loader
Picha

Chozi kupata mtoto baada ya miaka 20

“NILIOLEWA nikiwa na miaka 20. Baada ya ndoa, mimi na mume wangu tulitumia kila njia kutafuta mtoto bila mafanikio. Leo ni mwaka wa 20; natoa chozi la furaha baada ya kupokea mtoto katika mikono yangu, hatimaye tumepata mtoto, Mungu ni mwema amejibu maombi yetu.”

Ndivyo anavyosema Ekilia Chiteto (40) aliyeolewa mwaka 1999 jijini Dar es Salaam.

Ekilia sasa ni mama wa mtoto wa kike mwenye umri wa miezi mitano. Anaelezea safari yake ya kukata tamaa na kisha, kupata matumaini kupitia majawabu ya Mungu, baada ya imani na maombi yake na familia kwa jumla.

Ekilia anasema pamoja na changamoto hiyo kubwa aliyopata katika maisha yake, imani yake kwa Mungu haikuondoka na kkwamba, ndiyo imemfanya leo kubeba mtoto katika mikono yake kama wanawake wengine katika ndoa.

Anasema safari ya kutafuta mtoto yeye na mumewe Lukelo Jonas, iliwafikisha katika kutumia njia nyingi ikiwemo kutumia dawa za asili, kwenda kwa waganga wa kienyeji na tiba za hospitali, lakini hawakufanikiwa kwa muda wote huo.

“Baada ya kupita miaka mitano ya ndoa bila kuona dalili za kupata mtoto, tulienda hospitali, nilianza mimi, nilijitahidi kuhangaika kutafuta mtoto kwa sababu unajua mwanzoni, wanawake huwa tunakuwa na hofu zaidi tunapokosa mtoto katika ndoa,” anasema.

Anasema alikwenda kwa kila daktari ambaye aliyesikia anasaidia wanawake kupata mtoto, baadaye alifika kwa daktari mmoja na alipomfanyia vipimo, alimwambia hana tatizo lolote. Hata hivyo licha ya daktari huyo kumpa dawa, alimpa dawa za homoni na za kupevusha mayai.

Hata hivyo, licha ya kuzitumia kwa zaidi ya miezi sita, hawakufanikiwa kupata mtoto.

Baada ya kuona hakuna mafanikio, anasema daktari huyo alimhamishia kwa mwenzake akimwambia kuwa huyo pia ni mtaalamu na ana vipimo zaidi.

Anasema alikwenda na kufanya vipimo pamoja na kusafisha kizazi, lakini bado hakupata matokeo aliyotarajia.

“Kwa huyu daktari nilikwenda karibia mwaka mzima, nikapewa dawa kibao na kusafishwa kizazi, hakukua na lolote, nilianza kuchoka kwa kweli,” anasema.

Ekilia anasema aliamua kumshirikisha mumewe kwenda hospitali, walipimwa wote na kuonekana hawana tatizo. Hata hivyo, daktari aliwapa dawa alizowaeleza kuwa zitawasaidia.

Baada ya vipimo na dawa kutumia yeye na mume wake, Ekilia anasema hakurudi tena hospitali na badala yake, akaamua kumgeukia Mungu kwa ‘kuokoka’ na kuanza maisha mapya na kuzidi kumuomba Mungu.

"Mwanzoni haikuwa rahisi, maana mimi niliokoka, lakini mume wangu alikuwa hajaokoka, changamoto ziliendelea lakini nashukuru Mungu hatukufikia kuvunja ndoa. Mwaka mwaka 2012, mume wangu naye akaokoka,” anaeleza Ekilia.

Anasema wazo la kutafuta mtoto walilifuta wakiamini kuwa, huenda wamepangiwa na Mungu kuishi bila mtoto wa kumzaa wao.

Wanandoa hao wakaamua kuchukua mtoto wa ndugu na kuishi naye wakimpa mapenzi yote kama mtoto wao wa kuzaa.

Ekilia anasema Mwaka 2017, ghafla katika mazungumzo, mume wake alimwambia amemuomba Mungu ampatie mtoto.

"Nilipuuza yale maneno yake kwasababu mimi nilishaamini kwamba haya ndiyo maisha tuliyopangiwa na Mungu.”

Mwaka 2018 bila kutarajia alihisi hali ya ujauzito ingawa alikuwa hajawahi kushika mimba, lakini alihisi hali ile ni mimba.

Anasema: “Nilikua nimezoea wakati mwingine sioni hedhi mwezi au miezi miwili, lakini safari hii ilipita miezi mitatu nikashtuka. Pia, nikaona tumbo gumu, lakini nilikuwa sitapiki wala siumwi. Nikadhani labda ni uvimbe, nikaanza kusikia pia kitu kinacheza tumboni,” anasema Ekilia.

Anaongeza kuwa, hakumwambia mume wake mabadiliko hayo katika mwili wake na wala hakwenda hospitali kupima wakati huo. Baada ya miezi mitano anasema, aliamua kwenda hospitali kupima.

Akamwambia daktari kwamba, anaumwa tumbo na pia amesimama hedhi kwa miezi kadhaa. “Daktari akasema kwa umri huu, wamama wengi huwa wanakoma hedhi, nikashituka nikasema huyu daktari nae anaongea nini na mimi nimeshaamini nina mimba, akaniambia nifanye kipipimo cha ultrasound.”

Anasema: “Mtu aliyenipima, naye akanipokea kwanza kwa utani, lakini baada ya kupima aliniambia mbona ni mjamzito…. Akaniambia tazama hapa mtoto mkubwa kabisa. Sikuweza kuangalia, nililia tu ilikuwa ni furaha kubwa mno kwangu,” anasema Ekilia huku machozi yakionekana katika macho yake.

Anasema wakati mpimaji akimuonesha mtoto kwenye kipimo kile, hakutaka kutazama, na alipomwambia kwamba hajawahi kupata mtoto katika maisha yake alishituka na baadaye, akamtolea majibu na picha ndogo.

Akamwambia akamuoneshe na mume wake ili aamini. Ekilia anasema alipofika nyumbani alimuonesha mumewe majibu bila kuzungumza kitu.

"Akakimbilia kwenye picha akauliza ni nini hii? Nikamwambia ni mtoto wako, akashangaa akakaa chini".

Anasema kitu pekee alichokisema mumewe ni: "Kweli kama mtu kukata tamaa mimi nilishakata tamaa."

Anasema baada ya mazungumzo hayo hawakuzungumza kitu tena kuhusu suala hilo kwa siku hiyo.

Ekilia alianza kliniki na kupata chanjo zote, hakupata usumbufu wowote wa mimba mpaka alipofikia wakati wa uchungu wa kujifungua.

Anasema nyumba yake ilijaa furaha baada ya ujauzito huo na mume wake, dereva wa daladala alikuwa kila akirudi nyumbani usiku, anakwenda kuzungumza na mtoto tumboni.

Hata hivyo, anasema mumewe alitamani Ekilia asijifungue kwa upasuaji.

Anasema alipohisi dalili ya uchungu, alikwenda hospitali na baada ya kupokelewa, daktari alimshauri asijifungue kwa njia ya kawaida, bali afanyiwe upasuaji ili kumuokoa yeye na mtoto kwa kuwa umri wake ni mkubwa na hajawahi kujifungua.

“Wakasema mama haiwezekani utatusababishia kesi, wakampima na kusema ndio kwanza njia imefunguka senti mita moja, baadaye wakasema tatu, wakanibembeleza sana pale kwenye kitanda cha vipimo wakinishawishi, nikakataa kabisa nikasema Mungu aliyenipa huyu mtoto, atanisaidia nitajifungua kawaida,” anasema.

Anasema walipomfikisha chumba cha kujifungulia huku wakiendelea kumshawishi afanyiwe upasuaji, hakukubali hata alipohisi hali ya kujifungua bado.

“Nikaamua kusukuma mwenyewe mtoto, wakashangaa najifungua, baada ya mtoto kutoka namsikia analia, nililia kwa furaha kubwa. Mungu ni mkubwa sana sikuamini, sasa nina mtoto, saa sita mchana wa Desemba 3 mwaka jana, tukapata mtoto,” anasema Ekilia huku akifuta machozi.

Anasema katika vitu ambavyo hatavisahau ni siku ya kwanza aliyomwambia mume wake wakapime kujua kwanini hawapati mtoto, mume wake akakasirika na kuona kama amemuona yeye ndiye mwenye tatizo, kwa hasira akamjibu waende.

“Alinitembeza kutoka mabibo mpaka jangwani kwa miguu tunakwenda Muhimbili, hii sitaisahau alikuwa anaongea njia nzima,” anasema.

Mwanasaikolojia tiba, Saldin Kimangale, anasema tatizo la mtu kukosa mtoto kwa muda mrefu inaweza kumuathiri mtu au isimuathiri inategemea na msukumo kutoka kwa familia au mume.

“Hali zote mbili zinategemea ‘pressure’ kutoka kwa mume, ndugu wa mume, hamu yake yeye mwenyewe na matarajio yake na pia watu waliomzunguka,” anasema mwanasaikolojia.

Anasema iwapo kuna msukumo mkubwa itamsumbua kwa sababu kuna kukataliwa kisaikolojia, kutakuwa na ukatili wa kihisia na maneno, kutengwa na kunyanyapaliwa na kuna kupoteza ujasiri na kujiamini.

Anasema katika mila hasa za kiafrika kupata mtoto katika ndoa kunaongeza usalama wa ndoa na mahusiano ya kifamilia na kinyume chake inaweza kusiwe na furaha katika ndoa na wakati mwingine ndoa kuvunjika.

“Iwapo mwanamke atakosa mtoto kisha akakosa kutiwa moyo anaweza kupata msongo wa mawazo na hata sonona jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yake,” anasema.

Daktari Bingwa wa Mfumo wa Uzazi kutoka Hospitali ya Kairuki, Clementina Kairuki anasema ndoa nyingi hutarajia kupata mtoto muda mfupi baada ya kufungwa.

Anasema watu wanapoanza maisha ya ndoa wanakuwa na asilimia ndogo ya kukosa mtoto lakini miaka inavyozidi kwenda uwezo wao hupungua wa kupata mtoto hata hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi wote wawili kujua sababu ya kuchelewa au kukosa mtoto.

Anasema kwamba wanawake ni wepesi kutafuta msaada wa hospitali kwenda kupima na kutafuta suluhisho tofauti na wanaume.

“Kuna asilimia 15 ya watu wanaoishi pamoja na kushiriki tendo la ndoa vizuri katika siku zinazotakiwa lakini hawapati mimba lakini wanawake wanaongoza kwa tatizo hilo,” anasema.

Anavitaja vitu ambavyo vinaweza kumfanya mwanamke kukosa au kuchelewa kupata mimba kuwa ni pamoja na kuwa na tatizo kwenye mirija ya uzazi, homoni kutokukaa sawa pamoja na uvimbe katika kizazi.

Kwa upande wa wanaume tatizo hilo huchangiwa na ubora wa mbegu ambayo inabeba vitu vingi, umbile la mbegu, kasi yake katika kutoka, kiwango cha mbegu zinazozalishwa pamoja na maradhi mbalimbali.

“Pia kuna mambo kama joto lililokithiri linaweza kuathiri mfumo wa uzazi na mbegu zinazozalishwa zinaweza kuwa chache,” anasema. Shirika la Afya Duniani (WHO) linatambua tatizo la uzazi kuwa ni janga.

Hivi karibuni katika maadhimisho ya siku ya kupinga na kuzuia ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi