loader
Picha

Mashindano ya afya yazaa matunda

MASHINDANO ya afya na usafi wa mazingira yanayofanyika kila mwaka tangu 1988, yamechangia kupunguza magonjwa ya kuhara kutoka wagonjwa 1,300,000 katika mwaka 2014 hadi 70,000 katika mwaka 2018.

Akizungumza wakati wa kuzindua mashindano hayo jijini hapa jana, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alisema yameongeza hali ya afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya kaya na katika taasisi. Alisema mashindano hayo, pia yameongeza kazi ya kujenga madampo ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Arusha, Kigoma na Mtwara na na machinjio katika miji mbalimbali nchini.

“Kutokana na mshindano hayo, ujenzi wa vyoo bora umeongezeka kutoka asilimia 34.5 mwaka 2014 hadi 55 mwaka 2018, wakati unawaji wa kutumia maji na sabuni umeongezeka kutoka asilimia 11 hadi 19.4 katika kipindi hicho,” alisema. Dk Ndugulile alisema vijiji vinavyotumia vyoo bora kwa asilimia 100 vimeongezeka kutoka 1,300 katika hadi kufikia 4,000, vile vile shule za msingi zinazotumia vyoo bora zimeongezeka kutoka asilimia 38 hadi 89.5.

Alisema mashindano ya mwaka huu baada ya kuongeza vipengele viwili vya ofisi ya makatibu tawala wa mikoa na taasisi ya kibenki, yatahusisha makundi 12 ambapo kila kundi litatoa washindi watatu wa kwanza, pili na tatu ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia gari na wengine kupata pikipiki pamoja na zawadi nyingine.

Dk Ndugulile alisema katika mashindano ambayo kamati ya kitaifa ya mashindano inajumuisha wajumbe kutoka taasisi, wizara na idara za serikali, yatahusisha halmashauri zote 184 nchini, yakiwemo majiji manne na manispaa 21 na halmashauri za miji 21 nchini.

Pia, kutakuwa na mashindano kutafuta kijiji bora, hospitali za rufaa za mikoa, za rufaa za binafsi, hoteli, shule za msingi na sekondari za bweni, shule binafsi za sekondari za bweni pamoja na ofisi za umma. Dk Ndugulile alizipongeza halmashauri za Njombe, Iringa, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro kwa kuongoza katika usafi huo kwa muda mrefu akaomba halmashauri nyingine ziige mfano huo.

Mratibu wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima alizitaja halmashauri ambazo zimefanya vizuri katika masuala ya usafi kwa miaka mingi iliyopita, kuwa ni pamoja na Iringa, Arusha na Moshi. Mashindano ya mwaka huu ya afya na usafi wa mazingira kwa mwaka 2019 yamezinduliwa rasmi na kilele chake kitakuwa Novemba mwaka huu.

BENKI ya NMB imezindua 'NMB Afya loan', ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi