loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nabii Eliya kukamatwa

JESHI la Polisi mkoani Pwani limetakiwa kumkamata mtu anayejiita Nabii Eliya ambaye jina lake ni Hamza Issa anayetuhumiwa kufanya mahubiri ambayo yanaweza kuhatarisha amani kwa jamii.

Aidha, Nabii Eliya ambaye anadaiwa kuwa anawafanyia maombi watu wenye matatizo amewakusanya wanawake wengi ambao ndiyo waumini wake wakuu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alipozungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa Kamati ya Amani ya Mkoa na wadau wa afya juu ya namna ya kupambana na ugonjwa wa dengue.

“Naagiza Jeshi la Polisi kumtafuta popote pale alipo na kuna taarifa zinasema kuwa yuko Mtaa wa Misugusugu akamatwe na ahojiwe juu ya anachokihubiri kwani kuna taarifa kuwa ana mahubiri ambayo yanaweza kuhatarisha amani na utulivu uliopo na anaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema Ndikilo.

Ndikilo alisema kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo vifuatilie suala hilo kwa umakini ili kumbaini mtu huyo anawafundisha nini waumini hao.

“Akishakamatwa na kuhojiwa asimamishwe kufanya shughuli hizo na akikaidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake kwani anaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuleta madhara,” alisema Ndikilo.

Alisema jambo ambalo amelifanya ni kumchukua mke wa mdogo wake akidai kuwa anamtibu, lakini kila wakipigiwa simu hawapatikani ikidaiwa kuwa yuko kwenye huduma. “Anaishi na shemeji yake na mtoto wa mdogo wake wa kiume, lakini anapopigiwa simu ili awarudishe hapatikani kwani mdogo wake anataka mke wake arudi, sasa ikitokea mdogo wake akija huku nini kitatokea, itakuwa ni ugomvi ambao utahatarisha usalama wa watu,” alisema Ndikilo.

Kwa upande wake, Shehe wa Wilaya Kibaha kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Said Mtonda amesema suala la Issa lilianza mwaka mwaka jana ambako alifika na kujitangaza kuwa yeye ni mhubiri wa dini ya Kiislamu na aliomba kutoa mihadhara kwa baadhi ya maeneo ya Kibaha lakini walimkatalia.

Mtonda alisema walikaa naye kwa kina na kutaka kujua anachotaka kuhubiri kwenye maeneo hayo na kuona kuwa mahubiri yake hayaashirii kuleta amani na hayastahili kwenye dini ya Kiislamu na kuachana naye na kumpiga marufuku asifanye shughuli hizo.

Alisema kutokana na kuwa na utovu wa nidhamu, aliendelea kufanya hivyo wakaamua kulipeleka suala hilo kwa Kaimu Shehe wa Mkoa na kugundua kuwa mahubiri yake hayako kwenye utaratibu wa dini ya Kiislamu na ni kama vurugu na baada ya hapo taarifa ilipelekwa kwa Mufti wa Tanzania aliyetoa tamko la kutomruhusu kufanya hivyo, lakini sasa amekuja kwa njia nyingne, kwa kubadili utaratibu na kujifanya Mkristo na kwenda makanisani.

Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye ni Kaimu Shehe wa Mkoa, Hamis Mtupa amesema kuna baadhi ya watu wanajifanya kuja kufanya mahubiri, lakini wana mambo yao mengine hivyo mashehe lazima wawe makini nao.

Mtupa alisema hata Mungu anasema lazima umfanyie utafiti mgeni anayekuja kabla ya kumpa hifadhi ambapo zamani walikuwa wakiruhusiwa kulala miskitini, lakini kwa sasa hali imekuwa ni mbaya.

Alisema ili kukabiliana na watu ambao wanaweza kuleta hali ya uvunjifu wa amani, kuwe na ushirikiano na viongozi wa kamati za ulinzi, viongozi wa dini na wananchi ambao ni raia wema na wageni wanaokuja kwa ajili ya kuhubiri wawe na vibali toka Bakwata na vibali vyote na kujua taarifa zao kwa kina.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza rasmi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Kibaha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi