loader
Picha

Marekani yaingilia kati mgogoro Sudan

MJUMBE wa Marekani katika Afrika, Tibor Nagy anakwenda Sudan ambako kuna hali tete kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea.

Nagy ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika, anakwenda kuomba kusitishwa mashambulio dhidi ya raia. Kutokana na mgogoro huo, kumekuwa na mgomo wa kitaifa wa wafanyakazi ulioanza Jumapili ukilenga kushinikiza serikali ya kijeshi kutoa fursa ya kuwapo serikali ya kiraia. Watu wanne waliuawa siku ya kwanza ya mgomo baada ya vikosi vya usalama kupiga mabomu ya machozi na risasi za moto.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Wizara ya Mambo ya Nje imesema Nagy ataomba pande zinazokinzana kushirikiana katika kuweka mazingira ya kuendeleza mazungumzo kati yao. Kutokana na hali tete katika baadhi ya miji ikiwamo mji mkuu, Khartoum, maduka, masoko na benki zilifungwa ingawa juzi machache yalianza kufunguliwa.

Maeneo hayo ya kibiashara yalifungwa kutokana na wafanyakazi kuzingatia maagizo ya kikundi cha upinzani; Sudanese Professionals Association (SPA) kilichowataka wasiende kazini. SPA iliitisha mgomo baada ya zaidi ya waandamanaji 100 kuuawa na kundi la kijeshi, Rapid Support Forces (RSF) Juni 3 mwaka huu. Jeshi lilimwondoa madarakani Rais Omar al-Bashir Aprili mwaka huu baada ya maandamano yaliyochukua miezi kadhaa yakishinikiza aondoke madarakani.

Baada ya hapo, baraza liliahidi kwamba utawala utakabidhiwa kwa raia. Wanaharakati wanaounga mkono demokrasia wanasema baraza haliwezi kuaminika kutokana na kushambulia waandamanaji.

Hivyo wamekataa mapendekezo ya kufanya mazungumzo. Shirika la Habari la Reuters limenukuliwa likisema viongozi wa upinzani wameweka mipango ya serikali ya mpito itakayoongozwa na mwanauchumi maarufu nchini humo. Imeelezwa upinzani utamchagua aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Uchumi la Umoja wa Mataifa barani Afrika, Abdullah Hamdouk, kuwa waziri mkuu. Aidha wanapanga kuteua watu wengine wanane wakiwamo wanawake watatu watakaoingia kwenye baraza hilo la mpito.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu ...

foto
Mwandishi: KHARTOUM, Sudan

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi