loader
Picha

Spika Rwanda amkubali Magufuli

SPIKA wa Bunge la Rwanda na ujumbe wake wamewaambia wabunge wa Tanzania kuwa utendaji kazi wa Rais John Magufuli unafanana na ule wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, hivyo kazi iliyobaki ni kwa wabunge kunyanyuana.

Akizungumza na wabunge mjini Dodoma baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa, Spika wa Bunge la Rwanda, Donatille Mukabalisa alisema nchi yao imefanikiwa kulipa suala la jinsia kipaumbele na kila bajeti kabla ya kusomwa ni lazima iwe imezingatia masuala ya usawa wa kijinsia.

“Suala la jinsia nchini Rwanda ni la msingi sana ndio maana utaona hata bunge letu asilimia 61.3 ni wanawake na kila bajeti kabla ya kusomwa lazima iwe imezingatia masuala ya usawa kwa sababu nchi haiwezi kuendelea kama kuna kundi linaachwa nyuma hususan wanawake na watoto,” alisema Spika Mukabalisa.

Akijibu swali la baadhi ya wabunge wa Tanzania waliohoji Rais Kagame ametumia mbinu gani kufanikisha usawa huo na Tanzania itawezaje, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Siasa na Jinsia wa Rwanda, Rubagumya Furaha Emma alisema utendaji kazi wa Rais Magufuli unafanana kabisa na ule wa Kagame, hivyo kilichobaki ni kwa watendaji wakiwemo wabunge kunyanyuana.

“Rais Magufuli anafanya kazi vizuri na utendaji wake ni sawa na wa Kagame ambaye anajali watu wake wote wameweka mazingira mazuri, sasa nyie wabunge mna wajibu wa kusaidiana na kuhimizana kuhakikisha masuala ya usawa wa kijinsia yanazingatiwa na sisi ndivyo tunavyofanya wabunge, sio kila kitu afanye Rais,” alisema.

Aliongeza Rais Magufuli amefanya mengi na wao wanaona na kilichobaki ni kuhakikisha mazingira au misingi iliyowekwa ya kusaidia kuleta usawa wa kijinsia inatekelezwa na mihilimi mingine ya dola likiwemo bunge kwa sababu hilo sio jambo la kufanywa na mtu mmoja, bali inahitajika nguvu na ushiriki wa wanaume kufanikisha hilo.

Awali akizungumzia hatua walizochukua nchini Rwanda kufanikisha masuala ya usawa wa jinsia, Spika Mukabalisa alisema tukio baya la mauaji ya Kimbari mwaka 1994, yalisababisha vifo vya watu zaidi ya milioni moja na zaidi ya asilimia 75 ya vifo hivyo walikuwa ni wanawake na watoto, jambo ambalo liliacha picha mbaya na ndio maana Rais Kagame aliamua kundi hilo sasa lipewe kipaumbele kwa sababu wana haki ya msingi kama binadamu wengine.

Alisema nchi hiyo kwa sasa inafanya vizuri kwenye usawa wa jinsia katika ngazi mbali mbali ikiwemo ngazi za maamuzi, mahakamani ambako idadi ya wanawake ni asilimia 49.7 na pia sasa wamefanya mapinduzi kwenye sekta ya mawasiliano na kuhakikisha wanawake na wasichana wengi wanapata fursa za kusoma masomo ya sayansi.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi