loader
Picha

Ijue teknolojia ya kibao cha kufulia nguo

PAMOJA na maendeleo makubwa ya kiteknolojia ulimwenguni, jamii ya Watanzania hasa wanawake ni miongoni mwa watu wenye uzoefu wa kusisimua kuhusu muda na nguvu wanazotumia kufua nguo kwa mikono.

Uzoefu huo wa karne na karne kwa baadhi ya maeneo, umeanza kusahaulika kutokana na matumizi ya mashine za kufua nguo na ugunduzi wa njia rahisi ya kufanya kazi hiyo.

Moja ya teknolojia mpya ni ya kibao cha kufulia nguo za aina zote iliyoletwa nchini Tanzania na raia wa Japan, Okamoto Ryuta. Teknolojia hiyo inaweza kuwakomboa wanawake wengi na watoto katika kazi ya kufua kwa kutumia mkono na kupunguza muda mwingi wa kufanya kazi hiyo.

Ryuta kwa taaluma ni Ofisa Maendeleo na anafanya kazi katika Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma kwa kujitolea kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA). Anasema teknolojia ya kufua nguo kwa kutumia kibao ilianzia katika Bara la Ulaya kisha ilikwenda nchini Japan barani Asia. Hata hivyo, anasema alijifunza kutumia teknolojia hiyo kutoka kwa bibi yake nchini Japan na bado anatumia hadi leo.

“Wanawake na watoto wengi katika Tanzania bado wanafua nguo kwa kutumia mkono, naamini wakitumia kibao hiki kitawarahisishia sana kazi ya kufua kwa muda mfupi bila kutumia nguvu na kuchoka,” anasisitiza Ryuta.

Anasema amefika Songea kutokea nchini Japan tangu Mei 2018 na anajishughuli-sha na miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa kutengeneza jiko sanifu la kupikia linalotumia kuni kidogo na muda mfupi wa kupika.

Mintarafu mradi wa teknolojia ya kibao cha kufulia, Ryuta anashirikiana na Kitengo cha Useremala cha Chuo cha Ufundi (Veta) Songea. Wanatengeneza vibao hivyo na kuviuza kwa wananchi kwa gharama nafuu hali iliyosababisha wanawake wengi kuvinunua. “Teknolojia ya kibao hiki inakuwezesha kufua nguo moja kwa nusu dakika. Kwa Tanzania, hii ni teknolojia mpya hivyo haijafahamika vya kutosha kwa watu wengi.” “Songea ndiyo sehemu ya kwanza kutumika. Ukweli kibao hiki ni ukombozi katika familia,’’ anasema Ryuta.

Anasisitiza kuwa kila mahali walipopeleka vibao hivyo wamevifurahia na kununua na kwamba, yeyote aliyetumia kibao hicho kufua nguo, hawezi kuacha kutumia kwa kuwa kinarahisisha kazi na kuokoa muda. Mwalimu wa Kitengo cha Useremala katika Chuo cha Veta Songea, Fabius Mchami anasema wanashirikiana na Ryuta kutengeneza vibao hivyo.

Mchami anasema moja ya shughuli zinazofanywa na Veta Songea kwa sasa ni kutengeneza kibao cha kufulia nguo za aina zote. Anasema kibao hicho hutengenezwa kwa ubao maalumu unaotokana na miti ya kupandwa aina ya “mbolea” yenye sifa ya kutopinda, kutooza na kutoharibika hata ukiingizwa kwenye maji. “Ubao huu huwekwa matuta maalum yanayotumika kufulia, umbali kutoka tuta moja hadi lingine ni sentimeta moja,” anasema.

Anazidi kufahamisha akisema: “Matuta hayo huwezesha kufua na kukamua nguo, kitendo hicho kinawezesha nguo yako kutakata kwa muda mfupi na kwa urahisi.” Anasema katika chuo cha Veta Songea, kazi ya kutengeneza vibao hivyo inafanywa na wanachuo wanaosomea kozi ya useremala na kwamba, kibao hicho kinapendwa sana na familia kutokana na kurahisisha kazi ya kufua.

Mwalimu wa useremala chuoni hapo, Hawa Mosha anasema tangu waanze kutengeneza vibao hivyo, watumiaji wakubwa ni wanawake na watoto wao. Kwa mujibu wa Hawa, kwa kutumia kibao cha kufulia nguo, mtoto wa kuanzia miaka minne anaweza kufua nguo zake vizuri yeye mwenyewe kwa sababu wakati anafua anakuwa ni kama anacheza kumbe anafua nguo.

Anasema hii na tofauti na kufua kwa kawaida bila kutumia kibao hicho kwani mtoto wa miaka minne hawezi kufua na kutakatisha nguo zake. Anashauri kila familia hununua kibao hicho ili kuwafundisha watoto kufua tangu wakiwa wadogo. Mwalimu Hawa anafahamisha kuwa, kibao hicho kinapendwa na wanafunzi katika shule za msingi kwa sababu wanaweza kufua nguo kwa urahisi kuliko kufua kwa mikono.

“Familia isione ugumu wa kupata hiki kibao ni mkombozi kwa wanaume ambao hawajaoa kwa sababu hawatakuwa na sababu tena ya kupeleka nguo zao kwa madobi’’, anasisitiza. Mwanafunzi wa Veta Songea, kitengo cha useremala, Jacob Challe, anasema wanatengeneza vibao hivyo na kuviuza kwa gharama nafuu. Anasema katika maonesho ya bidhaa waliofanyia wilayani Mbinga mkoani Ruvuma walikwenda na vibao 50 vya kufulia na ndani ya muda mfupi waliviuza vyote na wateja wakuu walikuwa ni wanawake.

Akizungumzia namna kibao hicho kinavyofanya kazi, Challe anataja vitu muhimu vya kuandaa kabla ya kuanza kufua kuwa ni sabuni ya kipande au unga, maji kwenye ndoo na beseni. “Mtumiaji atapaswa kuchukua kibao na kukiingiza ndani ya chombo chenye maji kisha kuanza kupitisha nguo juu ya kibao, ndani ya sekunde 30 nguo inakuwa imetakata kisha inasuuzwa na kuanikwa,” anasema Challe.

Evodia Joseph, mwanamke aliyetumia kibao hicho kufulia anasema tangu alipoanza kutumia kibao hicho, anafua nguo nyingi kwa muda mfupi bila kutumia nguvu nyingi. Anasema anatumia muda mfupi kwa kazi kubwa na anaona teknolojia hii ni mkombozi kwa jamii hasa wanawake kwa kuwa shughuli nyingi za familia zinawategemea. “Kwa kutumia kibao hiki, ninapofua nakuwa kama nacheza tu, sichoki wala mikono haiumi. Kibao hiki ni ukombozi kwetu akinamama. Kabla ya kibao hiki kazi ya kufua kwangu ilikuwa ni kama kulima kwa jembe la mkono, lakini sasa ni kuteleza tu’’, anasisitiza Evodia. Ni dhahiri kwamba, teknolojia kama hizi ni muhimu kwa maendeleo ya jamii za Kitanzania, haipaswi kubaki Songea bali isambae nchini kote na kuwanufaisha Watanzania wengi. Albano Midelo ni mchangiaji katika gazeti hili. Anapatikana kwa baruapepe:albano.midelo@ gmail.com, simu 0784765917

Afrika ni bara lililobarikiwa kuwa na maliasili nyingi, ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi