loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jafo akataa visingizio uchelewaji ujenzi hospitali

SERIKALI imezitaka halmashauri zote zinazojenga hospitali za wilaya mkoani Lindi, zimalize kwa wakati uliopangwa bila kutoa sababu na kusababisha ujenzi wa hospitali hizo kuchelewa zaidi.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo mwishoni mwa wiki wakati alipokagua Hospitali ya Wilaya ya Lindi inayojengwa katika kata ya Kiwalala. Ujenzi wa hospitali hiyo unagharimu Sh bilioni 1.5 zilizotolewa na serikali kuu.

Waziri Jafo alisema katika halmashauri nyingi tayari fedha za ujenzi wa hospitali hizo za wilaya zimeshatolewa, hivyo ni vyema ujenzi wake ukamilike mapema bila sababu zisizo za msingi. Alisema amekuwa akipokea sababu nyingi kutoka kwa wakurugenzi kuhusu kutokamilika kwa wakati kwa ujenzi wa hospitali hizo, jambo ambalo kuanzia sasa hatolikubali tena.

“Unasikia mkurugenzi anakuambia njia ilikuwa haipitiki, mara maji shida, hizi ni baadhi ya sababu nyingi tu ambazo hazina athari ya kusababisha mradi usiishe kwa wakati unaotakiwa,”alisisitiza. Alisema ni lazima majengo saba ya hospitali mkoani humo yakamilike haraka hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, ili wananchi wapate huduma safi na ya karibu ya afya.

“Sitamvumilia mkurugenzi yeyote yule anitolee sababu za ujenzi wa hospitali uchelewe kukamilika, mimi sitamuelewa kabisa,’’ alisema. Pamoja na hayo, Waziri Jafo alionesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea katika hospitali hiyo ya Lindi ambao umefikia katika hatua ya kuezeka bati. Aliimpongeza Mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye kwa kazi aliyoifanya ya kufuatilia hospitali hiyo mpaka kujengwa hapo Kiwalala wilayani Lindi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya, Dismas Masulubu alisema serikali kuu ilishatoa Sh bilioni 1.5 na mpaka sasa zimeshatumika Sh milioni 950. Alisema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza Januari na unatakiwa ukamilike Juni 30, mwaka huu ambapo majengo saba, kati ya 22 ya hospitali hiyo yanayotakiwa kujengwa mwaka huu.

Dk Masulubu alisema majengo hayo saba yanahusisha pia jengo la wazazi, mapokezi, maabara, x-ray, kufulia nguo, upasuaji na jengo la watoto wachanga. Diwani wa Kiwalala, Mohamedi Chilumba alisema tangu kuanzishwa wilaya ya Lindi mwaka 1983 haijawahi kuwa na hospitali ya wilaya.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza rasmi ...

foto
Mwandishi: Kennedy Kisula, Lindi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi