loader
Picha

Viongozi wakifuata nyayo za JPM taifa litafika mbali

IJUMAA iliyopita wakati mkutano baina ya Rais John Magufuli na wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini na wajumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) ukiendelea, kuna watu waliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Mmoja akaandika: “Kutazama mkutano huu ni zaidi ya kuangalia mpira baina ya Barcelona na Real Madrid.” Mwingine naye akasema: “Yaani, Rais wangu amenikosha sana kwa huu mkutano.

Ni mtamu sana kuuangalia.” Wakati nikipitia mara moja moja kinachotokea katika mkutano huo kwa kuwa nilikuwa na majukumu mengine, nilikuwa ninajiona kama ninapitwa na mengi. Ndiyo maana pamoja na kufuatilia habari katika runinga usiku huo, Jumamosi nilikuwa mmoja wa waliowahi kwenye mbao au meza za kuuzia magazeti.

Bila shaka mkutano huo umempatia Rais Magufuli majibu mengi kuhusu matatizo na adha mbalimbali wanazopata wafanyabiashara na hasa baada ya yeye mwenyewe kuwa wazi na kutaka uwazi utawale katika mkutano wake kwa asilimia 100.

Na kweli hilo lilifanyika. Wakati Rais na watendaji wanaomsaidia wakikuna vichwa kushughulikia changamoto za wafanyabiashara hao ambao ni wadau muhimu katika maendeleo ya nchi yetu kama zilivyojitokeza, nimekuwa nikijiuliza viongozi wengine kuanzia kaya hadi wizara wanajifunza nini kutoka kwa Rais angalau katika hili?

Je, wale ambao wamekuwa na kawaida ya kupinga kila kitu kinachofanywa na rais bado wameshindwa kuona nia thabiti ya kulisukuma Taifa letu aliyo nayo Rais Magufuli, hata kupongeza tu hili ili kumtia nguvu? Wakati Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku (Msukuma) aliposema kwamba aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, alikuwa hajulikani kwa wafanyabiashara wengi, kuna watu wamekuwa wakiona kama mbunge huyo aliamua kumfanyia ‘kitu mbaya’ Kakunda.

Kuna mmoja alisema: “Yaani Msukuma ambaye anakutana na Kakunda kila siku bungeni anasema hajulikani (kwa maana ya kwamba naye hamjui?)” Huyu aliona kana kwamba hoja hiyo ilipaswa kutolewa na mfanyabiashara mwingine. Kimsingi, alichokuwa akimaanisha Msukuma ndicho msingi wa makala haya; kwamba, kama kiongozi hakutani na watu unaowaongoza watawezaje kumfahamuje? Ukweli ni kuwa, kama hukutani na watu unaowaongoza, huwezi kujua na hatimaye kutatua matatizo na changamoto zao.

Kwa lugha nyingine, Msukuma anasema nchi yetu ina shida kubwa kwa viongozi kiasi kwamba, hawafiki kwa wananchi. Kwamba, wakishachukua madaraka, hujifungia ofisini na unaweza kuwaona tu kwenye mialiko ya kuzindua warsha, semina na mikutano.

Je, viongozi wetu wa ngazi mbalimbali wanachukua hatua gani za kuwasiliana na wale wanaowaongoza? Je, wawakilishi wa wananchi kama vile wabunge na madiwani wanakutana mara kwa mara na wananchi kupeleka kwa watunga sera hoja zao au wanajiwakilisha wenyewe bungeni? Miongoni mwa vitabu vya dini, vipo vinavyofundisha kwamba “kila mchunga (kiongozi), ataulizwa mbele ya Mahakama ya Mwenyezi Mungu kwa kile alichokichunga (watu anaowaongoza).”

Je, sisi wachunga wa ngazi mbali, hata hapa duniani tukiulizwa tuna majibu sahihi kuhusu wale tunaowachunga? Sikumbuki huu wa Jumamosi ulikuwa ni mkutano wa ngapi kufanywa na Rais John Magufuli kwa makundi mbalimbali ya Watanzania. Ninazo kumbukumbu kwamba, Rais alishakutana na viongozi wa dini, alishakutana na wachimbaji madini, wazee wastaafu na hii ni mara ya pili kukutana na wafanyabiashara.

Mara zote alipokutana na haya makundi maalumu, Rais wetu hakuteka kikao kwa kuzungumza yeye anayotaka kusema, bali amekuwa akiacha uwanja mpana kwa watu aliowaita kutema kila nyongo waliyo nayo kwenye mioyo yao ili kujenga. Je, viongozi wengine mmeshindwa hata kuiga hilo hadi unakuta wadau muhimu katika sekta, wizara, wilaya, mkoa au kada yoyote mnazoziongoza wala hawawajui? Alichokuwa anasema Msukuma kwa lugha nyingine ni kwamba, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara alipaswa kuwa amechukua mapema hatua kama alivyofanya Rais.

Kwamba, ingawa amekuwa katika wizara hiyo kwa kipindi kifupi, ilitarajiwa awe ameshakutana na makundi ya wafanyabiashara, kama si kuwaita wote Dar es Salaam, basi hata katika kata, tarafa, wilaya, mikoa au katika kanda zao. Ninachotaka kuwakumbusha viongozi wengine hapa ni kuiga jambo hili jema la kukutana na wale wanaowaongoza mara kwa mara katika ngazi na kada zao kusikia hoja na changamoto na mawaidha. Wakati fulani nilimsikia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akimsifu waziwazi Mkuu mwenzake wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel kwa jinsi anavyosimamia na kutumia mapato yanayofanywa na wawekezaji kwa halmashauri katika mkoa wake.

Akasema atakwenda kujifunza kwa kuwa ni jambo jema. Jambo likiwa jema, hata kama linafanywa na mtu usiyempenda ni busara kujifunza na ikibidi, kupongeza. Katika jamii yetu kuna viongozi vijana wanaotazamia kuendelea kwa miaka hata zaidi ya 30 kama Mwenyezi Mungu atawajaalia uhai, kudumu katika uongozi. Unaweza kukuta wana matarajio hayo ya kudumu katika uongozi, lakini hawajifunzi mambo muhimu yatakayofanya wananchi ili waendelee kuwachagua na kuwapenda likiwemo hili analofanya Rais Magufuli la kukutana na makundi ya watu anaowaongoza pamoja na suala zima la uadilifu na kutenda haki.

Ni vyema sasa kila ‘mchunga’ akawa anafanya vikao vya mara kwa mara na wananchi wake, na asihodhi mkutano, bali aachie wajumbe wafunguke huku akiwahakikishia uhuru wao wa ‘kutapika nyongo’ alimradi wanachokisema wana uhakika nacho, wana ushahidi na hawalengi kumhujumu yeyote. Yaani uwe ni mkutano ambao kila anayeufuatilia hata kama hauonekani kwenye runinga, basi ajione kwamba mkutano ule ni bora kuliko hata kutazama mechi baina ya Yanga na Simba.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi