loader
Picha

Wakandarasi kunyang'anywa pasipoti

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko kushikilia hati za kusafi ria za wakandarasi watatu kutoka Kampuni ya Angelique International Ltd ya India inayotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA) mpaka pale watakapokamilisha kazi hiyo.

Wakandarasi hao wanaoshikiliwa na Polisi ni Dilip Patra, Dilip Sighn na Ramashakur wote raia wa India waliosaini mkataba wa muda wa miezi sita na kutoonekana eneo la kazi muda wa miezi miwili mfululizo.

Dk Kalemani aliagiza hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Namba Tano katika Kata ya Mwakitolyo katika Halmashauri ya Wilaya Shinyanga, ambako alitoa Umeta 50 bure na kuwaeleza wananchi kuwa waondoe wasiwasi vijiji na vitongoji vyote vitapatiwa nishati ya umeme kwani serikali imekwisha toa kiasi cha Sh bilioni 36 mkoani Shinyanga kutekeleza mradi.

Alimwagiza DC Mboneko kuhakikisha wakandarasi hao wanafuatiliwa na pasipoti zao kushikiliwa na kutoruhusiwa kuondoka hadi watakapokamilisha mradi huu Desemba katika vijiji na vitongoji vyote.

“Mkandarasi anasuasua na baadhi ya vijiji kurukwa wakati vimo kwenye orodha ya kupatiwa umeme. Wananchi changamkieni fursa hii. Leo nimekuja rasmi kuangalia kazi inavyoendelea. Nilipata taarifa mkandarasi hayupo saiti wakati mkataba alisainishwa, akaenda kwao India aliposikia nakuja kufanya ziara naye ndiyo karudi,” alieleza Dk Kalemani.

Alimtaka afanikishe kazi hiyo kwani eneo la Mwakitolyo lina wachimbaji wengi wanaohitaji nishati hiyo ili walipe vizuri mapato ya serikali hivyo urukwaji wa vijiji utawafanya wananchi kuja kupata gharama kubwa kupewa umeme wa Tanesco kwa Sh 580,000 badala ya REA kwa Sh 27,000.

Aliwaeleza wakandarasi kuwa vijiji au vitongoji vitakavyorukwa watavirudia kuweka nishati ya umeme kwa gharama zao, kwani mkataba wamesaini vitongoji na vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga vipate umeme vyote Desemba mwaka huu na halmashauri zilipie taasisi, shule na zahanati.

Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum alimweleza waziri wakandarasi wanafanya kazi polepole tangu wapatiwe mkataba na wameruka baadhi ya vijiji kama cha Pandagichiza.

Alisema ingawa hii ni awamu ya tatu, vitongoji 13 vilikuwa kwenye orodha awamu ya kwanza, lakini vilivyopata ni vitatu.

“Upatikanaji wa nishati ya umeme ni fursa katika utoaji ajira kwa wananchi, lakini tunashangaa awamu ya tatu vijiji 54 vilivyoorodheshwa kupata nishati ya umeme wa REA, lakini mkandarasi anasuasua tangu aliposaini mkataba ikiwa Kata ya Mwalukwa imerukwa pia ambayo ilikuwa kwenye orodha haijapata umeme hata kijiji kimoja na Kata ya Iselamagazi Kijiji cha Mwambasha kimerukwa,” amesema Salum.

BENKI ya NMB imezindua 'NMB Afya loan', ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy, Shinyanga

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi