loader
Picha

Mali zinazotokana na uhalifu kutaifishwa

SERIKALI imesema itaendelea kutaifisha mali zinazotokana na uhalifu ili kuhakikisha hakuna mhalifu anayenufaika na mali hizo. Imesema kuwa adhabu ya vifungo sio njia madhubuti ya kukabiliana na uhalifu badala yake imethibitika utaifishaji wa mali zinazohusiana na uhalifu ndio njia madhubuti.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk Augustine Mahiga wakati akizungumzia maadhimisho ya miaka 10 ya Umoja wa Taasisi Zinazokabiliana na Uhalifu kwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (ARINSA).

Dk Mahiga alisema yapo makosa ya uhalifu ambayo Umoja wa Mataifa (UN) imeyataja kuleta tishio la amani na usalama duniani ambayo ni biashara ya dawa za kulevya, biashara ya binadamu, uhalifu wa mitandao, utakatishaji fedha na ugaidi.

Alisema kupitia maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia leo hadi Juni 14, mwaka huu, yatawakutanisha mawaziri, makatibu wakuu, wanasheria wakuu wa serikali, waendesha mashitaka, wakuu wa upelelezi na viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama wa ARINSA.

Alifafanua kuwa umoja huo ulianzishwa Machi 2009, nchini Afrika Kusini baada ya mkutano uliojumuisha wawakilishi wa taasisi za mashitaka na upelelezi wa makosa ya jinai kutoka nchi tisa za kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Umoja huu sasa una wanachama 16 kutoka Angola, Botswana, eSwatini, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe. Kwa sasa, Tanzania inashikilia kiti cha Urais wa umoja huu kuanzia mwaka 2018 hadi 2020,” alisema Dk Mahiga.

Alieleza nchi hizo zitakutana kujadiliana namna bora ya kukabiliana na uhalifu mkubwa unaovuka mipaka kwa kutumia dhana ya utaifishaji na urejeshaji wa mali zinazohusiana na uhalifu.

Alisema lengo la umoja huo ni kuwa na ushirikiano wa karibu wa kitaasisi baina ya wanachama kwa lengo la kuhakikisha wahalifu hawafaidiki na mali zinazohusiana na uhalifu na hawana mahali pa kujificha katika nchi wanachama.

Rais wa ARINSA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga alisema zaidi ya watu 250 watashiriki kwenye mkutano huo ikiwemo 150 ambao ni wageni.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi