loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mshauri Mkuu ACT - Wazalendo pokea ushauri wangu wa bure

“LEO tumetangaza kujiondoa kwenye CUF tunajiunga rasmi na Chama cha ACT-Wazalendo… Ofi si zote za CUF tumezibadili na sasa zitapeperusha bendera za ACT.”

Ndivyo alivyosema Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), wakati anatangaza uamuzi wa kujiondoa CUF na kujiunga na ACT-Wazalendo. Nimeyakumbuka na kuyarejea haya baada ya jana kusoma katika baadhi ya vyombo vya habari nchini kuwa, wanachama waliohama CUF wamepata vyeo ACT-Wazalendo.

Jana gazeti moja litolewalo kila siku nchini kwa Kiswahili limeripoti kuwa, wakati Tanzania ikijiandaa kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kuelekea mwishoni mwa mwaka 2020, chama chako kipya cha ACT-Wazalendo kimepanga safu mpya ya uongozi.

Katika mpango huo wa safu ya uongozi, Maalim Seif ambaye ana kadi namba 1, unakuwa mshauri mkuu wa chama. Hatua ya chama chenu inakuja miezi kadhaa baada ya wewe kuhamia katika chama hicho ukitokea CUF; chama ulichosema wewe na wenzako kadhaa mmeona ni ‘mzigo’ sasa mmeutua.

Maalim Seif! Wewe ni mwanasiasa mwenye ushawishi katika siasa za Visiwani Zanzibar; umehama na baadhi ya wanasiasa waandamizi waliokuwa wakikuunga mkono na umechukua uamuzi huo baada ya mvutano kati yako na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kutolewa uamuzi wa Mahakama Kuu iliyompa ushindi Lipumba na hivyo, jukumu lake la uenyekiti.

Kumbuka tu, namna mgogoro huo uliokinyemelea CUF ulivyoweka mpasuko baina ya wafuasi wa Profesa Lipumba na wafuasi wako. Kimsingi, pande zote zimekijeruhi CUF. Hata hivyo, kujiondoa kwako katika chama ulichodumu nacho kwa miongo kadhaa, kunatarajiwa kuandika historia mpya katika medani za siasa visiwani Zanzibar na huenda hili likathibitika zaidi katika uchaguzi mkuu ujao.

Hatua yako ya kukihama CUF ni mwendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayoendelea kuzipamba siasa za Tanzania, hivyo japo Watanzania wengi walishituka, lakini hawakushangaa. Kwa upande wao, wanachama wa ACT-Wazalendo, wanauona mwanga mpya wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Kwao, huenda ikawa neema iliyofunguliwa maana chama chako kipya kinaye mbunge mmoja pekee, aliyepatikana katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ambaye ni Kiongozi Mkuu wa cha cha ACT- Wazalendo, Kabwe Zitto.

Huyu ni Mbunge wa Kigoma Mjini. Hivi karibuni aliyekuwa mgombea wa upinzani kupitia Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa alirejea tena chama tawala CCM, katika kile alichosema: “Nimerudi Nyumbani.” Hata hivyo, licha ya tofauti za kawaida na za asili za binadamu, kisiasa wewe na Lowassa bado ni tofauti hasa katika upokeaji wa matokeo katika ‘mashindano’ ya kisiasa.

Wewe, umekuwa na hali ya kutopenda kuridhika na matokeo ya uchaguzi; tangu uanze mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini mwka 1992 na baada ya mashindano (uchaguzi) hayo, matokeo mara nyingi yamekuwa agenda yako ya kudumu katika karibu kila mkutano wako. Kama ilivyo nia njema ya serikali kuhakikisha demokrasia ya vyama vingi inastawi nchini, vyama vya siasa kikiwamo ACTWazalendo, Chadema, CUF na vingine vitoe mchango unaoonekana wakati wa mwanga na hata wakati wa giza, kuhakikisha kunakuwa na demokrasia iliyo makini.

Ikumbukwe kuwa, ili nchi ionekane inastawisha demokrasia, siyo kwamba lazima watu watoke chama tawala na kuhamia vyama vya upinzani; siyo lazima katika uchaguzi, vyama vya upinzani vishinde dhidi ya chama tawala na siyo kwamba lazima wanasiasa waachwe kuugua ugonjwa wa lawama, matusi, visingizio na kukiuka taratibu, kanuni na sheria za nchini bila kuchukuliwa hatua za kisheria; hapana siyo hivyo. Kwa nchi yoyote makini yenye watu na viongozi makini, chama kinachoendekeza migogoro, ubaguzi, ubadhirifu, ukabila, umatabaka, matusi na lugha za uchochezi unaoelekea kutisha amani na usalama wa nchi, kabla ya kukiunga mkono, husikitikiwa na ‘kufanyiwa maombi kwanza.’

Ndiyo maana leo katika Kauli ya Mdadisi ninasema, wewe na viongozi wenzako katika ACT- Wazalendo, mkitaka mafanikio msikubali kusombwa na mafuriko ya siasa za lawama, visingizio, migogoro na matusi dhidi ya viongozi waliochaguliwa kihalali na wananchi. Siku zote mkumbuke na kuzingatia kuwa, unapomtukana kiongozi aliyechaguliwa kihalali na wananchi, siyo kwamba unamtukana kiongozi huyo pekee, bali unawatukana na kuwachokoza Watanzania wote anaowaongoza kwa mujibu wa sheria hivyo, chama husika kijue kinazidi kuongeza urefu wa kaburi lake kinalojichimbia kisiasa.

Katika mchakato wa kisiasa, hasa katika muktadha wa uchaguzi, mwamuzi wa mwisho ni kura ya mwananchi na siyo visingizio lukuki vya kushindwa. Hivyo, kila mmoja aingie katika mchakato akijua kuwa, kutendeka kwa haki siyo tu pale mgombea au chama fulani kinaposhinda, bali hata mgombea huyo au chama chake kushindwa, nayo ni haki yake inayotendeka na kuonekana imetendeka.

Maalim Seif! Mshauri Mkuu ACT-Wazalendo! Naomba kukupa ushauri wangu. Ukipenda upokee na ukipenda ukatae, lakini nakushauri uupokee na kuufanyia kazi ushauri wangu kwa manufaa ya taifa lako, chama chako na kwa manufaa yako mwenyewe. Maalim! Umefika ACTWazalendo, sasa tulia. Badala ya mpambano, sasa anzisha na kuendeleza siasa za kistaarabu, vinginevyo unaweza ‘kumaliza bucha, lakini ukakuta nyama ni ileile.’ Fanya ushauri hasa na siyo kuendelea kuamini kwamba lazima wewe ndiye uwe mgombea urais.

Siyo hilo pekee, bali shirikiana na viongozi wengine wa chama katika ngazi zote, kujenga na kuchochea siasa za kistaarabu; siasa zisizo na ugomvi, wala matusi; siasa zisizo za kutarajia kushinda tu, wakati katika mashindano kuna kushinda au kushindwa. Huko ulikokwenda katika makao mapya ya kisiasa, jenga na kuendeleza utamaduni bora wa kusifia na kuunga mkono mema yanayofanywa na serikali ya chama tawala na panapohitaji kukosoa, kosoa kwa busara na kuonesha njia kistaarabu. Huo ndio ungwana na tiketi bora ya kisiasa.

Pamoja na viongozi na wanachama wengine wa ACT- hakikisheni mnalinda kwanza maslahi ya nchi, na siyo maslahi ya chama maana ACT-Wazalendo, Chadema, na vyama vingine vya siasa vimo ndani ya Tanzania na siyo kwamba Tanzania imo ndani ya ACT-Wazalendo au chama chochote. Fanyeni mapinduzi ya kisiasa ili kila mmoja ndani ya nafasi yake kila wakati ajisemee maneno: “Tanzania kwanza.” Maalim! Wewe usikubali ugonjwa wa kwenda kujikomba kwa “ndugu matajiri” ili “wakugawie nguo, viatu, pipi, au pesa.”

Hilo liepuke. Usiende kuwateta ndugu zako Watanzania kwa mataifa ya jirani ili eti uonewe huruma na kupewa misaada. Maalim! Kama nawe utaugua ugonjwa huo, utapata faida na furaha gani kula kitu kilichopatikana kwa kuusaliti ukoo wako! Hilo liepuke na wakataze wenzako wenye ugonjwa huo katika chama maana siyo siri hilo linawachukiza wengi, na kuwafanya kukichukia chama.

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments