loader
Picha

Upelelezi kutekwa Dewji haujakamilika

KESI ya tuhuma za kumteka nyara mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu MO inayomkabili dereva teksi, Mousa Twaleb (46) Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilitajwa tena jana na ikaelezwa na upande wa mashitaka kuwa upelelezi haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Dais Makakala alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 25, mwaka huu na mshitakiwa ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, amerudishwa rumande. Twaleb anakabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo kumteka nyara mfanyabiashara maarufu nchini, MO.

Katika mashitaka ya kwanza, inadaiwa mshitakiwa huyo alijihusisha na genge la uhalifu. Inadaiwa Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, 2018, maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na Johannesburg nchini Afrika Kusini, kwa makusudi alitoa msaada wa kutendeka vitendo vya jinai au uhalifu wa kupangwa ili kujipatia faida.

Pia inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, akiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumweka maeneo ambayo ni hatari.

Pia inadaiwa Julai 10, mwaka jana Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha, Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

MO alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART), Robert Kisena (46) na wenzake wanne wanaokabiliwa na mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ya kuisababishia serikali hasara wanaendelea kusota rumande kwa sababu upelelezi wake haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizire kesi hiyo ilikuja kutajwa na upelelezi haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Rwizire aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana kisheria.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi