.

Nyingine ni Kituo cha Uwekezaji (TIC) bilioni tisa, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) bilioni nne, Kituo cha Elimu Kibaha bilioni tano, Kampuni Mery bilioni tano, Kampuni ya Rasilimali za Reli bilioni nne, Bodi ya Katani Tanzania bilioni tatu, Sido bilioni tatu, Shirika la Nyumba (NHC) bilioni tatu na Kampuni ya Saruji Mbeya bilioni tatu.

Lukuvi aliziomba taasisi, kampuni na mashirika hayo ambazo takwimu za wizara zinapishana na zake, kwenda kushauriana na wakurugenzi wa ardhi wa kanda ili kupata madeni halisi, lakini wahakikishe wanalipa madeni hayo kabla ya Juni 20, mwaka huu.

Alisema taasisi, kampuni na mashirika hayo ambayo yadaiwa, lazima wawe wamelipa madeni hayo, baada ya hapo wizara hiyo haitasita kukamata magari, kukamata viongozi, nyumba na kufunga ofisi na kushika miradi ili kuhakikisha kwamba kodi ya ardhi inalipwa.

Alisema taasisi mbali mbali ambazo zinaomba msamaha, zinatakiwa kuandika barua na kuomba msamaha huo kwa waziri baada ya kusoma tangazo GN 347 alilotoa Julai mwaka jana katika sura 113, lakini wajue wazi kwamba hawatasamehewa madeni ya nyuma.

Alisema wanatakiwa kuandika na kuonesha ardhi hiyo wanatumia kwa shughuli gani mfano taasisi za dini na mashirika mbalimbali yanatakiwa kuandika barua baada ya kusoma na kuangalia vigezo vya tangazo hilo.

Waziri huyo alisema hana mamlaka ya kufuta sheria na kubadilisha kanuni wanachotakiwa ni kulipa kodi ya ardhi kulingana na viwango vilivyowekwa ili kuepuka kulipa kodi na riba.

Aliwataka wafuatilie hati za majengo na ardhi kwani kwa wakazi wa Dar es Salaam zipo hati 500 za kielektroniki hazijachukuliwa na hati za kawaida 7,000 ambazo hazijachukuliwa.

Aliwataka pia wachimbaji wa madini wanaomiliki maeneo ambayo wamehodhi baada ya kuwalipa fidia wananchi na kupata leseni za uchimbaji wanatakiwa kulipa kodi za ardhi kutokana na kwamba ardhi hiyo ni ya kwao.

Alisema awamu ya kwanza ameita kampuni, taasisi na mashirika 207 na awamu ya pili orodha ya kampuni zaidi ya 600, hivyo watu wote wanaomiliki ardhi wanatakiwa kulipa kodi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Akizungumza awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Doroth Mwanyika aliwataka watendaji wa taasisi, kampuni na taasisi hizo kulipa madeni.

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kipindi ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi